Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » John Mnyika:Taarifa kwa Umma:Madini, Mafuta na Gesi

John Mnyika:Taarifa kwa Umma:Madini, Mafuta na Gesi


 Mbunge wa jimbo la Ubungo-Chadema, John Mnyika
--
Spika wa Bunge Anna Makinda ndani ya wiki moja atumie madaraka
na mamlaka yake kutangaza kwa umma kamati nyingine ya kudumu ya Bunge
itayoshughulikia masuala ya gesi asili kabla na wakati wa mkutano wa tisa wa
Bunge uliopangwa kuanza tarehe 30 Oktoba 2012 kufuatia hali tete na tata kuhusu
sekta ndogo ya gesi asilia nchini na kwa kuzingatia umuhimu na unyeti wa sekta
hiyo katika uchumi wa nchi na maisha ya wananchi.


Pamoja  na mambo mengine
aelekeze kamati hiyo kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Maazimio ya
Bunge ya mwaka 2011 kuhusu Sekta Ndogo ya Gesi Asili ikiwemo juu ya hatua
iliyofikiwa katika kushughulikia tuhuma za ufisadi, madai ya mapunjo ya fedha
za mauzo ya Gesi asili na hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya sera, mpango
mkakati na sheria ya gesi asili.

Hatua
hii ni muhimu kufuatia ukimya wa Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter
Muhongo kuhusu kauli yangu ya tarehe 4 Oktoba 2012 ya kutaka Taarifa ya
ufafanuzi kuhusu utafutaji wa mafuta na gesi asili nchini iliyotolewa na Wizara
ya Nishati na Madini tarehe 21 Septemba 2012 ifutwe kwa kuwa italinda ufisadi
na kukwaza utetezi wa rasilimali za taifa.

Taarifa
hiyo ya Wizara ya Nishati na Madini ilieleza kuwa maandalizi ya sera ya gesi
asili yapo katika hatua za mwisho wakati ambapo kamati mbalimbali za kudumu za
Bunge hazijahusishwa katika mchakato huo muhimu pamoja na kuwa mamlaka ya
kutunga sera kwa mfumo wetu wa sasa ni ya Baraza la Mawaziri hata hivyo kwa
unyeti na upekee wake sera ya gesi Spika wa Bunge anapaswa kuwezesha Kamati za
Kudumu za Bunge zihusishwe ili pawepo mashauriano na maridhiano kwa mapana na
marefu.

Taarifa
hiyo ya Wizara ya Nishati na Madini ilieleza kuwa mikataba 26 ya TPDC ni sehemu
ya nyaraka muhimu za kuboresha utayarishaji wa sera ya gesi asili, hata hivyo
mikataba hiyo imeendelea kuwa siri hivyo Spika aingilie kati kuziwezesha Kamati
za Kudumu za Bunge kuisimamia serikali
kurekebisha mikataba ya sasa na kuboresha mikataba ijayo kwa Serikali
kutekeleza mwito wangu wa toka mwaka 2011 wa kutaka mikataba hiyo iwasilishwe
bungeni na iwekwe wazi kwa umma.

Izingatiwe  kwamba katika
Mkutano wa Nane wa Bunge Spika alitangaza kuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Nishati na Madini imevunjwa na kwamba majukumu yaliyokuwa yakishughulikiwa na
kamati hiyo yatashughulikiwa na kamati nyingine kwa mujibu wa madaraka na
mamlaka ya Spika.

Irejewe kwamba kwa mujibu wa Kanuni ya 116 na Kanuni ya 114
fasili ya 14 Spika ana mamlaka na madaraka ya kukabidhi mambo mengine
yashughulikiwe na Kamati ya Kudumu ya Bunge nyingine kama  atakayoelekeza.

Ikumbukwe
kuwa Julai 2011 na Julai 2012 kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na
Madini na kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani nilieleza namna nchi yetu
ilivyojaliwa utajiri wa gesi asilia katikati ya lindi la umasikini wa wananchi
na kwamba taifa letu lina fursa ya kuwa nchi kiongozi katika gesi Afrika na
kushindana kimataifa ikiwa tutaweka mstari wa mbele upeo, umakini na uadilifu
katika sekta ya nishati kuepusha laana ya rasilimali.

Hata
hivyo, mapitio ya utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2011/2012 yanaonyesha bado
serikali haichukui hatua thabiti kushughulikia ufisadi na udhaifu wa kiuongozi
katika sekta ndogo ya gesi asili  hivyo
hatua za haraka zisipochukuliwa katika mwaka wa fedha 2012/2013 na
kuendelea  rasilimali  inaweza kuwa chanzo cha migogoro na
kuhatarisha pia usalama wa nchi.

Kwa
niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani nilieleza bungeni tarehe 15 Julai 2011 kuhusu
tuhuma za ufisadi na ukiukwaji wa mikataba katika sekta ndogo ya gesi inaoihusu
pia Kampuni ya Pan African Energy Tanzania (PAT) na kutaka kuundwa kwa kamati
teule ya bunge kuchunguza suala hilo.

Badala
yake Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini uliunda kamati ndogo ya
iliyofanya uchunguzi uchunguzi wa masuala husika na taarifa kuwasilishwa
bungeni mwaka 2011 ; hata hivyo mpaka sasa maamizio ya bunge kufuatia taarifa
hiyo hayajatekelezwa kwa ukamilifu.

Tarehe
27 Julai 2012 kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani niliitaka Serikali kueleza
ni kwanini mpaka sasa kiasi cha dola milioni 20.1 zilizopunjwa kifisadi
hazijareshwa na kuitaka serikali iache kutumia kisingizio cha kuundwa kwa Timu
ya Majadiliano (GNT) kuchelewesha utekelezaji wa maazimio, suala ambalo Wizara
ya Nishati na Madini itapaswa kueleza hatua iliyofikiwa iwapo Spika atazingatia
mwito huu na kuchukua hatua za haraka.

Ifahamike
pia kwamba mwaka 2011 kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
niliitaka  serikali ambazo kuweka wazi
bungeni na kwa umma mikataba ya madini, mafuta na gesi asili katika nchini  ili kuongeza tija na uwajibikaji.

Aidha
nilitoa mwito mwito kwa wananchi na wabunge kuongoza marekebisho ya kikatiba na
kisheria ili kuweka vifungu vya kulazimisha uwazi katika mikataba katika hizo
muhimu kwa uchumi na usalama wa nchi.

Uwazi
katika mikataba utadhibiti pia mianya ya ufisadi miongoni mwa baadhi ya
watendaji wa serikali kwa kuwa mikataba hiyo itajadiliwa na umma na hivyo
kupunguza uwezekano wa viongozi kutanguliza maslahi binafsi na kuwa na mikataba
bora ya baadaye yenye kuzingatia maslahi ya umma.

Usiri
katika mikataba ni tatizo kwa sababu masharti kama ya kushughulikia madhara ya
kimazingira na kuchangia katika huduma za jamii pamoja na kulipa kodi
zinazokusudiwa yanaweza yasitekelezwe kwa ukamilifu kama hayatafahamika kwa
wabunge na umma. Aidha, ipo mikataba yenye vifungu ambavyo vinakinzana na
sheria nyingine ama vinalinda kupindukia makampuni dhidi ya sheria nyingine za
nchi zinazotungwa masuala ambayo yanaingilia mamlaka ya bunge ya kutunga sheria
na kuisimamia serikali.

Sheria
mpya ya madini Tanzania ya mwaka 2010 ina kifungu kinachotaka uwazi hata hivyo
kimejikita katika uwazi wa rekodi na ripoti hakijaweka bayana mfumo wa uwazi
katika mikataba ya  madini,  sheria ya mafuta nayo haina kifungu cha uwazi
katika mikataba na sheria ya gesi haipo kabisa; hali ambayo inahitaji
kurekebishwa.

Pamoja
na mapato uwazi katika mikataba utachangia katika kupata tija ya ziada katika
uchimbaji kwa kulinda maslahi ya wafanyakazi na kuweka mfumo mzuri zaidi wa
makampuni kununua bidhaa za ndani kwa majibu wa vifungu vya mikataba hali ambacho
itawezesha rasilimali kunufaisha wananchi wengi zaidi.

Uwazi
katika mikataba utawezesha wabunge na wadau wengine kusimamia ipasavyo taasisi
za kiserikali kuhusu mifumo ya kifedha na kibenki ambayo itaongeza mchango wa
sekta za nishati na  madini katika
kuimarisha uchumi kwa kudhibiti mfumuko wa bei na kuporomoka kwa sarafu wakati
huu ambapo thamani ya mauzo imeongezeka duniani lakini mzunguko umejitika
katika masoko na mabenki ya nje. Kwa ujumla, uwazi katika mikataba utapanua pia
uwajibikaji wa kuongeza umiliki wa nchi na wananchi wa michakato ya utafutaji
na uchimbaji wa mafuta na gesi asili.

Pamoja
na kuwa ibara ya nne ya katiba inasema kwamba rasilimali na mali asili zote
ziko chini ya usimamizi wa serikali; na ibara ya 63 inaeleza kwamba bunge ndicho
chombo kikuu cha kuisimamia serikali kwa kutunga sheria na kupitisha mipango,
katiba haijalazimisha mikataba ya madini, mafuta na gesi kuridhiwa na bunge
hivyo katika kipindi cha sasa mikataba hiyo iwasilishwe kwa rejea na mapitio.

Katika
muktadha huo, tarehe 4 Oktoba 2012 nilimtaka Waziri wa Nishati na Madini Prof.
Sospeter Muhongo afute taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo kuwa
lengo la agizo lake la kupitiwa kwa mikataba yote 26 ya utafutaji mafuta na
gesi asili ni “kuhakikisha kwamba endapo kuna mapungufu katika mikataba hiyo,
mapungufu hayo yasijirudie tena katika mikataba mipya ya baadaye” kwa kuwa
ikiachwa ilivyo italinda ufisadi na kukwaza utetezi wa rasilimali za taifa.

Nilieleza
kwamba ufafanuzi uliotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini
unatoa mwanya kwa mikataba mibovu kulindwa wakati ambapo kuna madai tuliyotoa
toka mwaka 2011 kwamba baadhi ya mikataba hiyo imeingiwa kifisadi na mwaka huu
wa 2012 zimeibuka tuhuma za vigogo wa serikali kuingiziwa fedha kifisadi katika
akaunti zao za nchini Uswisi na makampuni ya nje ya utafutaji mafuta na gesi
asili.

Aidha,
pamoja Serikali kuwasilisha bungeni mikataba inapaswa pia kuwasilisha mipango
kabambe (master plan) ya mafuta na gesi asili yenye kuzingatia mabadiliko ya
kisera na kimfumo yenye kuwezesha nchi na wananchi kunufaika na rasilimali
husika.

Kauli
hii nimeitoa leo tarehe 14 Oktoba 2012 ikiwa ni Siku ya Kumbukumbu ya Hayati
Julius Nyerere ambaye alipinga ufisadi na kutaka rasilimali za nchi zitumike
kwa manufaa ya maisha ya wananchi:

John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa