Na Mwandishi Wetu
WAKALA wa Vipimo nchini (WMA), amewapa
changamoto wazalishaji wa asali kufungasha kwa kutumia njia za kisasa na
kutambulisha bidhaa zao ili ziweze kukubalika katika masoko ya kimataifa.
Ushauri huo ulitolewa jana na Mkuu wa Kitengo cha Mipango wa WMA, Moses Ntungi,
wakati akiwaelezea wananchi waliotembelea Banda la WMA kwenye maonyesho ya Wiki
ya Asali yanayofanyika kitaifa katika Viwanja vya Maonyesho vya JK Nyerere,
Barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam.
Alisema kwamba, wafanyabiashara wa asali na bidhaa mbalimbali hapa nchini
wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kutokujua kufungasha bidhaa zao kwa njia za
kisasa na namna ya kutambulisha bidhaa zao kwa kwa walaji hali ambayo inaweza
kusababisha bidhaa zao kukosa soko kwenye nchi zilizoendelea licha ya bidhaa
zao kuwa bora.
Alisema kwamba, WMA imekuwa ikiwapa mafunzo wajasiriamali mbalimbali kuhusu
namna bora ya kutambulisha bidhaa zao zilizofungwa kama kuandika utambulisho wa
bidhaa, jina la kampuni au mzalishaji au mfungashaji, eneo zinakopatikana
biashara hizo, uzito au ujazo halisi wa bidhaa husika na kipimo husika ikiwamo
gramu au kilogramu.
Alisema kwamba, mzalishaji au mfungashaji anatakiwa kuandika tarehe ya
kutengenezwa na muda wa kwisha kwa matumizi ya bidhaa husika.
‘Vile vile wakati wa kuandika maelezo ya kutambulisha bidhaa husika, mzalishaji
au mfungashaji anatakiwa kutumia lugha angalau moja inayotambulika nchini
mahali bidhaa zinakopelekwa, maelezo yawe wazi, rahisi kusomeka na rahisi
kuonekana na mteja,” alisema.
Ntungi alisema mzalishaji anapofungasha bidhaa yake anapaswa kupima bidhaa yake
kwa kutumia mizani inayofaa kupimia bidhaa husika na kisha kuandika kipimo
sahihi alichotumia wakati anafungasha bidhaa hiyo.
“Kama ametumia gramu kipimo cha uzito aandike gramu, kama ametumia kipimo cha
ujazo, lita, basi aandike kipimo hicho. Katika pitapita yetu kwenye mabanda ya
wajasiriamali hawa wa asali, tumekuta wengine wameandika labda 500 tu na kuacha
hivyo hivyo, sasa hapo mnununuzi hawezi kujua umetumia kipimo gani, cha uzito
au ujazo.
“Vile vile, baadhi ya wajasiriamali hawa utakuta wametambulisha bidhaa zao kwa
lugha ya kigeni, kama vile Kiingereza bila kuweka neno la Kiswahili hata moja,
wakati lengo lao ni kuuza bidhaa hiyo hapa hapa nchini.
“Hivyo basi, ni vema wanapofungasha bidhaa zao, waandike lugha ambayo kule
anakopeleka bidhaa itaeleweka na kama anauza hapa Tanzania akiandika Kiingereza
basi aandike na Kiswahili ili watu wengi hapa nchini waweze kuelewa vyema
maelezo ya bidhaa hiyo,” alisema.
Alisema WMA inawashauri wafanyabiashara watumie mizani inayofaa wakati wa
ufungashaji na kwamba mfungashaji anapaswa kupima kifungashio kabla ya
kufungasha bidhaa na kisha kupima kifungashio kikiwa na bidhaa tayari ili
kupata uzito au ujazo halisi wa bidhaa iliyofungashwa.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment