Dar es Salaam. Suala la gesi lilizua balaa jana wakati wa mkutano wa
wadau wa sekta hiyo baada ya malumbano makali kati ya Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi na Mwenyekiti wa Mfuko wa
Sekta Binafsi (TPSF), Dk Reginald Mengi.
Maswi na Mengi walitofautiana juu ya suala la nafasi ya wawekezaji
wazawa kwenye sekta hiyo ya gesi katika kongamano la pili la wadau wa
mafuta na gesi jana jijini Dar es Salaam.
Malumbano hayo yalichochewa zaidi na kauli iliyotolewa juzi na Waziri wa
Nishani na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ambaye alisema kuwa wazawa
wana uwezo mdogo wa kuwekeza katika sekta hiyo.
Mengi arusha kombora
Mengi ndiye aliyeanza mashambulizi pale alipotaka wazawa wapewe kipaumbele kwenye uvunaji wa mafuta na gesi.
“Tunaambiwa sisi hatuna fedha. Eti hela zetu ni kwa ajili ya kufanyia
biashara ya matunda. Lakini tunayo ardhi, Tanzania siyo nchi maskini,
gesi ni mtaji wetu, tuweke mkakati wa kugawana hii rasilimali,” alisema
Mengi na kuongeza;
“Huku ni kuwa maskini wa fikra na tutakuja kuulizwa na Mwenyezi Mungu.
Kama Serikali haina sera itauzaje rasilimali zetu kwa wageni?
Tusingependa kuyazungumza haya hadharani, lakini tunasema tu. Mtu mwenye
hekima pale wizarani wa kutusikiliza ni Maswi peke yake.” Mengi alisema
anataka kuona Serikali ikitumia mfumo wa taifa la Nigeria kwa kutoa
kipaumbele kwa wazawa.
“Mimi katika masuala ya uwekezaji kwa kweli `role model’ (kivutio) ni nchi ya Nigeria,” alisema Mengi.
Mwakilishi wa taasisi
za dini ashindilia
Baada ya Mengi kukaa, alisimama Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili na Haki
za Jamii, Mchungaji William Mwamalanga alisema Serikali inatakiwa
kukubaliana na hoja za Watanzania katika uwekezaji wa sekta hiyo.
Mchungaji Mwamalanga aliongeza kuwa huu siyo wakati wa kuendelea kuwaachia wawekezaji hatua zote katika rasilimali ya Tanzania.
“Lazima tujifunze kwa mataifa kama Nigeria, serikali yao imetoa nafasi
ya mwananchi kusimamia, yaani mwekezaji akiingia lazima apitie kwa
mwekezaji wa ndani kabla ya kufanya mazungumzo na serikali. Kwa nini
tusifanye hivyo pia? “alihoji Mchungaji Mwamalanga.
Mbali na hilo Mchungaji Mwamalanga alisema Serikali inatakiwa kukiri dhambi ya kuingia mikataba bila kuwapo kwa sera ya gesi.
Maswi ajibu mapigo
Baada ya Mengi na wajumbe wengine kutoa maoni ya kuilaumu Serikali,
Maswi alitakiwa kutoa maelezo ya Serikali kuhusiana na suala hilo.
Maswi alionyesha wazi alikuwa amepandwa na jazba kufuatia maoni ya
kuiponda Serikali na hakuchelewa kuanza kuwakosoa Mengi na wadau
wengine.
“Katika andiko letu tumeandika, nawahimiza mkalinunue, tumewagusia
wazawa ambao watahusishwa katika ununuzi wa vitalu. Hakuna aliyesema
kuwa sekta binafsi haitashirikishwa,” alisema Maswi huku akifoka.
Maswi alisema kuna mambo mengi ambayo Watanzania wanayo fursa ya
kushiriki katika uwekezaji wa sekta hiyo na siyo kukaa majukwaani na
kuzungumza kwa unafiki.
Aidha, aliongeza kuwa mpaka sasa hajaona kampuni yenye uwezo mkubwa hapa
nchini katika ushiriki wa moja kwa moja katika uwekezaji wa sekta hiyo.
“Tusijidanganye kwa vikampuni vidogovidogo tulivyonavyo, tukadhani kama
vinaweza kuingia kwenye ushindani wa moja kwa moja. Vikampuni vyenyewe
vimejaa rushwa tu za kuhonga, hakuna lolote tuache ubabaishaji, “
alisema Maswi. Aliukosoa pia mtindo wa uwekezaji wa Nigeria ambao Mengi
ameupendekeza:
“Mengi kaka yangu, hakuna suala la mjomba katika masuala ya uwekezaji.
Huo mtindo wa Nigeria siyo mzuri, huwezi kuwapa watu wachache rasilimali
wakati wengi wakiwa kwenye umaskini. Nigeria imejaa vurugu na hatuwezi
kuichukulia kama mfano mzuri,” alisema Maswi na kuongeza:
“Jukumu letu kama wizara na kila ninapokutana na ninyi, nakutana kama
Katibu Mkuu, siyo Maswi. Lengo letu ni kuwaeleza kinachoendelea na jinsi
ya kuwawezesha wazawa.”
Akijibu hoja ya Mchungaji Mwamalanga, Maswi aliwataka viongozi hao kushirikiana na Serikali badala ya kuinyooshea kidole.
“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iko tayari kukutana na
kundi lolote. Mkitaka tuonane, leteni barua tu. Tuko tayari na hatufichi
kitu,” alisema na kuongeza: “Tatizo la nchi yetu watu ni kulalamika tu,
fanyeni kazi... Mkitusaidia maaskofu, tutatoka hapa tulipo, siyo
kutunyooshea tu vidole.
Maaskofu wenyewe wanakula rushwa, wanafanya vitu vya ajabu, mbona sisi
hatuwanyooshei? Au tuwataje? Kwa sababu msione tu Serikali ni watu
wabaya, `no, let’s work as a team’,” alisema Maswi.
Aliendelea kusisitiza kuwa fursa ya uwekezaji ipo kwa watu wote bila kujali wa ndani au wa nje.
“Hakuna mtu anayekuja hapa ambaye ni mjomba wenu. Sasa kama nyie mnakaa nyuma nyuma, hebu muwekeze basi.
Hivyo vitalu tumetoa, nani ametaka `document’ tumemkatalia? Watu
wanakuja wanaleta hela, sasa tuzikatae?” Kuhusu sera na sheria ya gesi
na mafuta, Maswi alisema sheria ipo ila sera itakamilika ifikapo Mei
mwakani.
“Nawaahidi hadi mwisho wa mwaka huu tutakuwa na sera ya wazawa, hivyo
nawaomba mshiriki kutoa maoni. Kama tunayo sheria tangu mwaka 1970 na
1980 tunataka nini tena? Tunataka sera au sheria? Nadhani sheria ni
kubwa zaidi, huwezi kwenda kinyume na sheria. Hata hivyo, sera tunayo
tangu Oktoba mwaka huu, lakini bado iko kwenye mchakato. Itakamilika
ifikapo Mei, 2014,” alisema Maswi.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment