Bondia Saidi Hofu wa Tanzania (kushoto) akioneshana ufundi wa kutupiana masumbwi na bondia Caristo Bwalia wa Zambia wakati wa mpambano wao wa kirafiki wa Kimataifa uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Mchezaji wa Timu ya Taifa ya Masumbwi (Tanzania) Mohamed Chibumbuli akiwa chini huku akihesabiwa baada ya kupata kichapo kutoka kwa bondia Mbachi Kaonga wa Zambia.
Meneja Mwendeshaji wa Kampuni ya Joker Club Olec Aleksejev (kulia) akitunishiana misuli na bondia wa timu ya Taifa ya Masumbwi Said Hofu baada ya kumkabidhi vifaa kwa ajili ya mchezo huo baada ya kuibuka mcherzaji bora wa mashindano kati ya Zambia na Tanzania.
Pichani juu na chini ni Wasanii wa kikundi cha Sanaa cha Zinduka Entertaiment cha Temeke wakitoa burudani kabla ya mpambano kati ya mabondia wa Zambia na Tanzania uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Mabondia wa ngumi za Ridhaa wa Tanzania wamechezea kichapo baada ya kupigwa michezo minne kati ya mitano iliyochezwa dhidi mabondia toka Zambia kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo.
Mapambano hayo ambayo yalikuwa ni ya kirafiki ya kimataifa yanayojulikana na Shirikisho la ngumi za Ridhaa Duniani AIBA yenye raundi tatu ilishuhudia Said Hofu akifungua pazia (kg 49) kwa kupigwa kwa pointi na Caristo Bwalia toka Zambia
Mpambano wa pili (kg 56) ulishuhudia Frank Nicolaus wa Tanzania akipigwa na Russel Mwamba wa Zambia kwa pointi pia.
Katika pambano la ( Kg 60) ndipo mtanzania Ismail Galiatano alimshushia ngumi nzito nzito John Chimpwele wa Zambia na kusababisha kuchanika juu ya jicho na kutokwa damu nyingi ndipo mwamuzi alisimamisha mchezo na kumpa ushindi Ismail Galiatano.(RSC)
Mpambano wa nne (kg 64) Mtanzania Kassim Hussein alipokea kipigo toka kwa Charles Lumbwe kwa kupigwa kwa pointi.
Funga kazi (kg 75) ikawa ndio usiseme maana Mohamed Chimbumbui alipigwa kwa TKO na Mbachi Kaonga wa Zambia baada ya kumsukumizia makonde mazito na kushindwa kuyahimili na kujikuta akianguka kila mara.
Katibu wa Chama ngumi za ridhaa, Makore Mashaga amesema wamepoteza mpambano huo lakini anashukuru wamepata mazoezi ya kujiandaa na mashindano ya ndani yanayotarajiwa kuanza Novemba 26 kwenye uwanja wa ndani wa taifa, jijini Dar es salaam.
Mabondia watanzania wamesema kupigwa kwao kunatokana na maandalizi hafifu waliyopata na mashindano kuahirishwa mara kwa mara pia kuliwafanya morali kushuka.
Naye Katibu wa Ngumi za Ridhaa wa Zambia Luteni Kanali Man Muchimba amesema amefurahi kucheza na watanzania kwani wamepata mazoezi ya kuwasaidia kucheza mashindano ya kanda ya tano yatakayofanyika nchini kwao mapema Desemba.
0 comments:
Post a Comment