na Abdallah Khamis
LICHA
ya aliyekuwa mwenyekiti wa UWT wilaya ya Kinondoni, Agnes Luvanda (Mama
Makete), kujisalimisha Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni jana, hakuweza
kuhojiwa kutokana na kupoteza fahamu ghafla mara baada ya kuelezwa sababu za
kutafutwa kwake.
Habari
kutoka chanzo cha ndani ya jeshi hilo, zilieleza kuwa baada ya Mama Makete
kufika katika kituo cha polisi, Osterbay, alikutana na Kamanda wa Polisi wa
mkoa huo, Charles Kenyela, na kuelezwa sababu za kutafutwa kwake.
Taarifa
zinaeleza kuwa baada ya kufahamishwa madhumuni ya kutafutwa, mama huyo alisema
kuwa hawezi kuongea akiwa peke yake mpaka atakapokuwa na wakili wake hali
iliyomfanya Kamanda Kenyela kumpa fursa ya kumsubiri wakili wake.
Hata
hivyo chanzo chetu kilieleza kuwa akiwa katika chumba cha kusubiria, hali yake
ilianza kubadilika ghafla na kisha kupoteza fahamu jambo lililowafanya askari
pamoja na ndugu zake wa karibu kumuwahisha katika Hospitali ya Masama iliyoko
Mbezi Beach kwa matibabu.
Tanzania
Daima iliwasiliana na Kamanda Kenyela kupata usahihi wa taarifa hizo ambapo
alikiri akisema, “Unayonieleza ni kweli; huyu mama tulipomweleza sababu za
kumtafuta aliomba awasiliane na wakili wake lakini baada ya muda tukaona
anaishiwa nguvu na kisha kupoteza fahamu, hivyo tukamuwahisha hospitali,”
alisema.
Kenyela
alisema watamsubiri mama huyo awe katika hali nzuri ya kiafya ili wafanye
mahojiano naye juu ya tuhuma zinazomkabili ambapo inadaiwa kuwa ameonekana
katika picha za video akiwahimiza vijana kufanya vurugu na kisha wakavamie
kituo cha polisi, Wazo Hill.
Hivi
karibuni jeshi hilo, mkoa wa Kinondoni, lilitangaza kumsaka mama huyo baada ya
kupatikana kwa picha za video zinazomuonyesha mtu anayedhaniwa kuwa yeye
akiwahimiza vijana kuua hata mtu mmoja katika vurugu zilizotokea mwaka mmoja uliopita
katika mtaa wa Mivumoni, kata ya Wazo Hill, na kusababisha vifo vya watu
wawili.
Katika
mfululizo wa picha hizo za video anaonekana mtu aliyevaa gauni la mawingu
akisikika kuwahimiza vijana kuua na kisha kwenda kuvamia kituo cha polisi.
Baada
ya muda wanaonekana vijana wakilishambulia gari kwa mawe na kisha wakamwendea
mtu mmoja na kuanza kumshambulia kwa mapanga, rungu na shoka sehemu mbalimbali
za mwili wake.
Mbali
na matukio hayo yanayodaiwa kusababisha vifo vya watu wawili na majeruhi saba
pia wanaonekana vijana wakiwa wamesogelea kituo cha Wazo hali inayowafanya
polisi wa kituo hicho kuweka zuio kwa kutumia alama za kipolisi.
Na
baada ya muda picha zinamuonyesha kwa ufasaha Anna Luvanda (mama Makete)
akiongea kuelezea namna watu aliowaita wabomoaji wa maeneo yao walivyowafikia
na wao kutoa taarifa kituo cha polisi bila kupata msaada wowote.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment