Alisema uamuzi huo, umekuja baada ya kufanyika upekuzi dhidi ya askari hao, ambao walikutwa na hati ya akaunti ya benki inayotumika kuiibia Serikali, mikanda 82 ya askari wa jeshi hilo na stakabadhi na nyaraka za malipo mbalimbali yanayofanywa katika ukaguzi wa viwanda na majengo.
Waziri Nchimbi alitoa kauli hiyo mjini Dar es Salaam jana, wakati wa hafla ya ufungaji wa mafunzo ya maofisa na wakaguzi wasaidizi katika Chuo cha Maofisa wa Polisi Kurasini.
Alisema hatua ya kufukuzwa askari hao, ilifikiwa kutokana na tuhuma za wizi na kughushi nyaraka dhidi ya jeshi hilo.
Alisema baada ya kupata taarifa hizo, alilazimika kuunda timu ya uchunguzi ili kuweza kubaini ukweli uliofichika kwa askari hao.
Alisema timu ya uchunguzi iliongozwa na Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Advocate Nyombi, kutoka Kitengo cha Upelelezi Makao Makuu, huku akisaidiwa na Luteni Kanali Lidwino Mgumba, Kaimu Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
Wajumbe wengine wa timu hiyo, ni Kamishna Msaidizi wa Polisi Ahmed Msangi, Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Salum Hamduni kutoka Makao Makuu ya Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai ambaye alikuwa katibu wa kamati.
Alisema hata baada ya kupekuliwa na kuhojiwa, walikutwa na vielelezo husika ambavyo vilisaidia kuwatia hatiani askari hao.
Kutokana na hali hiyo, Waziri Nchimbi alisema tayari jalada dhidi yao limeshaandaliwa na kupelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wakati wowote watafikishwa mahakamani.
Waziri Nchimbi, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Joseph Mwasabeja ambaye ni Mkaguzi Msaidizi wa Zimamoto, Dankan Mwakajinga, Sajini Meja wa Zimamoto na Hashim Kapamba.
Wengine,ni Boniface Mbele na Kenned Kipali, ambao ni makoplo wa Jeshi la Zimamoto.
“Ni wazi kabisa hivi sasa hatuwezi kuvumilia vitendo vya aina yoyote vya kihalifu dhidi ya maofisa wa jeshi. Ninataka kuwahakikishia kati ya hawa watuhumiwa, mmojawapo ni Kamishna wa Mkoa wa Pwani, ambaye alitafutwa kwa zaidi ya siku tatu bila mafanikio,” alisema Waziri Nchimbi.
Alisema mwaka uliopita zaidi ya askari 100, walitimuliwa kazi kutokana na kukiuka maadili, wakiwemo wanafunzi zaidi ya 90, waliojiunga na Jeshi la Polisi bila kufuata utaratibu.
Awali akifunga mafunzo hayo, Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, alisema katu haamini ndoto za watu wanaoota kupewa dola ili waongoze nchi kama itatimia kutokana na tabia yao ya kudharau mamlaka zinazoongoza.
Alisema kama wataendelea na tabia ya kuwadharau na kutoheshimu mamlaka walizojiwekea, ni wazi wanapungukiwa sifa ya kupewa nchi.
Dk. Bilal, alionya katika siku za karibuni wameibuka wananchi ambao kwa sababu zao, wameamua kudharau amri zinazotolewa na vyombo vya dola.\
\
CHANZO : GAZETI LA MTANZANIA
0 comments:
Post a Comment