Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala Mhe Jerry Silaa (wa
pili kushoto) akizungumza na waandishi wa habari leo asubuhi kuhusu
kampeni ya ‘Dawati ni Elimu’ kupitia wasanii mbalimbali wa kuchora
nchini. Kulia kwake ni Msanii Robin Mtila na Kushoto ni Meneja Mkuu wa
Hyatt Regency Kilimanjaro, Trevor Saldanha na Mustafa Hassanali Mratibu
wa Kampeni hiyo.
Meneja Mkuu wa Hyatt Regency Kilimanjaro, Trevor Saldanha
akizungumzia mchango wa hoteli yake katika kampeni ya Dawati ni Elimu
yenye kauli mbiu ya "Kalisha mmoja boresha Elimu".
Mchoraji Robin Mtila akizungumza kwa niaba ya wasanii wenzake
ambapo ameelezea umuhimu wa sekta ya Elimu katika fani ya sanaa nchini.
Mkurugenzi wa Advert Construction Ltd Dhmy Jog akizungumza na
waandishi wa habari baada ya kampuni yake kuchangia Tsh 10 milioni
kwenye kampeni hiyo ya kuondoa tatizo la madawati katika shule za msingi
na sekondari nchini.
Baadhi wasanii watakaoshiriki kwenye tamasha kubwa la Sanaa lenye lengo la kuchangia kampeni ya Dawati ni Elimu.
Mkutano na waandishi wa habari ukiendelea.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala Jerry Silaa akiwa katika
picha ya pamoja na wasanii wa Sanaa ya Uchoraji pamoja na baadhi ya
wadhamini wa kampeni hiyo.
.Kampeni ya Dawati ni Elimu yakusanya Tsh 1bilioni mpaka sasa lengo ni kufikia Tsh 4.98bilioni
.atoa wito kwa watanzania kujitokeza kwa wingi siku ya tamasha la mwaka dawati ni elimu
Na Moblog Team
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala Mhe Jerry
Silaa akishirikiana na Hyatt Regency Kilimanjaro Hotel na wasanii kumi
maarufu nchini wameandaa tamasha kubwa la sanaa la mwaka kwa wasanii wa
kuchora (Painters) lenye lengo la kuchangia kampeni ya “Dawati ni Elimu”
katika shule za msingi na sekondari jijini Dar es Salaam. Moblog
linaripoti
Akizungumza na waandishi wa habari leo
jijini Dar es Salaam, Mhe Silaa amesema kuwa katika kampeni hiyo ya
‘Dawati ni Elimu’ kupitia programu ya (Annual Mayors Charity Ball)
wameamua tarehe 16 ya mwezi Novemba kuwa na tamasha la sanaa ya uchoraji
itakayowashirikisha wasanii kumi maarufu nchini.
“kwenye tamasha la tarehe 16 mwezi Novemba
mwaka huu wasanii wa kuchora wataweza kuchora picha mbalimbali kwa
ubunifu wao na kuweza kuonyesha kazi zao pamoja na kuuza kwa wateja
katika Hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro Hotel na sehemu ya mapato
yatachangia madawati na asilimia zingine itakuwa faida yao baada ya
mauzo kwenye maonyesho ya picha ,” amesema
Amesema kuwa katika tamasha hilo la sanaa ya
kuchora wasanii wataweza kuonyesha kazi zao za sanaa katika harakati za
kuhamasisha jamii kuchangia kupunguza tatizo la madawati kwenye shule
za msingi na sekondari kupitia kauli mbiu ya “Kalisha mmoja, boresha
elimu”
Silaa aliongeza pia kwamba katika tamasha
hilo la mwaka pia kutakuwa na chakula cha mchana kwa wageni wote
wataohudhuria Shughuli hiyo ambayo itakuwa ya wiki nzima katika
kuhakikisha lengo hilo la kupata madawati kwenye shule linafanikiwa.
Amesema kuwa kwa sasa takwimu zinaonyesha
asilimia 30 ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wanakaa chini
kwa kukosa madawati katika shule nyingi za kata mkoa wa Dar es Salaam.
Alisisitiza kuwa ofisi yake kwa kushirikiana
na Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Ilala wanatafuta njia bora ambayo
wachangiaji wanaweza kuchangia kupitia mitandao ya simu ili kuhakikisha
wananchi wote wanapata fursa hiyo adhimu na pesa za wananchi zinafanya
kazi iliyokusudiwa.
“watanzania ni lazima waamke ili waweze
kuchangia maendeleo ya elimu nchini katika kusukuma mbele maslahi mapana
ya nchi kwa siku za usoni ili taifa letu liweze kuwa na wananchi
waliopata elimu bora na si bora elimu,” alisisitiza Mhe Silaa
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Hyatt Regency
Kilimanjaro, Trevor Saldanha amesema kuwa ni sehemu ya mpango wa hoteli
hiyo kurudisha faida wanayopata kwenye jamii ili kusaidia kupunguza
matatizo na changamoto mbalimbali katika sekta ya elimu.
“Ni muhimu kwa wafanyabiashara kushirikiana
na jamii inayoitumikia na tutaendelea kusaidia jamii katika siku za
usoni tukiwa kama sehemu ya jamii husika,’ amesema
Naye Mkurugenzi wa Advert Construction Ltd
Dhmv Jog amesema kampuni yake inatambua umuhimu wa sekta ya elimu kwa
manufaa ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla katika kufuta ujinga.
Amesema kampuni yake kupitia kitengo chake
cha kusaidia jamii kimetoa Tsh 10milioni katika kusaidia kampeni hii ya
“Dawati ni Elimu” ili kupunguza na kuondoa kabisa tatizo la madawati
mashuleni
Wasanii wataopata nafasi ya kuonyesha kazi
zao za sanaa ya kuchora ni Robin Mtila, Aggrey Mwasha, Salum Kambi,
Cathbert Mkocha, Haji Chilonga, Tobias Miza, James Haule na Victor
Malulu.
0 comments:
Post a Comment