na Hellen Ngoromera
KAMPUNI ya usafiri wa anga ya Precision Air, imetangaza kuongeza safari zake za kila siku kufikia mara tano kwa siku, kuelekea mkoani Arusha, na kuboresha huduma zake za Mwanza, kuanzia Agosti 22 mwaka huu.
Kampuni hiyo imezindua safari mpya kwa ndege ya Boeing 737-300 siku za Jumatano, Ijumaa na Jumapili kwenda Mwanza, ikiwa ni katika kuboresha safari zake na kukidhi mahitaji ya wateja wake.
Akizungumza wakati wa kuzindua safari hizo, Mkurugenzi wa Biashara wa Precision Air, Patrick Ndekana, alisema kuwa kampuni imeshuhudia ukuaji mkubwa kwa kuongezeka kwa njia za safari za nje na ndani ya nchi kwa nusu msimu sasa.
“Tumeongeza safari mpya kwenda Lubumbashi na Lusaka kwa miezi miwili iliyopita na kuongeza kwa kiasi kikubwa ukuaji wa kampuni. Tunajivunia kukua kwa kampuni yetu kwa sasa, tuna njia na vituo 16 hadi sasa na tuna lengo la kuboresha ili kuendelea kuongoza katika huduma za usafiri wa anga nchini,” alisema.
Ndekana alifafanua kuwa Precision Air ndio kampuni pekee inayoongoza kwa huduma za usafirishaji wa anga nchini na kutoa huduma za usafiri katika sehemu mbalimbali za ndani na nje ya nchi.
Alisema kuwa kampuni ilikuwa katika malengo ya kuboresha safari za ndani zaidi, na hivyo imeamua kusitisha huduma za safari kwenda Johannesburg, Afrika Kusini, tangu kuanzishwa kwake kwa takriban mwaka sasa.
“Tumejipanga kuhakikisha tunakidhi mahitaji ya usafi wa anga wa ndani kwanza,” alisema Ndekana.
Pia alibainisha kusitishwa kwa safari za Kigoma na Musoma kutokana na sababu za kiusalama pamoja na kupisha ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kigoma.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment