Tamasha la muziki la kimataifa ambalo hufanyika kila mwaka la
‘World Music Day’ linafanyika leo (Ijumaa) katika viwanja vya posta Kijitonyama
jijini Dar es Salaam ambapo wanamuziki Kala Jeremiah, Ben Paul, bendi ya Twanga
pepeta na wengineo wanaotamba katika tasnia ya muziki nchini watalipamba
tamasha hilo.
Tamasha hilo ambalo limeandaliwa na Umoja wa Ulaya wa taasisi
za utamaduni (EUNIC) zikiwamo Aliance France-Dar es Salaam, Goethe
Institut-Tanzania na British Council linalenga kutoa fursa kwa wanamuziki
wakongwe na wachanga kukutana katika jukwaa hilo la kimataifa kutoa burudani
hiyo kwa wapenzi na mashabiki wa muziki.
Mratibu wa Tamasha hilo Abel Shuma ambaye pia ni Mratibu wa
Shughuli za Utamaduni Alliance France Dar es Salaam, anasema wanamuziki wengine
watakaotumbuiza kwenye tamasha hilo ni pamoja na Godzila, Barnaba na bendi yake,
mwanamuziki mkongwe wa Reggae Jhiko Man bila kusahau ngoma za asili kutoka kwa
kundi la Super Maya Baikoko na Makini Kids.
Kala analielezea onyesho hilo kama mazao ya kazi nzuri
aliyoifanya katika muziki wake “Nimepata faraja sana kualikwa kutumbuiza kwenye
world music day, inaonyesha ni kwa jinsi gani muziki wangu unakubalika na
kutambulika kitaifa na kimataifa” anaeleza na kuongeza “Kupitia show hii
naamini jina langu litakuwa juu na kuniletea show nyingine za kimataifa ndani
na nje ya nchini”
Juma Nassoro aka Super Maya ambaye kiongozi wa kundi la
Baikoko anasema “Tamasha hili tutalitumia kama kipaza sauti cha kutangaza
muziki wetu wa asili kitaifa na kimataifa”
Shirika la ndege la FasJet kupitia
kwa Afisa Masoko Mtendaji Lucy Mbogoro linajivunia kudhamini tamasha hilo likitumia
nafasi hiyo kurejesha shukran kwa Watanzania kwa mchango wao mkubwa katika
shirika hilo kwa kuchagua kutumia huduma zake za usafiri wa anga.
Mbogoro anasema “World Music Day ni fursa nzuri ya kukutana
na wadau wetu kwakuwa tamasha litawakutanisha watu wa mataifa mengi watapata
kujua huduma zetu katika wakati huu tunaoelekea kuanzisha safari za ndege za
kimataifa katika nchi za Afrika Kusini, Zambia na Rwanda”
Tamasha hilo ambalo limeandaliwa na European Union National Institutes For Culture (EUNIC),
ikiwemo Goethe
Institut Tanzania, Alliance
Francaise na British
Council pia limedhaminiwa na Pepsi, Total na balozi za Ujerumani na
Ufaransa.
0 comments:
Post a Comment