Home » » STENDI YA MWENGE SASA KUHAMISHIWA MAKUMBUSHO

STENDI YA MWENGE SASA KUHAMISHIWA MAKUMBUSHO


Na Mwandishi wetu
Uongozi  Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam umesema kuwa wakati wowote kuanzia sasa utaihamisha stendi ya mabasi ya Mwenge na na kuipeleka Makumbusho.

Zoezi hilo litakwenda sambamba na kuwaondoa wamachinga wanaoendesha shughuli zao za kibiashara katika maeneo yasiyoruhusiwa kisheria ikiwa ni pamoja na pembezoni mwa barabara na ndani ya vituo vya magari.

Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Mawasiliano wa Manispaa ya Kinondoni, Sebastian Mhowera, wakati akizungumza na NIPASHE.

Mhowera alisema maandalizi ya kuiondoa stendo hiyo yanaendelea na kwamba kinachosubiriwa ni kumalizika kwa zoezi la sensa litakaloanza Agosti 26, mwaka huu.

Aliongeza kuwa matengenezo ya stendi hiyo mpya ya Makumbusho yanaendelea na kwamba hadi sasa yamekamilika kwa asilimia 75 na kuongeza kuwa kilichosababisha matengenezo hayo kuchelewa ni kuwepo kwa mgogoro kati ya manispaa na wafanyabiashara katika eneo hilo ambao kwa sasa umesuluhishwa.

Kwa mujibu wa Mhowera, baada ya kukamilika kwa mabadiliko hayo, hakuna gari litakaloruhusiwa kuingia tena ndani kwenye stendi ya Mwenge na badala yake stendi kubwa kwa magari yote itakuwa ni Makumbusho na Mwenge litakuwa ni  eneo la kushusha na kuondoka.

Alisema zoezi hilo litaambatana na kuwaondoa wafanyabiashara wote waliokuwa wakiendesha shughuli zao kwenye stendi hiyo na nje kando kando ya barabara akisema kuwa kama walivyofanya Ubungo ndivyo itakavyokuwa kwenye eneo hilo.

Pia aliongezakwamba wafanyabiashara wote wa bidhaa za viwandani na mashambani wanapaswa kuendesha shughuli zao kwenye masoko yanayotambuliwa kisheria na kwamba mikopo ipo kwa ajili ya wafanyabiashara watakaokubali kujiorodhesha kuhamia kwenye masoko hayo.

Wakati huo huo, wakazi wote wa jijini Dar es Salaam katika Manispaa ya Kinondoni waishio maeneo ya mabondeni wametakiwa kuondoka mara moja kabla mamlaka haijahukua hatua yoyote ya kubomoa makazi hayo.

Kwa mujibu wa Mhowera, zoezi hilo linahusisha pia wakazi wote ambao nyumba zao zimewekwa alama ya X na kupewa hifadhi eneo la Mabwepande nje kidodo ya Jiji la Dar es Salasaam kutokana na mafuriko yaliyolikumba jiji hilo Disemba mwaka jana na kuyarudia tena makazi hayo ya zamani.

Aliwataka wakazi hao kuondoka kwenye maeneo hayo na kuhamia katika viuwanja walivyopewa Mabwepande.


Chanzo: Nipashe

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa