Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » Lipumba alibebesha JWTZ tuhuma nzito

Lipumba alibebesha JWTZ tuhuma nzito


*Adai wamehusika kutesa viongozi watano CUF

*Kanali Mgawe akanusha
CHAMA cha Wananchi (CUF), kimezidi kulitupia lawama nzito Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kuwa limewatesa vibaya viongozi wake waliokamatwa mkoani Mtwara wiki iliyopita.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mjini Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ilisema viongozi wa chama hicho, waliokamatwa wiki iliyopita, wameteswa kwa kupigwa na kuumizwa vibaya pasipo na kosa lolote.

“Jeshi la Wananchi wa Tanzania katika kambi ya Naliendele, wamewafanyia mateso makubwa viongozi wa CUF, akiwemo Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Uchaguzi na Bunge, Shaweji Mketo, ambaye alipigwa mpaka akazimia.

“Kibaya baada ya kipigo hiki, alichomwa sindano na kuwekewa dripu tatu za maji hospitalini ambazo hazikumsaidia kuzinduka mpaka ilipofika saa 10 alfajiri.

“Alfajiri hiyo hiyo askari jeshi wale walirudi, wakamlaza kifudifudi Mketo na kuanza kumpiga kwa fimbo katika miguu yake, walimpiga kwa saa nzima hadi walipochoka na kuondoka. Baadaye alianza kusikia maumivu makali maeneo yenye upasuaji (ubavuni na tumboni), anasema anahisi kuna matone ya maji au vitu laini vinadondoka ndani kwa ndani katika eneo alilofanyiwa upasuaji mkubwa, si vizuri.

“Mketo anasema wenzake watano ndio waliopigwa kuliko yeye, walipigwa kwa zamu na askari jeshi waliokuwa wakiingia ndani,” alisema Profesa Lipumba.

“Namuomba Rais Jakaya Kikwete asitishe mara moja vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu unaofanywa na askari mkoani Mtwara. Taarifa ninayoitoa inatokana na maelezo na utafiti uliofanywa na Naibu Katibu Mkuu, Julius Mtatiro, niliyemtuma kwenda Mtwara kufuatilia kukamatwa kwa Mketo na wenzake,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema viongozi hao, walitumwa Juni 26, mwaka huu na kuhudhuria kesi inayowakabili viongozi mbalimbali wa CUF katika mahakama ya Mtwara Mjini.

“Mketo alipotoka mahakamani alifanya kikao na wanachama wa CUF Mtwara Mjini, ambao walimueleza unyanyasaji na ukatili mkubwa ambao wanajeshi na polisi wanawafanyia wananchi wa Mtwara. 

“Palitolewa taarifa ya mwanamke mmoja aliyenajisiwa na ambaye aliripoti tukio husika katika kituo cha polisi cha Msimbati, kilichoko Mtwara na alipeleka polisi hadi ushahidi wa mipira ya kiume (kondomu), iliyotumika kumfanyia unyama huo, lakini polisi hawakuchukua hatua yoyote hadi leo,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema Mketo na wenzake walikamatwa katika eneo la Njia Panda, baada ya magari mawili ya kijeshi, moja likiwa aina ya TATA na lingine likiwa Defender ya jeshi kuziba barabara ghafla.

Alisema Mketo ambaye alikuwa anatumia gari lenye bendera ya chama, akitumia gari aina ya Nissan Patrol yenye namba T 866 BGW mali ya CUF, alizingirwa na askari jeshi zaidi ya 50 ambao walianza kuwapiga vibaya.

Aliwataja viongozi waliotekwa kwa kushtukizwa na vyeo kwenye mabano ni Shaweji Mketo (Naibu Mkurugenzi wa Oganaizesheni Uchaguzi na Bunge), Salum Hamis Mohamed (Mwenyekiti CUF Mtwara Mjini), Ismail Hamis Jamal (Mwenyekiti CUF Mtwara Vijijini), Ismail Bakari Njalu (Mwenyekiti wa vijana (JUVICUF) Mtwara Mjini), Said Issa Kulaga (Katibu CUF Mtwara Mjini) na Kashindye Kalungwana (dereva).

Alisema baada ya kuwakamata waliwashikilia mpaka siku iliyofuata ambako waliwakabidhi kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara.

Alisema viongozi hao, walifika katika mahakama ya Wilaya ya Mtwara Mjini na kusomewa mashtaka matatu katika kesi ya jinai namba 137 ya mwaka 2013.

Alisema shtaka la kwanza, ni njama za kutenda makosa kinyume na kifungu cha 384 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kama ilivyorekebishwa mwaka 2002, ambapo inadaiwa Juni 27, 2013 katika eneo la barabara ya Msimbati ndani ya Wilaya ya Mtwara Mjini, watuhumiwa kwa pamoja walipanga njama za kutenda makosa.

Shitaka la pili, ni kusanyiko lisilo halali kinyume na kifungu cha 74(1) na 75 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kama ilivyorekebishwa mwaka 2002 na kwamba shtaka hilo pia linakwenda kinyume na kifungu cha 43, 44 na 45 cha Sheria ya Polisi na Polisi wasaidizi kama ilivyorekebishwa mwaka 2002, ambapo inadaiwa siku hiyo hiyo, washitakiwa pamoja walifanya kusanyiko ambalo si halali ambalo lilisababisha kuvunjika kwa amani na kuleta hofu kwa wananchi.

Alisema shitaka la tatu ni kupanga na kuchochea ufanyaji wa makosa kinyume na kifungu cha 390 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kama ilivyorekebishwa mwaka 2002 ambapo inadaiwa siku hiyo katika eneo la barabara ya Msimbati kwa pamoja waliwachochea wananchi wa Mtwara kutenda makosa.

MASHARTI 

Alisema baada ya kuwekewa masharti magumu mahakamani, viongozi hao walipelekwa gereza kuu la Mtwara mjini. 

“Askari magereza walipowakagua walikataa kuwapokea, kwa sababu wao hawapokei wagonjwa kwani walithibitisha kupigwa na kuumizwa kikatili kwa wahusika wote sita. Iliwapasa askari polisi kuondoka nao wote katika gari la polisi na kuwapeleka Hospitali ya Mkoa wa Mtwara, hospitalini madaktari walijionea kipigo kikubwa walichopata maeneo mbalimbali ya miili yao, kibaya zaidi nao wakasema hawana dawa za kuwatibu,” alisema Lipumba.

KANALI MGAWE

Alipoulizwa jana kuhusiana na tuhuma hizo, Msemaji wa JWTZ Kanali Kapambala Mgawe, alisema madai hayo hayana msingi na kumtaka Profesa Lipumba aache vyombo vya dola vitimize wajibu wake.

“Sisi hatufanyi kazi kisiasa, sina uhakika kama askari wetu wanafanya mambo hayo, naelewa wapo Mtwara kulinda amani,” alisema Kanali Magawe.

CHANZO: MTANZANIA

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa