Home » » Mama Kikwete awataka watanzania kuthamini bidhaa zinazozalishwa nchini

Mama Kikwete awataka watanzania kuthamini bidhaa zinazozalishwa nchini


Na Anna Nkinda – Maelezo
1/7/2013 Watanzania wametakiwa kujifunza kuthamini  vitu vya kwao na kuona kuwa ni bora zaidi kwa kufanya hivyo hata wageni watavipenda  kwani bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi  hazitapandishwa thamani na watu kutoka nje. 

Mwito huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza kutembelea maonyesho ya 37 ya Biashara ya Kimataifa yanayofanyika katika  uwanja wa Mwalimu Nyerere uliopo barabara ya Kilwa wilayani Temeke jijini Dar es Salaam.

Mama Kikwete aliambatana  na Mke  wa Mfalme Mswati  wa Swaziland Inkhosikati  Lambikiza, Mke wa Makamu wa Rais wa Zambia Mama Charlotte Scott na  Mwakilishi wa Mke wa Rais Joseph Kabila wa Jamuhuri ya watu wa Congo ambaye ni Waziri wa Jinsia, Watoto na Familia Inagosi Bulo.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa walitembelea maonyesho hayo  ili  kuona shughuli mbalimbali zinazofanywa ndani na nje ya nchi  kuanzia ngazi ya juu hadi  chini. 

“Tumeona bidhaa za aina mbalimbali zinazozalishwa ndani na nje ya nchi na jinsi watu wanavyoweza kubadilishana uzoefu wa biashara hakika kadri siku zinavyozidi  kwenda kuna maboresho makubwa juu ya utengenezaji wa bidhaa zinazozalishwa nchini”, alisema Mama Kikwete.

Aliwashukuru wageni alioambatana nao kwa kuzipenda bidhaa zilizopo kwenye mabada ya watanzania na kuwaomba wananchi kutoka  maeneo mbalimbali ndani na nje ya mkoa wa Dar es Salaam kutembelea  maonyesho hayo kwani kuona ni kujifunza.

Pia  aliwapongeza na kuwashukuru wanawake kwa kazi kubwa wanazozifanya za kuzalisha bidhaa na kufanya biashara mbalimbali ambazo zimewasaidia  kujiletea maendeleo yao na jamii inayowazunguka.

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa