Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » Kiu chatimua wahadhiri wake 35

Kiu chatimua wahadhiri wake 35


Chuo cha Kimataifa Kampala (Kiu), kimewatimua wahadhiri wake 35 kwa madai ya utovu wa nidhamu ikiwamo kutohudhuria darasani kwa wiki tatu.

Hata hivyo, wahadhiri hao wamedai kwamba kufukuzwa kwao kumesababishwa na kudai mishahara yao ya miezi tisa.

Mkurugenzi wa Kiu, Hassan Bassaja, alisema wahadhiri hao wamekiuka sheria za msingi za chuo hicho kwa kugoma kuingia darasani kwa wiki tatu mfululizo.

"Nimeamua kuwafukuza kazi wahadhiri hao kwa kuwa wamekiuka sheria zetu kwa kutoingia darasani kufundisha, kitu ambacho kimesababisha kuahirishwa mitihani kwa wanachuo mpaka Januari, mwakani," alisema Bassaja.

Hata hivyo, mmoja wa wahadhiri hao ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, aliliiambia NIPASHE kuwa kufukuzwa kwao kumechangiwa na kuidai menejimenti ya chuo mishahara yao ya miezi tisa.

Alisema walilazimika kutoingia darasani kwa lengo la kuishinikiza menejimenti iwalipe mishahara yao hiyo lakini uongozi imeamua kuwafukuza kazi.

"Tumefanya kazi kwa miezi tisa mfululizo bila kulipwa mishahara yetu na kila tukifikisha malalamiko yetu kwa Mkurugenzi amekuwa akiyapuuza na ndipo tulipoamua kugoma kufundisha," alisema mhadhiri huyo.

Hata hivyo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU), Profesa Sifuni Mchome, alisema wahadhiri hao lazima walipwe mishahara yao na suala la kuwafukuza kazi ni jambo tofauti kabisa.

"Walipwe mishahara yao kisha suala la kuwafukuza kazi litaangaliwa kwa undani zaidi. Maana hapa ni kama kuanzisha suala lingine wakati la awali bado halijashughulikiwa," alisema Profesa Mchome

Aidha, imedaiwa kuwa tayari uongozi wa chuo hicho umewaleta wahadhiri wengine 30 kutoka nchini Uganda kuchukua nafasi za wahadhiri waliofukuzwa kazi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick, amemuagiza Afisa Elimu wa Mkoa, Raymond Mapunda, kufuatilia suala hilo.

Sakick amemtaka pia Afisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, kulifikisha suala hilo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi pamoja na TCU.

Hata hivyo, Afisa Elimu mkoani Dar es Salaam, alisema tayari amewasilisha TCU malalamiko ya wahadhiri pamoja na wanafunzi wa chuo hicho na kuhakikishiwa kuwa suala hilo litafanyiwa kazi ipasavyo.

CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa