Home » » SHEIKH PONDA AANZA CHOKOCHOKO.

SHEIKH PONDA AANZA CHOKOCHOKO.

  Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Issa Ponda.
KATIBU wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, amewatangazia Waislamu kwamba mihadhara iliyopigwa marufuku na Serikali, itaendelea kufanyika kama kawaida na ataka yeendelea kuikataza watakabiliana naye kwa nguvu zote.
Sheikh Ponda aliyasema hayo jana katika Ukumbi wa Diamond Jubilee kwenye mamia ya Waislamu waliokusanyika kwa ajili ya kongamano la kujadili mada mbalimbali, ikiwamo uhuru wa Waislamu na haki zao na usalama wa watu, miradi na mali zao.

“Tunatoa tamko kwa Waislamu, mihadhara iliyopigwa marufuku itaendelea kufanyika kama kawaida, Waziri wa Mambo ya Ndani azingatie kauli hiyo, hatuogopi ujinga, tunataka utaratibu ufuatwe, atakayekataza mihadhara kufanyika tutakabiliana naye kwa nguvu zote,” alisema Ponda.

Alisema kwamba, Waislamu wamekuwa hawasikilizwi katika mambo mengi wanayoomba kufanyiwa, lakini kwa upande wa maoni waliyotoa katika Katiba Mpya wanategemea kuyaona yakiwamo.

“Endapo maoni ya Waislamu hayataonekana katika Katiba mpya, tutaanzisha mtiti hadi kiama, hatuogopi mtu, hapa tulipofikishwa hatukubali,”alisema Sheikh Ponda.

Alisema kwamba, walipeleka mapendekezo serikalini, kwamba iundwe tume ili waweze kupeleka madai yao, lakini hadi sasa tume hiyo haijaundwa.

“Kwa hiyo, hatutarudi nyuma kudai haki zetu, tutatumia mazungumzo, kuandika na kusema, kufanya mihadhara na makongamano, kufanya maandamano mchana na hatimaye kufanya maandamano usiku na mchana.

“Pia, tunatarajia kufikisha mahakamani kesi nzito tatu kuhusu viongozi, sitazitaja kwa kuwa bado ni mapema mno,” alisema.

Naye Sheikh Kondo Bungo, akizungumzia matukio yanayotokea nchini, alisema Serikali inayo majibu ambayo yanatakiwa kuwekwa wazi ili wananchi wayajue.

“Kuna dhana potofu imejengwa ili kuonyesha Waislamu ni hatari, Zanzibar kumetokea mauaji ya Padri Mushi, makachero kibao wamekwenda huko, baada ya siku mbili kanisa likachomwa, kweli kuna mzanzibari gani mwenye kuweza kufanya tukio kama hilo katika mazingira ambayo makachero wamejaa?

“Waislamu hatuna ugomvi na Wakrito, chuki iliyopo ya kidini inapandikizwa na Serikali, kwa hiyo wakiristo waungane na Waislam kuifanya Serikali iseme ukweli juu ya matukio hayo,”alisema Kondo.

Akizungumzia umoja wa Waislamu, Sheikh Nassoro Mohammed, alisema mkutano wao huo unathibitisha Waislamu ni wamoja na hawana ugomvi na Wakrito isipokuwa ugomvi wao upo kwa Serikali.

“Hatuna ugomvi na Wakristo bali ugomvi wetu upo kwa Serikali kwani kuna haki zetu tunalalamikia hatupewi, mtu akidai haki asipigwe badala yake asikilizwe na kueleweshwa, tunashangaa kuona watu wakiijibia Serikali kuhusu madai yetu,” alisema Mohammed.

Akizungumzia kufutwa kwa somo la dini kufanyiwa mtihani, Mwenyekiti wa Baraza la Wakuu wa Shule, Hussein Pilly, alisema wanacholalamikia wao siyo kufutwa kwa masomo ya dini bali kufutwa kwa mitihani ya masomo ya dini mwaka huu.

“Hakuna aliyesema Serikali imefuta somo la dini shuleni, somo la dini litaendelea kufundishwa, lakini halitafanyiwa mtihani, hicho ndicho tunacholalamikia kwa sababu wanafunzi watakata tamaa kulisoma,”alisema Pilly.

Kwa mujibu wa Pilly, kitendo cha somo la dini kutofanyiwa mtihani, kitasababisha madhara kwa Waislamu na Serikali kwa sababu somo hilo hadi kufikia hatua ya kukubaliwa kufanyiwa mtihani, mijadala ilifanyika na wadau wakakubaliana ingawa sasa mabadiliko yanafanyika bila wadau kushirikishwa

MTANZANIA.


0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa