Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Msemaji wa Jeshi la Polisi, ASP, Advera Senso, baadhi ya silaha zilizosalimishwa na idadi yake katika mabano ni pamoja na shortgun (29), gobore (352), SMG (11), riffle (20), bastola (22), airgun (1), rocket launcher (2) na SAR (2).
Kutokana na tatizo la kuzagaa na matumizi holela ya silaha zinazomilikiwa isivyo halali na kinyume cha sheria nchini, Desemba 4, mwaka jana, Waziri Nchimbi aliagiza kuwa katika kipindi cha mwezi mmoja mtu yeyote ama kikundi chochote kinachomiliki silaha kinyume cha sheria kuzisalimisha katika vituo vya polisi au ofisi yoyote ya serikali iliyo karibu nao.
Waziri Nchimbi aliagiza pia silaha hizo kusalimishwa kwa wenyeviti wa serikali za mitaa, vijiji, vitongoji, wakuu wa wilaya, mikoa na madhehebu ya dini.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, zoezi hilo limefanyika kote nchini kuanzia Desemba 3, 2012 hadi Januari 4, mwaka huu mtu yeyote ambaye amesalimisha silaha yake ndani ya kipindi hicho cha msamaha, hakuna hatua zozote za kisheria zitakazochukuliwa dhidi yake.
ASP Senso katika taarifa hiyo alisema kuwa usalimishaji wa silaha kwa hiari umefanyika kwa mafanikio makubwa na kwamba msalimishaji ndani ya kipindi hicho hatabughudhiwa.
Senso pia aliongeza kuwa, baada ya kipindi hicho cha msamaha kumalizika, Jeshi la Polisi limejipanga vya kutosha kwa ajili ya kufanya oparesheni maalumu inayoendeshwa nchi nzima kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola pamoja na raia wema, kuwakamata wale wote wanaomiliki silaha kinyume cha sheria na waliokaidi agizo hilo.
Sambamba na hilo, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa kutoa taarifa za mtu ama kikundi cha watu wanaosadikiwa kujihusisha na umiliki wa silaha isivyo halali au matukio ya uhalifu wa aina yoyote ile na kwamba yeyote atakayewezesha kukamatwa kwa wahusika hao, atazawadiwa kiasi cha Sh. 100,000.
Wiki iliyopita, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ilisema kuwa zaidi ya silaha 310 tayari zilikuwa zimesalimishwa kwa hiari tangu kutolewa kwa tamko hilo mwezi uliopita.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment