Home » » Rage aigeuka Yanga kweupe

Rage aigeuka Yanga kweupe

Dar. Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage amesema msimamo wa Simba ni kwamba kukitokea mdhamini katika Ligi Kuu Bara, inapaswa kila klabu ipewe mgao sawa.

Rage alisema Azam wanakuja kuonyesha Ligi Kuu kwa hiyo sisi tunaomba tupewe mgao sawa na klabu nyingine. Tusiwe wabinafsi.

Kauli hiyo ya Rage inapingana na ile aliyotoa wiki chache zilizopita aliposema kwamba hawawezi kupewa mgao sawa na klabu nyingine wakati wao na wapinzani wao Yanga ni timu kubwa na kutangaza kuweka mkakati wa kuhakikisha wanagomea mkataba huo wa Azam.

Awali, Yanga na Simba waliungana kutaka walipwe zaidi ya klabu nyingine ambazo kila moja itapewa Sh100 milioni kutoka kwa Azam TV, itakayokuwa na haki ya kuonyesha mechi za Ligi Kuu.

Hata hivyo, usiku wa kuamkia jana Rage alichekelea mamilioini ya Azam na kuwageuka mahasimu wao Yanga ambao walipanga wote kugomea mkataba huo na badala yake kuukubali ule wa SuperSports.

Katika sherehe hiyo Simba iliingia mkataba wa Sh331 milioni na Kampuni ya Azam Media ili kipindi cha Simba TV kiwe kinaonekana katika televisheni ya Azam (Azam TV).

Katika hafla Simba walikabidhiwa Sh100 milioni ambazo ni kwa ajili ya udhamini wa mwaka wa kwanza zilizokabidhiwa kwa Rage. Mwaka wa pili, Simba itapewa Sh110 milioni na mwaka wa tatu watapokea Sh111 milioni.

“Huu ni mkataba wa aina yake, yaani siku ya kwanza tu tumepewe hundi ya Sh100 milioni,” alitamba Rage.

Rage alisema bajeti ya Simba kwa mwaka ni Sh1.6 bilioni, lakini kiasi walichokipata kutoka Azam, wakipata na fedha za mauzo ya Emmanuel Okwi Sh480 milioni pamoja na Sh100 milioni nyingine ambazo watapewa na Azam Tv za udhamini wa ligi, hiyo itafanya Simba kuwa na akaunti iliyojitosheleza.
Chanzo: Habari Leo

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa