Afisa
Uhusiano wa Chuo cha Serikali za mitaa Bw.Sebera Fulgence akiongea na
waandishi wa habari(hawapo pichani) kuhusu mafanikio ya chuo hicho ikiwa
ni pamoja na kufanya mafunzo kwa Watumishi wa Serikali wapatao
4,913,wakati wa Mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO)
Jijini Dar es Salaam.Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano toka
Ofisi ya Waziri Mkuu,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Bi.
Rebecca Kwandu.(Picha na Eliphace Marwa-Maelezo).
Chuo
cha Serikali za Mitaa, Hombolo Dodoma kimetoa mafunzo kwa Watumishi
zaidi ya 4,913 toka 2009 mpaka kufikia Septemba 2013 kwa Watendaji na
Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, pia idadi ya walionufaika na
mafunzo haya ni kama ifuatavyo:
a) Wenyeviti wa Vijiji/Mitaa/Vitongoji 3,733
b) Maafisa Watendaji wa Vijiji/Mitaa 282
c) Maafisa Watendaji wa Kata 388
d) Madiwani 327
e) Wawezesha Mafunzo 52
f) Maafisa Elimu Sekondari 48
g) Wahudumu wa Ofisi 20
h) Wajumbe wa ALAT 18
i) Wakuu wa Idara 45
Pia
Chuo kwa kushirikiana na Taasisi ya Forum syd ya Mwanza, tangu mwaka
2011 kimeweza kutoa mafunzo ya muda mfupi ya Uwajibikaji wa Kijamii
(Social Accountability) kwa watumishi na viongozi wa ngazi zote za
Serikali za Mitaa pamoja na Asasi za Kiraia, wakiwemo Wenyeviti na
Maafisa Watendaji wa vijiji, Vitongoji, Mitaa na Kata, Waheshimiwa
Madiwani, Wakurugenzi na wakuu wa Idara na Vitengo, Wakuu wa Magereza,
Mabenki, TAKUKURU, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya na Maafisa
Tarafawa Halmashauri za Wilaya za Ukerewe, Magu na Karagwe .
Mwaka
2009 Chuo cha Serikali za Mitaa kiliteuliwa na Serikali kuwa Taasisi
Kiongozi ya Mafunzo (Lead Training Institution) katika kuratibu na
kusimamia ubora wa mafunzo yatolewayo kwa watumishi katika Mamlaka za
Serikali za Mitaa. Kazi hiyo kwa sasa inafanywa na Chuo kwa kushirikiana
na wafadhili. Kwa sasa wafadhili ambao ni JICA na GIZ. Aidha, Mwaka
2012 Chuo cha Serikali za Mitaa kiliteuliwa na Serikali kutoa mafunzo
elekezi (Induction Courses) kwa watumishi wote wapya wanaoajiriwa na
Mamlaka za Serikali za Mitaa. Jukumu hilo ni kwa mujibu wa Waraka namba 5
wa Utumishi wa Umma wa mwaka 2012.
Aidha,
Chuo kwa kushirikiana na OWM TAMISEMI, kiliendesha mafunzo ya Semina
elekezi ya Makatibu Tawala wapya wa Mikoa sita (6) ya Tanzania Bara
mwezi Mei 2011 na Makatibu Tawala wa Mikoa yote tarehe 4/7/2011 hadi
tarehe 13/7/2011.
Mafunzo haya yamekuwa yakifanyika hapa Chuoni na Mengine kwenye Mikoa husika ya Watumishi.
Chuo
cha Serikali za Mitaa ni miongoni mwa Taasisi zilizoko chini ya
OWM-TAMISEMI na kilianzishwa kwa mujibu wa Sheria Na. 26 ya mwaka 1994
(Sura ya 396 toleo lililorejewa mwaka 2002). Lengo kuu la kuanzishwa
kwake ni kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kutoa huduma
bora zitakazowajengea wananchi uwezo wa kuimarisha utawala bora,
kuondokana na umaskini na kuboresha maisha yao.
Madhumuni
mahususi ya Chuo ni kuchangia katika uwezeshaji wa mchakato mzima wa
kupeleka madaraka kwa wananchi, kujenga na kukuza utawala bora, kukuza
uchumi na kuondoa umaskini katika ngazi mbalimbali za Serikali za
Mitaa hapa nchini.
Chuo
hiki kimesajiliwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (National
Council for Technical Education) ambalo ndilo lenye mamlaka ya kusimamia
ubora, viwango na uendeshaji wa Vyuo vya Elimu ya juu na Ufundi visivyo
Vyuo Vikuu hapa nchini.
Majukumu ya Chuo yamegawanyika katika sehemu kuu tatu:-
i)
Kutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu juu ya taaluma, ujuzi, stadi na
mbinu za uendeshaji wa Serikali za Mitaa kwa Viongozi na Watumishi walio
katika ngazi mbalimbali za Serikali za Mitaa;
ii)
Kutoa mafunzo juu ya mabadiliko yanayohusu Serikali za Mitaa kulingana
na Mpango wa Uboreshaji wa Mfumo wa Serikali za Mitaa na;
iii)
Kufanya utafiti na kutoa ushauri kwa Serikali Kuu, Mamlaka za Serikali
za Mitaa, Mashirika na watu binafsi juu ya masuala yote yanayohusu
Serikali za Mitaa.
Chuo
katika kutimiza lengo lake la kuwa ndicho Chuo Kiongozi cha Mafunzo
katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, kinaendelea na jitihada zake za
kuhakikisha kuwa zinawafikia watumishi wote wa Mamlaka za Serikali za
Mitaa kupia mafunzo ya kuwajengea uwezo wao kiutendaji na kitaaluma.
Pamoja na jitihada zinazofanywa na Chuo katika utoaji wa mafunzo ya muda
mfupi na yale ya Muda mrefu, bado kinakabiliwa na changamoto moja kubwa
kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa ni uhaba wa fedha za mafunzo
kinachopelekea kutofanyika kwa mafunzo mengi kwa Watumishi ndani ya
Mamlaka za Serikali za Mitaa ambao ndio Wadau Muhimu.
0 comments:
Post a Comment