Ndugu wafanyakazi na wadau wa hifadhi ya jamii,
Nawashukuru kwa kushiriki mkutano huu wa mtandaoni (online meeting) wenye ajenda moja ya kupokea maoni ya kuwezesha kuwasilishwa kwa Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Hifadhi ya Jamii kwa hati ya dharura kurejesha fao la kujitoa.
Toka juzi tarehe 3 Agosti 2012 nilipotoa taarifa kwa umma ya kueleza kusudio la kuwasilisha muswada husika katika mkutano wa Bunge unaoendelea nimepokea mwito wa wafanyakazi wa baadhi ya migodi nchini kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini kwenda kwenye migodi husika kwa ajili ya kupokea maoni. Aidha, kufuatia kusudio hilo yametolewa pia maoni na wafanyakazi wa sekta nyingine katika Jimbo la Ubungo na maeneo mengine nchini kwenye mitandao ya kijamii na kupitia simu kuhusu haja ya kukusanya maoni kuhusu muswada husika.
Mkutano huu ni mwanzo wa mchakato wa kuitika mwito huo na kuzingatia maoni yaliyotolewa na tutaelezana ratiba ya ukusanyaji wa maoni ya ziada kupitia mikutano na njia nyingine za mawasiliano kwa ajili ya kufanikisha azma husika kwa haraka.
Ikumbukwe kuwa tarehe 03 Agosti 2012 kwa mujibu wa Kanuni ya 68 (7) ya Kanuni za Kudumu za Bunge na kwa kuzingatia kuwa marekebisho yamefanyika kwenye ratiba ya bunge ambapo Mkutano wa Bunge sasa umepangwa kuahirishwa tarehe 16 Agosti 2012 na hoja za wabunge zimeondolewa kwenye ratiba.
Niliomba muongozo ama Serikali itoe kauli bungeni ya kutengua tangazo lililotolewa na Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) ili kuwezesha mafao ya kujitoa kuendelea kutolewa au uongozi wa Bunge uruhusu niwasilishe muswada binafsi wa sheria kwa hati ya dharura tarehe 16 Agosti 2012 kwa ajili ya kufanya marekebisho kwenye sheria husika ili kuruhusu mafao ya kujitoa kuendelea kutolewa.
Irejewe kuwa pamoja na hatua hiyo ya kuomba muongozo nilichukua hatua ya ziada ya kumwandikia Katibu wa Bunge kumweleza kusudio la kuwasilisha Muswada Binafsi wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Sheria za Hifadhi ya Jamii (The Social Security Laws (Ammendments) Act wa mwaka 2012 kwa hati ya dharura kwa mujibu wa Kanuni ya 81 ya Kanuni za Kudumu za Bunge (Toleo la Mwaka 2007).
Lengo la Muswada huo ni kufanya marekebisho yenye kuwezesha kurejeshwa kwa fao la kujitoa (withdrawal benefits) ili kuruhusu kuendelea kutolewa kwa mafao kwa mwanachama wa mfuko ya hifadhi ya jamii anapoacha kazi na kuhitaji kupewa mafao yake kabla ya kufikisha umri wa kustaafu kwa hiari (miaka 55) au kwa lazima (miaka 60) au pale anapopata ulemavu wa kudumu.
Katika mkutano wa leo, pamoja na mambo mengine napendekeza maoni yatolewe kuhusu masuala yafuatayo:
Mosi, kuhusu taarifa ya Serikali kuwa marekebisho kuhusu kusitisha fao la kujitoa yamefanyika ili kutimiza lengo na madhumuni ya Hifadhi ya Jamii ambayo ni kuhakikisha kuwa Mwanachama anapostaafu anapata mafao bora yatayomwezesha kumudu hali ya maisha uzeeni.
Pili, kwamba mchakato wa marekebisho hayo ulihusisha wadau kwa kuzingatia utatu yaani wawakilishi kutoka Vyama vya Wafanyakazi, Chama cha Waajiri na Serikali
Tatu, kuwa mchakato unaendelea wa kuandaliwa kwa miongozo na kanuni za mafao ambazo lengo lake ni kuboresha maslahi ya wanachama kwa kutambua tofauti za ajira, tofauti za mazingira ya kazi, tofauti za sababu za ukomo wa ajira na umuhimu wa mwanachama kunufaika na michango yake wakati angali katika ajira.
Nne, juu ya uamuzi wa kusitisha maombi mapya ya kujitoa kwa kipindi cha miezi sita kufuatia kuanza kutumika kwa sheria mpaka pale miongozo itakapotolewa na elimu kwa wadau kuandaliwa.
Tano, maoni mahsusi ya kuingizwa kwenye Muswada Binafsi wa Sheria kwa mujibu wa Kanuni ya 81 (1), Taarifa ya Muswada huo kwa mujibu wa Kanuni ya 81 (2), hati ya kuwasilisha muswada kwa dharura na hoja ya kutengua masharti kuhusu muda wa utangazaji wa Miswada ya Sheria kwa mujibu wa Kanuni ya 81 (5) ya Kanuni za Kudumu za Bunge (Toleo la Mwaka 2007).
NAMNA CHANGIA:
Baada ya mada hii “post” angalia chini eneo limeandikwa “comments” bofya hapo na utafunguka ukurasa wa kuandika. Unaweza andika na jina lako, au ukawa huru wa kutoandika jina “anonymous”. Changia sasa!!
Aidha, mwenye nyaraka yoyote anaweza kuituma kupitia jmnyika@parliament.go.tz na nakala kwenye mbungeubungo@yahoo.com; nyaraka hizo kwa ajili ya rejea ni pamoja na Social Security Ammendment Act no.5 ya mwaka 2012, Sheria za Hifadhi ya Jamii zinazohusika, Taarifa na mapendekezo yaliyowasilishwa na kupelekea kufutwa kwa mafao ya kujitoa (withdrawal benefits) na maelezo kuhusu hatua ambayo kifungu husika kiliingizwa na hatimaye kupitishwa na Bunge tarehe 13 Aprili 2012.
Mkutano huu unafanyika kwa kuzingatia haki za Katiba ya Nchi hususani ibara ya 18 juu ya haki ya uhuru wa mawazo na ibara ya 21 juu ya haki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayohusu raia, maisha yake au yanayolihusu taifa.
Pamoja na haki na uhuru huo nawaomba watoa maoni tuheshimu “Kanuni ya Dhahabu” katika mkutano wetu. Mkutano huu umefunguliwa rasmi na tuendelee kutoa maoni na kujadiliana.
Maslahi ya Umma KWANZA.
John Mnyika (Mb)
Bungeni-Dodoma
05/08/2012
0 comments:
Post a Comment