Na Masau Bwire
KATIKA hali isiyo ya kawaida, wanafunzi wa Shule ya Sekondari Makumbusho,
iliyopo Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam, jana walimshambulia na kumjeruhi
vibaya mwalimu wao aliyefahamika kwa jina moja la Bw. Epimack, ambaye aliumia
usoni.
Tukio hilo limetokea jana saa tano asubuhi baada ya Bw. Epimack kwenda kuamulia
ugomvi wa mwanafunzi wa kike na kiume ambao wanasoma kidato cha nne shuleni
hapo.
Inadaiwa wanafunzi hao walikuwa wakipigana darasani kutokana na wivu wa
kimapenzi baada ya mwanafunzi wa kike kutangaza kumkataa aliyekuwa mpenzi wake.
Hali hiyo ilimkasirisha mwanafunzi aliyeachwa ambaye aliamua kumshambulia
aliyekuwa mpenzi wake (mwanafunzi wa kike), kwa mateke na ngumi katika sehemu
mbalimbali za mwili.
Mbali ya kipigo hicho, mwanafunzi aliyeachwa aliahidi kuendeleza dozi ya
kichapo popote watakapokutana hadi atakapoamua kurudisha uhusiano wao wa
kimapenzi.
Baada ya Bw. Epimack kufika darasani na kuamlia ugomvi huo, alijikuta ananunua
kesi kutokana na baadhi ya wanafunzi kuamua kumvamia na kuanza kumshambulia kwa
kumpiga ngumi za uso.
Bw. Epimack aliokolewa na walimu wenzake wakati tayari uso wake ukiwa umeumuka
vibaya kwa kipigo.
Baada ya walimu hao kumuokoa mwenzao, mwanafunzi ambaye alianzisha ugomvi huo
alikamatwa na kufungiwa ofisini lakini alianzisha vurugu nyingine hivyo walimu
shuleni hapo waliamua kupiga simu polisi ili kuomba msaada.
Polisi walipofika shuleni hapo, walimchukua mwanafunzi huyo na wenzake
waliobainika kuhusika kumpiga Bw. Epimack.
Jambo la kushangaza, baada ya wanafunzi hao kuingizwa kwenye gari la polisi,
wanafunzi wote wa kidato cha nne walilizingira gari hilo na kulizuia lisiondoke
na wenzao huku wakirusha mawe.
Kutokana na hali hiyo, polisi walilazimika kufyatua mabomu ya machozi hewani
ili kuwatawanya wanafunzi hao lakini vurugu hizo zilizidi kuongezeka hivyo walilazimika
kuongezwa polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), ambao walifanikiwa
kuzituliza.
Ofisa mmoja wa Jeshi la Polisi ambaye jina lake halikufahamika mara moja,
aliwakusanya wanafunzi hao na kuwaambia wenzao waliokuwa wakishikiliwa na
polisi hawataondoka nao.
Aliwataka wanafunzi waliokamatwa warudi shuleni hapo leo kwa Mkuu wa shule
wakiwa na wazazi wao na baada ya polisi hao kuondoka, aliingia Ofisa Elimu wa
Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam, ambaye alijitambulisha kwa jina moja la
Sanga.
Baada ya ofisa huyo kufanya mazungumzo na Mkuu wa shule hiyo, aliwakusanya
wanafunzi wote na kutoa tamko ambalo liliwakera baadhi ya walimu wa shule hiyo.
“Natoa tamko kwamba, wanafunzi wote wa Sekondari ya Makumbusho, waliosajiliwa
kufanya mtihani mwaka huu, Jumatatu wataingia darasani na kufanya mtihani bila
masharti yoyote na hakuna mzazi atakayeitwa,” alisema ofisa huyo.
Baadhi ya walimu shuleni hapo waliifananisha kauli ya ofisa huyo na methali
isemayo “mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu” wakimaanisha kama wanafunzi
hao wangekuwa wamempiga yeye, asingethubutu kusema maneno hayo.
Walimu hao walidai shule hiyo imeharibika kutokana na kiongozi mmoja shuleni
hapo (jina tunalo), kushindwa kuiongoza na kuomba viongozi wa ngazi za juu
kumhamisha ili apatikane mwingine atakayerejesha nidhamu ya wanafunzi.
“Wanafunzi wanavuta bangi hadharani, wanacheza kamali hadi darasani, masuala ya
mapenzi kati yao ni ya wazi kabisa lakini kiongozi huyu akipelekewa mwanafunzi
mwenye matatizo ya
utovu wa nidhamu hachukui hatua yoyote zaidi ya kusema tusiwaonee watoto wa
watu,” walisema.
Chanzo: Majira
0 comments:
Post a Comment