Leo nimejipatia kitabu kiitwacho The Great Theft: Wrestling Islam From the Extremists. Mwandishi ni Khaled Abou El Fadl, profesa wa sheria katika Chuo Kikuu cha California, Los Angeles, ambaye kwenye jalada nyuma ya kitabu, ametajwa kuwa "one of the world's preeminent Islamic scholars and an accomplished Islamic jurist."
Nikitafsiri kwa ki-Swahili, ni kwamba mwandishi huyu ni mmoja wa wataalam wa u-Islam ambao wanaongoza hapa duniani na pia ni mwanasheria mahiri wa sheria za ki-Islam. Nimeanza kukisoma kitabu hiki leo hii. Tayari ninaona kuwa hiki kitabu ni moto wa kuotea mbali, kwa jinsi kinavyouelezea na kuutafsiri u-Islam kwa mujibu wa misahafu yake, na kwa jinsi kinavyowabomoa hao wanaoitwa wa-Islam wenye siasa kali. Mwandishi anawabainisha kuwa ni wapotoshaji, kwenye masuala kama nafasi ya wanawake katika u-Islam, jihad, haki za binadamu, ugaidi, na vita.
Kitabu hiki kinanikumbusha kitabu changu kingine, kiitwacho Muhammad: A Biography of the Prophet, ambacho nilikifurahia sana, nikakitaja katika blogu hii. Yeyote anayetaka kujielimisha kuhusu Mtume Muhammad S.A.W. ni vema akasoma kitabu hiki, ambacho gazeti la Muslim News lilikisifu kwamba kinaondoa umbumbumbu uliopo, na ni kitabu muhimu kwa wasio wa-Islam na wa-Islam pia.
Basi nimeona kuwa kitabu cha The Great Theft ni kimoja kati ya hivi vitabu vinavyofafanua kwa umahiri mkubwa ukweli kuhusu u-Islam, tofauti na yale yanayosemwa na hao wanaoitwa wa-Islam wenye siasa kali, ambao wameuteka nyara na wanaupotosha u-Islam. Ushauri wangu ni kuwa tuvisome vitabu hivi. Lakini je, kwa wa-Tanzania, ambao kwwa ujumla ni wavivu wa kujifunza lugha mbali mbali na ni wavivu wa kusoma vitabu, elimu hii itawafikia?
0 comments:
Post a Comment