Home » » Vodacom kufunga laini 450,000 kwa kutosajiliwa kisheria.

Vodacom kufunga laini 450,000 kwa kutosajiliwa kisheria.

Zaidi ya wateja 450,000 wa  Kampuni ya Vodacom Tanzania huenda wakakosa fursa ya mawasiliano kutokana na kushindwa kufanya usajili wa kisheria wa namabari zao za simu na hivyo kuilazimu Vodacom kuzifunga nambari hizo.
Uamuzi huo wa Vodacom umekuja baada ya kumalizika kwa kipindi cha usajili wa nambari zote za simu za mkononi nchini Julai 10 mwaka huu.
Akizungumza ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Vodacom Tanzania, Bw. Rene Meza, alisema kuwa ingawa sio jambo linalofurahisha lakini kama kampuni ni lazima iheshimu na kuzingatia sheria na kanuni za nchini na hivyo watazifungia nambari hizo
“Sheria mpya ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta   (EPOCA) ya Mwaka 2010,  imeainisha kifungu kinachoelekeza Makampuni ya Mawasiliano, namna ambavyo wateja wake wanatakiwa kusajili namba zao za simu za mikonon
“Tulikuwa na muda wa kutosha kwa wateja wetu kutekeleza wajibu huo wa kisheria huku tukitoa fursa na njia nyingi zaidi kuwawezesha kusajili nambari hizo kwa urahisi na wepesi kutumia maduka yetu na pia mawakala wa M-pesa nchi nzima na kwamba baada ya kumalizika kwa muda wa ukomo wa kufanya hivyo hatuna budi kuitekeleza sheria kwa vitendo kwa kuzifungia nambari zote ambazo hazijasajiliwa.”Alisema Meza
Meza amesema hadi kufikia Julai 10, kampuni yake imebaini kuwa takribani laini 450,000 hazijasajiliwa na ndizo ambazo zitakazofungwa.

“Tunapenda kuwashukuru wateja wetu kwa muitikio wao wa kujisajili na pia kwa uvumilivu wao wakati wa utekelezaji wa utaratibu huu wa usajili wa nambari za simu  na uhakiki wa namba na taarifa za wateja ,” alisema.Meza na kuongeza “Tumekuwa na mafanikio makubwa kutokana na idadi kubwa ya wateja wetu kujitokeza kusajili nambari zao, hili ni jambo jema kwao na kwetu sisi, na ni Imani yangu kwamba wale wote waliojisajili wataendelea kufurahia huduma za mtandao wa Vodacom.”

Kuhakiki usajili wa nambari Mteja wa Vodacom anaweza kupiga  *106 #.
Usajili wa namba za simu si chaguo mbali ni suala linaloendana na Sheria mpya ya EPOCA, ambayo inaelekeza wateja wanaotumia namba za simu ambazo hazijasajiliwa na ni kosa kwa mteja kutumoia nambari ambayo haijasajiliwa huku akikabiliwa na adhabau ya  ya Shilingi 500,000 au kifungo cha miezi mitatu au vyote kwa pamoja.

Awali Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilitoa tarehe ya mwisho ya kusitisha zoezi la usajili wa namba za simu za mikononi kuwa  Juni 1, 2013 kabla ya  kusogeza mbele hadi Julai 10, 2013 ili kuwapa fursa wateja ambao hawajakamilisha usajili kufanya hivyo kuepuka kukatiwa mawasiliano.

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa