Na Anna Nkinda - Maelezo
Viongozi
wa dini nchini wametakiwa kuhubiri amani katika majukwaa yao ili jamii
ielewe umuhimu wa kuwepo kwa amani na kuendelea kuishi kwa upendo na
ushirikiano.
Wito
huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati
akiwafuturisha wanakijiji cha Hoyoyo wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.
Mama
Kikwete alisema kuwa viongozi wa dini wanajukumu kubwa la kuhakikisha
kuwa waumini wao wanaelewa umuhimu wa amani katika nchi kwa kujenga
mshikamano kama waasisi wa Tanzania walivyouanzisha .
“Katika
shughuli yetu hii tumekusanyika watu wa dini mbalimbali wanaofunga
mwezi huu na wengine mwezi mwingine lakini dua ni dua kupitia kwa
mwanadamu yeyote Mwenyezi Mungu inamfikia, hivyo basi tuzidi kushikamana
kwa kila jambo”.
Aliendelea
kusema kuwa amani inatafutwa kwa miaka mingi lakini inaweza kutoweka
kwa muda mchache hivyo basi kila mtu hasa viongozi wa dini watumie muda
wao kuhubiri umuhimu wa amani katika nchi na neno amani
lisitoweke ndani ya vinywa vyao.
Kwa
upande wake Sheikhe Athuman Kinyozi alimshukuru Mama Kikwete kwa futari
aliyoiandaa kwa ajili yao na kusema kuwa mtu anayejitoa kwa ajili ya
kufuturisha wengine anapata thawabu kwa Mwenyezi Mungu.
Sheikhe
Kinyozi alisema kuwa kufanya kitendo cha kufuturisha si lazima uwe na
uwezo mkubwa kifedha bali unaweza ukanunua hata tende au maji na kuwapa
watu waliofunga kile ulichowapa kikiwa ni kitu cha kwanza kutia midomoni
mwao utalipwa thawabu za funga ya wale wote uliowapa kitu walichokula.

0 comments:
Post a Comment