Home » » Tume ya Kikristo ya Huduma za jamii (CSSC)yakabidhi jengo la huduma kwa wagonjwa wa nje (OPD) katika hospitali ya Cardinal Rugambwa.

Tume ya Kikristo ya Huduma za jamii (CSSC)yakabidhi jengo la huduma kwa wagonjwa wa nje (OPD) katika hospitali ya Cardinal Rugambwa.




Kaimu Mganga Mkuu wa
Serikali, Dk. Donan Mmbando na Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani
(KfW), Bw. Klaus Brendes wakipewa maelezo na Meneja wa Mradi Bi. Grace
Mwang'onda jinsi watakavyokata utepe kuzindua Jengo la huduma kwa wagonjwa wa
nje (OPD) katika hospitali ya Cardinal Rugambwa.
Mkurugenzi wa Benki ya
Maendeleo ya Ujerumani (KfW) Bw. Klaus Brendes akifungua Kitambaa kuashiria
ufunguzi wa jengo hilo la huduma kwa wagonjwa wa ndani (OPD) katika hospitali
ya Cardinal Rugambwa
Mkurugenzi
Mtendaji wa Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC), Bw. Peter Maduki
akisoma ripoti fupi ya mradi kwa mgeni rasmi Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Dk. Donan
Mmbando ambaye alimwakilisha waziri wa afya na ustawi wa jamii Dk. Hussein
Mwinyi
Meneja
wa Mradi Bi. Grace Mwang’onda akiongea na waandishi wa habari mara baada
ya uzinduzi huo.Kwa picha na habari zaidi www.afyamtandaonetwork.ning.com,
www.cssc.or.tz 
---
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema
itaendelea kuboresha zaidi ushirikiano na sekta binafsi yakiwemo mashirika
ya dini, kwa kuboresha zaidi mazingira yatakayowezesha sekta binafsi
kushiriki kikamilifu katika utoaji wa Huduma za afya.

Hayo yamesemwa na Waziri wa afya na ustawi wa jamii
Dk. Hussen Mwinyi katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Kaimu Mganga
Mkuu wa Serikali Dk. Donan Mmbando wakati wa ufunguzi wa jengo jipya
linalohudumia wagonjwa wa nje (OPD) liliojengwa kwa ufadhili wa Serikali
ya Ujerumani kupitia Benki ya maendeleo ya Ujerumani iitwayo KfW na
kusimamiwa na Tume ya Kikristo ya Huduma za jamii (CSSC) kwa lengo la
kuboresha Huduma ya afya na elimu nchini.

Dk. Mwinyi amesema uboreshaji wa mazingira ambao
serikali inatekeleza ni pamoja na kutoa ruzuku kadiri hali ya fedha
inavyoruhusu, kushirikisha sekta binafsi katika kupanga, kutekeleza
na kutathimini utoaji wa Huduma za afya nchini.

Aidha Dk. Mwinyi amebainisha kuwa kwa sasa serikali
inatumia hospitali Teule za wilaya zinazomilikiwa na Kanisa 39 na hospitali
mbili kama hospitali za rufaa za Kanda. Dk. Mwinyi amefafanua kuwa hivi
karibuni Serikali imezipandisha hadhi hospitali 10 za mashirika ya dini
na kuzifanya hospitali za rufaa ngazi ya mkoa.
Akiwasilisha ripoti fupi ya ujenzi wa jengo hilo,
Mkurugenzi Mtendaji wa CSSC, Bw. Peter Maduki amesema kuwa ujenzi wa
jengo hilo katika hospitali ya Cardinal Rugambwa ulianza rasmi mwaka
2008, chini ya usimamizi wa CSSC na mshauri msanifu wa ujenzi kutoka
Kampuni ya Landplan Icon Architects wa Dar es salam na Mkandarasi M/S
Build All Contractors.

Bw. Maduki amefafanua kuwa kazi ya kukamilisha ujenzi
huo imegharimu kiasi cha shilingi za Kitanzania milioni 900 na fedha
hizo zote zimetolewa na serikali ya Ujerumani.

Akielezea jengo hilo la kisasa, Bw. Maduki amesema
kuwa lina vyumba vya matibabu kulingana na mwongozo wa wizara ya Afya,
vyumba hivyo ni kwa ajili ya Huduma za maabara, upasuaji mdogo, dawa,
sindano, ushauri, mikutano uchunguzi (scanning) na mapumziko Aidha vyumba
vingine ni kwa ajili ya mazoezi ya viungo, ofisi na sehemu kubwa kwa
ajili ya kusubiria.

Naye Mkurugenzi wa Benki ya maendeleo ya Ujerumani
KfW, Bw. Klaus Brendes akizungumza katika ufunguzi huo kwa niaba ya
balozi wa Ujerumani nchini, amesema serikali ya Ujerumani inafadhili
miradi mingi ya maendeleo Tanzania kama vile; maji, afya, elimu nk.
inafarijika kuona miradi hii inafanikiwa vizuri ukiwemo mradi huo wa
ujenzi wa jengo hilo la hospitali ya Cardinal Rugambwa, na kuahidi kuendelea
kusaidia, miradi mingine ya maendeleo.

Akitoa neno la shukrani Askofu msaidizi wa Jimbo
Katoliki la Dar es salaam ambao ndiyo wamiliki wa hospitali hiyo, Mhashamu
Eusebius Nzingilwa amewashukuru wafadhili, serikali na CSSC kwa jitahada
kubwa walizoonyesha katika ujenzi huo. 

“Tunashukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano
na msaada mkubwa wanatoa katika kuboresha huduma za afya nchini pia
wafadhili kwa msaada wao wa kifedha pamoja na CSSC kwa utendaji wenu
wa kazi katika kusimamia ujenzi huo” amesema Askofu Nzigilwa.

Askofu Nzigilwa amebainisha kuwa Huduma za afya ambazo
zinatolewa na Makanisa ni kwa ajili ya watu wote bila bila kubagua dini
ya mtu yeyote yule, hivyo amewataka watumishi wa hospitali ya Cardinal
Rugambwa kuendelea kutoa Huduma bora yenye kujaa tunu ya upendo kwa
wagonjwa.

Hospitali ya Cardinal Rugambwa inamilikiwa na Kanisa
Katoliki Jimbo la Dar es Salaam, ilianza kama zahanati na baadaye kupandishwa
na hadhi na kuwa hospitali mwaka 2005. Inahudumia watu kutoka manispaa
ya Ilala na  maeneo mbalimbali kama vile Kisarawe, Mkuranga pia
na watu wengine kutoka maeneo ya Unguja na Pemba. 

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa