Home » » Wananchi wampora polisi SMG, risasi 30

Wananchi wampora polisi SMG, risasi 30

IGP Said Mwema,Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini.

  Wampiga mtama,wamshambulia kwa mawe
Watu 18 wametiwa mbaroni mkoani Singida kwa tuhuma za kumpora askari polisi bunduki aina Sub Machine Gun (SMG) na risasi zake 30 baada ya kumshambulia kwa mawe na fimbo.
Bunduki hiyo ni yenye namba za usajili 14300650.

Kamanda wa Polisi mkoani Singida, Geofrey Kamwela, alisema tukio hilo lilitokea Jumatatu wiki hii saa 11:15 jioni katika kijiji cha Milade kata Iguguno tarafa ya Kinyangiri wilayani Mkalama.


Kamanda Kamwela alisema askari polisi huyo akiwa na mwenzake, walikwenda katika kijiji hicho kwa nia ya kuchukua ng’ombe watano kama ushahidi waliokuwa wameibiwa katika kijiji cha jirani cha Mukulu, wilayani Iramba.

Imeelezwa kwamba wananchi walifanikiwa kuwapata ng’ombe hao watano na kumkamata mtuhumiwa Ramadhan Mohamed (33), wa kijiji cha Milade kisha kumpeleka kituo kidogo cha polisi cha  Iguguno.

Kwa mujibu wa Kamanda Kamwela, ng’ombe hao mali ya Samwel Mlata (71), mkazi wa kijiji cha Mukulu, baada ya askari hao kuripoti ofisi ya kijiji cha Milade, hawakuwakuta ng’ombe hao, kitendo ambacho askari hao walidai hakikufuata taratibu za kisheria.

Kutokana na hali hiyo, ilibidi askari hao wakiwa na uongozi wa kijiji kuwafuatilia ili wakiwapata ng'ombe hap waondoke nao hadi kituo cha polisi kwa ajili ya taratibu zaidi.

Hata hivyo, baada ya kufanikiwa kuwakuta ng'ombe hao, wananchi waligoma kuwaachia.

Wakati wakiendelea na majadiliano, ghafla mwananchi mmoja alimrukia askari mwenye silaha miguuni na kumwangusha chini na wengine wakaanza kumshambulia kwa mawe na fimbo, hali iliyomfanya aanguke chini silaha yake.

Baada ya askari huyo kudondoka chini, wananchi hao waliichukua silaha hiyo pamoja na ng’ombe wale watano na kutokomea porini.

Kamanda Kamwela alisema askari huyo alijeruhiwa vibaya kichwani na mkono wake wa kushoto.

Alisema alipelekwa katika Zahanati ya Iguguno ambako alitibiwa na kushonwa nyuzi tano kichwani akaruhusiwa kurejea nyumbani na hali yake kwa sasa inaendelea vizuri.

Kamanda Kamwela alisema baadaye, askari polisi kwa kushirikiana na wananchi na Ofisa Mtendaji kijiji cha Mukulu, Huruma Dickison, waliipata silaha hiyo ikiwa imetelekezwa porini.

Alisema kupatikana kwa silaha hiyo kulitokana na taarifa walizopewa na raia wema.

Kamanda Kamwela alisema baada ya kukamilika kwa upelelezi, watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayowakabili.

Aidha, ameiomba jamii kushirikiana na polisi ili kudumisha amani na usalama wa wananchi.

CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa