Home » » WIVU WA MAPENZI WASABABISHA MFANYA BIASHARA KUWAGONGA WATU SITA BAA

WIVU WA MAPENZI WASABABISHA MFANYA BIASHARA KUWAGONGA WATU SITA BAA

POLISI mkoani Dar es Salaam wanamshikilia mfanyabiashara Heaven Kassia (44) mkazi wa Bahari Beach kwa tuhuma za kuwagonga watu sita kutokana na wivu wa mapenzi pamoja na kujaribu kujinyonga. Kamanda wa Polisi Kaanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema mtuhumiwa huyo alikuwa anakunywa katika baa ya Kilongawima Resort akiwa na rafiki yake wa kike, Jovita Njunwa ambaye pia ni mfanyabiashara.
Aliwataja watu waliogongwa na mfanyabiashara huyo kuwa ni Solomoni Kirato, Peter Marwa, Yahaya albert, Noah Mmari na wengine ambao majina yao hayajafahamika.

Kova alisema wakati akiwa katika baa hiyo meza ya pembeni walikuwapo watu wapatao sita ambao nao walikuwa wakinywa pombe.

Alisema mwanamke huyo alihama katika meza ya rafiki yake na kwenda katika meza iliyokuwa na wanaume hao sita bila maridhiano na rafiki yake.

Kamanda alisema kitendo hicho hakikumfurahisha Kassia hivyo ilizuka tafrani kati yake na watu hao sita kwa kurushiana maneno makali katika kumgombea Jovita.

"Mlalamikaji alidai kuwa Jovina ni rafiki yake na amekwisha kumgharamikia fedha nyingi na hivyo akawa anawalalamikia wanaume hao kwa kumchukua mwanamke huyo.

"Pamoja na malalamiko hayo lakini hakufanikiwa kumrudisha mwanamke huyo kwenye meza yake na hivyo akapandwa na hasira na kumuagiza kijana mmoja akamletee gari lake la Toyota Hilux.

"Kilichotokea ni kwamba aliingia katika gari hilo na kuwasha na kuondoka kwa mwendo kasi kuelekea katika meza ya watu hao sita na kuwagonga.

"Watu sita waliumia vibaya kwa kujeruhiwa miguu, mbavu, kichwa na sehemu nyingine,” alisema Kova.

Kamanda alisema baada ya tukio hilo mtuhumiwa alijaribu kujinyonga lakini aliokolewa na ndugu zake.

Mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya jalada kupelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

CHANZO GAZETI LA MTANZANIA

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa