Waziri
wa Ujenzi, Dk John Magufuli ametoa mwezi mmoja kwa watumishi wa
Serikali ambao wanadaiwa mikopo ya nyumba kulipa madeni yao mara moja na
kuonya kwamba ikiwa watashindwa kulipa, watanyang'anywa nyumba hizo na
watakopeshwa watu wengine.
Dk
Magufuli ameibuka na hoja hiyo mpya, zikiwa ni siku chache tangu
alipopigwa 'stop' na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutekeleza sheria ya
kuondoa msamaha wa asilimia tano kwa mizigo inayozidi kwenye malori,
hali ambayo ilizusha mvutano mkubwa baina ya Serikali na wasafirishaji
wa mizigo nchini.
Akizungumza
wakati wa kuweka jiwe la msingi kuzindua ujenzi wa nyumba 851 za
watumishi wa Serikali eneo la Mabwepande jijini Dar es Salaam, Dk
Magufuli alisema watumishi 2500 hawajalipa mikopo ya nyumba walizonunua.
Dk
Magufuli alionya kuwa atafuatilia suala hilo na kuhakikisha madeni hayo
yanalipwa mara moja, huku akimwomba Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib
Bilal kumuunga mkono kwenye jambo hilo, ambalo ni utekelezaji wa sheria
za nchi.
"Naomba
ifahamike kwamba tunapojenga nyumba kwa ajili ya kuwakopesha watumishi
wa umma tunataka kuboresha makazi yao. Pia fedha tunazokusanya
zinasaidia kujenga nyumba zaidi," alisema Dk Magufuli. Hata hivyo
alisema hadi sasa watumishi wa Serikali 4,900 ambao walikopa nyumba hizo
tayari wamelipa madeni.
"Mimi
nafanya kazi kwa kufuata sheria na kila mtumishi wa Serikali anafahamu
jambo hilo, hivyo watu ambao wanajua tunawadai wakae kwa tahadhari,
kwani ndani ya mwezi mmoja kama hawatalipa tutawachukulia hatua bila
kupuuzia," alionya Magufuli.
Hii
siyo mara ya kwanza kwa Dk Magufuli kutangaza kunyang'anya nyumba hizo,
kwani alifanya hivyo mwishoni mwa Machi mwaka jana pale alipouagiza
uongozi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kuwapa siku saba watu wote
walionunua nyumba hizo kulipa madeni yao.
Dk
Magufuli aliwataka TBA kutoa ilani ya maandishi inayowataka wahusika
walipe fedha hizo ndani ya wiki moja vinginevyo wangenyang'anywa kwa
maelezo kwamba wanachelewesha malengo ya TBA kujenga nyumba zaidi. Hata
hivyo, hakuna taarifa zozote zilizowahi kutolewa kuhusu kutekelezwa kwa
amri hiyo iliyotolewa zaidi ya miezi 18 iliyopita.
Jana,
Makamu wa Rais, Dk Bilal alimuunga mkono Magufuli akisema: "Naunga
mkono tamko la Waziri wa Ujenzi kwamba ni lazima watumishi wa Serikali
ambao wanakopeshwa nyumba walipe haraka ili fedha hizo zisaidie kujenga
nyumba nyingine."
Dk
Bilal alikuwa mgeni rasmi katika shughuli ya kuweka jiwe la msingi la
ujenzi wa nyumba 851, kwenye eneo la Bunju 'B' Kinondoni, Dar es Salaam.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa TBA, Elius Mwakalinga, alisema ujenzi huo
unafanyika kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza iligharimu Sh2 bilioni
na awamu ya pili Sh1 bilioni.
"Nyumba
851 zinazojengwa Bunju B ni sehemu ya ujenzi wa nyumba 4,400 katika
Mkoa wa Dar es Salaam na nyumba 10,000 kwa nchi nzima," alisema
Mwakalinga.
Hafla
hiyo ilisimama takriban kwa dakika 10 wakati Dk Bilal akitaka kuhutubia
baada ya jenereta kushindwa kufanya kazi, hivyo kumlazimu kurudi kuketi
kwenye kiti hadi umeme uliporejea. Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan
Rugimbana alilazimika kwenda kufuatilia suala hilo na mafundi
waliokuwapo walifanikiwa kuunganisha mashine za kipaza sauti na umeme wa
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), hivyo Makamu wa Rais aliendelea
kuhutubia.
Uuzaji wa nyumba
Nyumba
nyingi za Serikali zilijengwa kipindi cha utawala wa ukoloni wa
Wajerumani uliodumu kati ya 1885 na 1919 na ule wa Waingereza ulioanza
1919 hadi 1961.
Taarifa
zilizopo zinaonyesha kuwa nyumba za Serikali zilizouzwa nchi nzima
tangu mwaka 2002 wakati wa uongozi wa awamu ya tatu chini ya Rais
Benjamin Mkapa ni zaidi ya 6,000. Malengo ya kuuza nyumba ni kwamba,
fedha zilizopatikana zingetumika kujenga nyumba nyingine kwa ajili ya
watumishi wa Serikali katika maeneo mbalimbali nchini yakiwamo Dar es
Salaam, Arusha, Dodoma na Mwanza.
Hata
hivyo, uuzaji huo ulikuwa na utata hali iliyosababisha kupingwa vikali
na watu wa kada mbalimbali wakiwamo wanasiasa na wanaharakati, kwa
maelezo kwamba uliwanufaisha vigogo.
Malalamiko
pia yalijengwa kwenye hoja kwamba nyumba hizo ziliuzwa kwa bei ndogo
ambayo haikuzingatia thamani ya ardhi husika, huku wengine wakisema
hakukuwa na umakini kwani viongozi wengi walikosa makazi na hasa wale
walioteuliwa baada ya Rais Jakaya Kikwete kuingia madarakani.
Miongoni
mwa walionunua nyumba hizo ni mawaziri wengi, kama si wote, wakati wa
Serikali ya Awamu ya Tatu, hasa katika mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma,
kwa kuwa walikuwa wakiishi katika nyumba hizo.
Hali
hiyo ilisababisha viongozi mbalimbali wakiwamo mawaziri, majaji, wakuu
wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa ngazi mbalimbali na viongozi
wengine kukaa hotelini na kuisababishia Serikali gharama kubwa.
Tatizo
lingine lililoibuka ni kuwa baadhi ya nyumba zilizouzwa zilikuwa ndani
ya maeneo ya jeshi na hasa Polisi, hivyo kuilazimisha Serikali ya awamu
ya nne ilipoingia madarakani kulazimisha kurejesha baadhi ya nyumba
hizo.
Hata
hivyo, kulikuwa na ugumu katika urejeshaji kwani baadhi ya waliouziwa
tayari walikuwa wamezibomoa na kuanza upya ujenzi wake na wengine
walikuwa tayari wamezipangisha kwa mabalozi, kampuni binafsi, mashirika
yasiyokuwa ya kiserikali (NGOs) na nyingine kujengewa maduka ya biashara.
MWANANCHI
MWANANCHI

0 comments:
Post a Comment