Home » » Jaji Mwesiumo asema Bunge limepoteza hadhi..!

Jaji Mwesiumo asema Bunge limepoteza hadhi..!


 Mbunge wa zamani wa Kilombero, Jaji mstaafu Edward Mwesiumo, amesema Bunge la sasa limepoteza hadhi na mvuto wake kutokana na vitendo vya baadhi ya wabunge wanaolitumia kujitafutia umaarufu badala ya kulitumia kutatua matatizo ya wananchi.

Aidha, alisema lazima wabunge watambue kuwa uhuru na demokrasia iliyopo nchini haiwapi kibali cha kutoleana lugha za kejeli na kudhalilishana wenyewe kwa wenyewe bungeni kwani kufanya hivyo ni kujivunjia heshima mbele ya wananchi.

Akizungumza katika mahojiano maalum yaliyofanyika jana kwenye ofisi za gazeti hili, Mikocheni jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, Jaji Mwesiumo alisema kauli na vituko vinavyofanywa na baadhi ya wabunge bungeni  inalipunguzia mvuto na heshima chombo hicho.

Jaji Mwesiumo ambaye pia aliwahi kuwa naibu waziri wa mambo ya ndani ya nchi, alisema kwa mtazamo wake, hivi sasa wabunge wamekuwa wakitumia chombo hicho ambacho ni mhimili wa pili wa Tanzania kama ‘kijiwe’ cha kujitafutia umaarufu na sio kuwasilishia matatizo ya wananchi.

“Wabunge wa sasa wamekuwa wakilitumia Bunge kama sehemu ya kujitafutia umaarufu hivyo kutamka au kufanya kituko kwa kuamini watasikika na kuonwa badala ya kuwafikishia wananchi wao matatizo ili yatatuliwe na serikali,” alisema Mwesiumo ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Chama cha Wakulima Tanzania (Taso).

Alisema hata lugha ya kibunge kwa sasa imesahauliwa na baadhi ya wabunge na ndio maana imeshuhudiwa wakitukanana na kukejeliana kama watu wasio na heshima tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Aliongeza kuwa hata kama ni uhuru na kushamiri kwa demekrasia, bado wabunge wanapaswa kujiheshimu na kukiheshimu chombo hicho kwa kupingana kistaarabu na kubwa kuhakikisha matatizo ya wananchi wao yanawasilishwa na kutautiwa ufumbuzi kwa njia za kiungwana.

“Inapofikia mbunge anamkejeli kwa lugha isiyo na staha mbunge mwenzake au mbunge mwanasheria kumtusi mwanasheria mwenzake ni wazi nidhamu na hadhi ya Bunge inashuka, je wananchi walifikiriaje bunge la namna hiyo, nadhani ni wakati wa waheshimiwa hawa kubadilika ili kulirejeshea Bunge heshima yake,” alisema Jaji huyo aliyeitumikia Mahakama tangu mwaka 1974-1980 kabla ya kuwa mbunge wa Kilombero kwa awamu mbili za mwaka 1980-85 na 1990-1995.

CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa