Mwenyekiti wa Kamati ya haki, Maadili na Madaraka ya Bunge Mhe. Brig. Jen. (Msataafu) Hassan Ngwilizi (Mb) akizungumza na waandishi wa Habari leo katika Ofisi Ndogo za Bunge
wakati akitoa tamko la kamati yake kuhusu shauri la Mhe. Tundu Lissu kuhusiana na uteuzi wa Majaji wa Mahakama
Mwenyekiti wa Kamati ya haki, Maadili na Madaraka ya Bunge Mhe. Brig. Jen. (Msataafu) Hassan Ngwilizi (Mb) akizungumza na waandishi wa Habari leo katika Ofisi Ndogo za Bunge Dar es Salaam wakati akitoa tamko la kamati yake kuhusu shauri la Mhe. Tundu Lissu kuhusiana na uteuzi wa Majaji wa Mahakama. Kulia ni Katibu wa Kamati hiyo Yona Kirumbi
Waandishi wakimsikiliza kwa Makini Mhe. Ngwilizi
Picha na Owen Mwandumbya
*********
JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA
BUNGE LA
TANZANIA
KAMATI
YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE
MAELEZO YA KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE KUHUSU
MWENENDO WA SHAURI LINALOHUSU KAULI YA MHE. TUNDU MUGHWAI LISSU (MB) KUHUSIANA
NA UTEUZI WA MAJAJI WA MAHAKAMA KUU KAMA LILIVYOOMBEWA MWONGOZO WA SPIKA NA
MHE. GOSBERT BEGUMISA BLANDES (MB)
1.0
UTANGULIZI
1.1
Mnamo tarehe 13 Julai, 2012
wakati wa Mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha
2012/2013, Mhe. Gosbert Begumisa Blandes (Mb) aliomba Mwongozo kwa mujibu wa
kanuni ya 68 (7) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2007.
1.2
Katika maelezo yake, Mhe.
Blandes (Mb) alinukuu ukurasa wa 9 aya ya 2 katika Hotuba ya Msemaji wa Kambi
ya Upinzani kwa Wizara ya Katiba na Sheria, Mhe. Tundu Mughwai Lissu (Mb)
unaosomeka kama ifuatavyo, nanukuu:-
“Kwa
mujibu wa taarifa tulizo nazo, sasa watu wanateuliwa kuwa Majaji wa Mahakama
Kuu ambao hawajawahi kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama na - kwa
sababu hiyo – hawajafanyiwa vetting yoyote na mamlaka hiyo ya kikatiba juu ya
uwezo na ujuzi wao na kama ‘wanafaa kwa kila hali kukabidhiwa madaraka ya Jaji
wa Mahakama Kuu.’ Inaelekea watu hao – wengi wao wakiwa wamekaribia muda wao wa
kustaafu kwingineko katika utumishi wa umma – wanapewa ‘zawadi’ ya ujaji ili
kuwawezesha kupata mafao ya Majaji wastaafu ambayo yameboreshwa sana katika
miaka ya karibuni. Matokeo yake ni kuwa na majaji ambao wamechoka na hawawezi
au hawajui namna ya kufanya kazi ya Jaji wa Mahakama Kuu.”
1.3
Mhe. Blandes aliendelea kwa
kusema kuwa anadhani msemaji huyo kwa kutamka maneno hayo, ameingilia mhimili
mwingine wa Mahakama ambao hauna nafasi ya kuja kujitetea ndani ya Bunge.
1.4
Aidha, alisema kuwa maneno hayo
yanalenga moja kwa moja kuwadhalilisha Waheshimiwa Majaji kwamba hawana uwezo,
wamechoka, hawajui wanafanya nini hivyo aliomba mwongozo kujua iwapo hizo ni
taratibu za Bunge kujadili na Mhimili wa Mahakama.
1.5
Kama kawaida ya uendeshaji wa
shughuli za Bunge ulivyo, Mwongozo huo ulipoombwa, ulihitaji kupatiwa majibu
ndani ya Bunge kwa sababu, matamshi ya Mhe. Lissu yalizungumziwa Bungeni, na
pia Mwongozo wa Mhe. Blandes pia uliombwa Bungeni, hivyo majibu kuhusiana na
Mwongozo huo yanapaswa kutolewa Bungeni.
2.0
HATUA
ZILIZOCHUKULIWA NA BUNGE
2.1
Mheshimiwa Naibu Spika, alitoa
maelezo kwa kusema kuwa anatoa nafasi kwa Kambi Rasmi ya Upinzani katika Wizara
hiyo kupeleka addendum kabla ya kikao
cha jioni siku hiyo ili kuweza kurekebisha maneno hayo kwa sababu kama dhamira
ya Kambi hiyo ni kusema maneno hayo, wanawavunjia heshima Waheshimiwa Majaji.
2.2
Katika kikao kilichofuatia
jioni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Jaji Frederick Mwita Werema (Mb)
alisema kuwa alimuomba Msemaji wa Kambi ya Upinzani katika Wizara ya Katiba na
Sheria, Mhe. Tundu Mughwai Lissu (Mb) aondoe maneno yanayozungumziwa katika
hotuba husika kwa sababu taarifa hizo ni kinyume na kanuni ya 64 (1).
2.3
Mwenyekiti wa kikao hicho, Mhe.
Jenista Joakim Mhagama (Mb), alitoa maelezo kuwa, kwa kuwa maelekezo ya Naibu
Spika katika kikao cha asubuhi yalikuwa ni kumtaka Mhe. Tundu Mughwai Lissu (Mb) kuja na addendum ya kuondoa maneno
yanayozungumziwa, anamuomba Mhe. Lissu, kwa heshima na taadhima ya Bunge na kwa
kuheshimu Mhimili wa Mahakama na kuheshimu wadhifa wa Rais katika uteuzi wa
Majaji na kwa kuwatendea haki Majaji, kutoendelea kuvunja kanuni ya 64 (1) (e)
kwa kujadili mwenendo wa Majaji hao ndani ya Bunge kinyume na utaratibu kama
ilivyoelekezwa na kuletwa ombi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
2.4
Hivyo basi, Mwenyekiti alimtaka
Mhe. Lissu (Mb) kuondoa au kutoondoa maneno yanayozungumziwa ili aweze kutoa
mwongozo.
2.5
Mhe. Tundu Mughwai Lissu (Mb)
alitoa maelezo yake kwa kusema kwamba, kwanza anashangazwa na utaratibu
unaotumika katika kulishughulikia suala hilo kwa kuwa haupo kwenye Kanuni.
2.6
Lakini pili, alisema kuwa kama
alichokisema hakikuwa cha kweli, kanuni ya 63 inayozungumzia kutosema uongo
Bungeni inatoa utaratibu wa kuzingatiwa kitu ambacho pia hakikufanyika.
Akaongeza kwa kusema kuwa, kwa kuwa
Kanuni hazikufuatwa, walioomba mwongozo hawakufuata Kanuni na Kiti
hakikifuata Kanuni kwa kumuambia afute kitu bila kutoa maelezo yanayotakiwa kwa
mujibu wa Kanuni, hivyo basi yeye hatashiriki kwenye kukanyaga Kanuni na kwenye
hilo asingekuwa tayari.
2.7
Kufuatia maneno hayo, Mwenyekiti
alitoa mwongozo wake kwa kuiagiza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge
ili ipitie mwenendo wa shughuli yote ya siku hiyo katika suala hilo kama
inavyoonekena katika Hansard na
kulishauri Bunge zima kwa ujumla wake hatma ya kufanya katika jambo hilo.
3.0
HATUA
ZILIZOCHUKULIWA NA KAMATI
3.1
Baada ya suala hili kuwasilishwa
na Ofisi ya Spika mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Kamati
imefanya yafuatayo:-
·
Kupitia na kuchambua Taarifa
Rasmi za Bunge (Hansard) ya tarehe 13 Julai, 2012 kwa madhumuni ya kuchambua
suala husika kama linavyojitokeza katika mwenendo wa majadiliano ndani ya Bunge;
·
Kuhoji mashahidi mbali mbali kwa
madhumuni ya kufikia maamuzi.
3.2
Pamoja na hatua ambazo Kamati
imezichukua, shauri hili bado linafanyiwa uchambuzi na uchunguzi zaidi ili
Spika ashauriwe hatua za kuchukua.
4.0
MASUALA
YALIYOJITOKEZA HIVI KARIBUNI
4.1
Katika siku za karibuni,
tumeshuhudia malumbano makali ambayo yamekuwa yakijitokeza magazetini na pia
baadhi ya taarifa zimekuwa zikirejea kinachosemekena kutokea ndani ya Kamati.
4.2
Baadhi ya vyombo vya habari
vilianza kwa kuripoti masuala ambayo yanajadiliwa mbele ya Kamati kitu ambacho
ni kosa kubwa kwa mujibu wa kifungu cha 31 (1) (f) cha Sheria Haki, Kinga na
Madaraka ya Bunge, Sura ya 296. Aidha, wengine wamekuwa wakichapisha masuala
hayo kana kwamba wamepewa taarifa hizo na mashahidi waliofika mbele ya Kamati.
4.3
Kamati imechukua hatua kadhaa kwa
baadhi ya Wahariri wa vyombo ambavyo vimekuwa vikiandika habari hizi kinyume na
Sheria. Zoezi hili bado linaendelea.
5.0
MSIMAMO
WA KAMATI
5.1
Ibara ya 100 ya katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, inasema kuwa kutakuwa na Uhuru wa mawazo, majadiliano
na utaratibu Katika Bunge na uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo
chochote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, au katika mahakama au mahali
penginepo nje ya Bunge.
5.2
Uhuru wa utaratibu unaohifadhiwa
na ibara hiyo ya Katiba umelipa Bunge mamlaka ya kujiwekea utaratibu wa kushughulikia
masuala yake katika Kanuni za Kudumu za Bunge zilizotungwa chini ya Ibara ya 89
(1) ya Katiba.
5.3
Nyongeza ya Saba, Fasili ya 3 ya
Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2007 imeweka utaratibu wa Majukumu ya
Kamati yatakayofanywa kwa faragha. Majukumu yatakayofanywa kwa faragha kwa
mujibu wa kifungu hicho, ni mambo yote ambayo yakitolewa kwa Waandishi wa
Habari kabla ya wakati wake yanaweza kuathiri maamuzi ya Kamati na pia
kusababisha ukiukwaji wa Kanuni za Bunge.
5.4
Mojawapo ya masuala ambayo
yanatafsiriwa na kifungu hicho kuwa ni ya faragha ni kazi zote zinazopelekwa
kwake na Mheshimiwa Spika ili baadaye apelekewe taarifa za mapendekezo ya hatua
za kuchukuliwa na Bunge au kuyatolea maamuzi kwa mujibu wa fasili ya 3 (1) (a).
5.5
Aidha, kwa mujibu wa fasili ya
3(2) ya Nyongeza ya Saba, Kamati ya haki, maadili na Madaraka ya Bunge imetajwa
wazi kuwa ni Kamati itakayofanya kazi zake kwa faragha.
5.6
Hivyo basi, kwa madhumuni ya kuendeleza
utaratibu wa mgawanyo wa madaraka ambapo mihimili mitatu ya dola inatakiwa mara
zote kuheshimiana na kutoingiliana katika utendaji kazi wake, hasa pale ambapo
suala linalokuwa linashughulikiwa na mhimili mmojawapo kusubiri uamuzi (subjudice rule) Kamati inapendekeza
yafuatayo:-
·
Kwa kuwa suala hili liko mbele
ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ambayo inaendelea na uchunguzi;
·
Haitarajawi kwa taasisi
nyingine, nje ya Bunge kulizungumzia suala hili kwa kuwa linajadiliwa na Kamati
ya Bunge;
·
Hivyo basi, Kamati inashauri
Watendaji wa Serikali, Watendaji wa Mahakama na taasisi nyingine zote, kuacha
kuzungumzia suala la Uteuzi wa Majaji kama ambavyo limewasilishwa Bungeni;
·
Kamati inavishauri Vyombo vya
Habari kuacha kuzungumzia suala hili mpaka pale ambapo uamuzi wa Kamati
utakapotolewa Bungeni;
·
Hata hivyo, Kamati inazishauri
taasisi zote ambazo zinadhani zina maoni yoyote kuhusiana na suala hili,
ziwasilishe maoni hayo kwa maandishi kwa Ofisi ya Katibu wa Bunge ili yafanyiwe
kazi na Kamati.
6.0
HITIMISHO
6.1
Kamati imeamua kutoa tamko hili
kwa madhumuni ya kuhakikisha kuwa uvunjifu wa kanuni na taratibu tulizojiwekea
kwa mujiu wa Katiba na Sheria nyingine za nchi kutoendelea kuvunjwa.
6.2
Kamati inaelewa unyeti wa suala
hili kwa pande zote ambazo zinahusika na inapenda kuwahakikishia umma wa
Watanzania kuwa ushauri wa Kamati kwa Bunge utazingatia ukweli, uwazi na
uwajibikaji bila kupendelea au kuonea mtu yeyote.
6.3
Hivyo basi, Kamati inaomba watu
wote tunyamaze tuliache Bunge kama chombo kikuu cha uwakilishi lifanye kazi
yake kwa uhuru.
Baada ya
kusema hayo, nawashukuru kwa kunisikiliza.
Brig. Jen. (Mstaafu) Hassan Athuman Ngwilizi (Mb)
MWENYEKITI
Kamati
ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge
20 Septemba, 2012
0 comments:
Post a Comment