Ufoo ambaye mara kadhaa katika mazungumzo na gazeti hili alionekana
kukunja uso akiashiria kupata maumivu, alionyesha eneo la chini ya bega
katika mkono wake wa kulia lililofungwa na bandeji ambalo alisema ndipo
alipopigwa risasi ya kwanza wakati akigeuka na kujaribu kuepuka mauti
muda mfupi baada ya Antheri kumfyatulia risasi zilizomkuta mama yake
mzazi.
Akijaribu kuvuta kumbukumbu ya tukio lilivyoanza, Ufoo alisema mzazi
mwenzake huyo alifika nyumbani kwake akitokea Sudan alikokuwa akifanya
kazi usiku huo huo wa tukio na akamtaka kwenda kwa mama yake (Ufoo) eneo
la Kibamba, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Kabla ya kufika Kibamba na kwa sababu ambazo Ufoo hakuzieleza,
alimkariri mzazi mwenzake huyo akisema alikuwa amefikia uamuzi wa kujiua
yeye na mtoto wao.
“Hata sijui ni nini kilitokea. Wakati tukitoka nyumbani Antheri alianza
kwa kuniambia kwamba alikuwa amepanga kujiua yeye na mtoto wetu,”
alisema Ufoo kabla ya kukaa kimya kwa sekunde kadhaa na kuendelea na
simulizi yake ya kusikitisha.
Akiwa na sura ya ujasiri, Ufoo anasema pamoja na kumwambia maneno hayo
bado Mushi alimsisitiza kwamba waende kwa mama yake (Ufoo) baadae warudi
kumchukua mtoto wao japo Ufoo hakusema walitaka kwenda wapi baada ya
hapo.
Alisema walipofika nyumbani kwa mama yake walikwenda moja kwa moja
sebuleni na wakiwa wamekaa kwenye makochi baada ya salamu za hapa na
pale ghafla Mushi akasimama akamwambia mama yake Ufoo kwamba; “Mama
nimeishafanya maamuzi”
Kwa mujibu wa maelezo ya Ufoo, baada ya Mushi kutamka maneno hayo ghafla
akaingiza mkono nyuma ya suruali alikokuwa ameweka bastola yake na
kisha akaichomoa.
Katika maelezo yake Ufoo alisema baada ya kuichomoa bastola hiyo mama
yake naye alisimama na kwenda kujaribu kumpokonya, kitendo hicho
kilimfanya amiminiwe risasi mfululizo.
Alisema kuona hivyo aliamua kukimbia kuelekea jikoni ambapo Mushi
alimuona na kuanza kumiminia risasi ambayo moja ilimpata eneo la mkono
wa kulia ambayo ilitokezea mbele na kuchana titi la kulia.
Kwa mujibu wa Ufoo jeraha hilo halikumfanya akate tamaa ya kunusuru
maisha yake kwani alijaribu kukimbia ingawa Antheri alifyatua risasi
nyingine kadhaa ambazo zilimpata juu kidogo ya mgongo na kutokea tumboni
ambazo zilisababisha aanguke chini
Akiendelea kusimulia, anasema ingawa alikuwa akivuja damu nyingi, na
huku akijiburuza ardhini, Ufoo alisema wakati akitambaa aligeuka nyuma
na akamuona Antheri akijielekeza bastola eneo la kidevu na alipofyatua
risasi alianguka chini.
“Nikiwa chini nilimuona Antheri akijipiga risasi kidevuni na akaanguka
chini, sikujua kilichofuata baada ya hapo kwani niliendelea kujiburuza
ili kuokoa maisha yangu,” alisema Ufoo
ALIVYOJIOKOA
“Nyumbani kwetu, pale Kibamba si mbali sana na barabarani, wakati
nikikaribia kufika barabarani wakati huo nikitokwa na damu nyingi huku
nikihisi tumbo langu limejaa sana nilikutana na dada mmoja ambaye
nilimuomba khanga ili nijifunge kuzuia damu zisitoke kwa wingi”.
Anasema dada yule alimpa khanga akajifunga na aliposogea barabarani alikutana na gari lililokuwa likiendeshwa na mwanamke mmoja.
“Nilipoona kuna gari linapita nikainuka kuomba msaada. Liliposimama
nilimuona mwanamke akiendesha nikamweleza kwamba nilikuwa nimepigwa
risasi na nilikuwa nikiomba msaada wake anikimbize hadi katika hospitali
ya Tumbi na kwamba akifika pale tu aniache mlangoni.
“Si rahisi kuamini, yule mama alikataa kunisaidia akisema alikuwa
akiwahi sehemu kumchukua mzazi. Sina la kusema niliamua kumsamehe tu
yule mama ingawa niliumia sana,” alisema Ufoo.
Alisema muda mfupi tu baadaye alitokea kijana aliyekuwa na pikipiki,
maarufu kwa jina la bodaboda ambaye alimuomba msaada wa kumkimbiza
hospitali ya Tumbi na akakubali.
“Yule kijana aliniuliza iwapo nilikuwa ninao uwezo wa kujishikilia
vizuri na niliposema nitaweza akanisaidia kupanda katika bodaboda.
“Wakati huo nilikuwa naona kama tumbo linazidi kujaa. Nikiwa kwenye
pikipiki kuna wakati nilikuwa nikihisi kwamba naweza nikaishiwa nguvu na
kuanguka katika barabara na kisha kupitiwa na gari na kupoteza maisha.
Lakini nilipata ujasiri na kujishikilia,” alieleza kwa sauti ya chini.
Alisema anakumbuka wakati walipofika eneo la Kibaha ilipo mizani ya
kupima uzito wa magari makubwa walikuta barabara ikiwa imejaa magari na
yeye alimuomba dereva huyo wa bodaboda kupita hata nje ya barabara eneo
la nyasi ili kumwahisha hospitalini jambo ambalo kijana yule
alilifanya.
“Nilipofika eneo la mapokezi pale Tumbi nilimueleza muuguzi niliyemkuta
kwamba nilikuwa nimejeruhiwa kwa risasi na nikamuomba asaidie kuokoa
maisha yangu. Yule nesi alisita akitaka kwanza kupata kibali cha polisi
(PF3) lakini nikaumuomba apigiwe simu, Kaimu Mganga Mkuu wa Tumbi, Dk.
Dattan ambaye tunafahamiana”
“Baada ya muda mfupi Dk. Dattan alifika na nikamweleza yaliyonipata na
mara moja nikaanza kuhudumiwa kwa kuniwekea dripu, na nikamsikia
akiwaeleza wauguzi kwamba isingekuwa busara kwa hali niliyonayo kama
wangeanza kuchukua picha za X-ray kwani hatua hizo zingeweza kusababisha
kupoteza maisha,” alieleza akikumbuka yaliyojiri hapo Tumbi.
Kwa mujibu wa Ufoo, akiwa bado ana fahamu alimsikia daktari aliyekuwa
akimhudumia akiomba msaada wa gari la kubeba wagonjwa ili limchukue na
kumkimbiza katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wito ambao ulijibiwa
kwa maelezo kwamba lilikuwa halina mafuta.
Majibu hayo kwa mujibu wa Ufoo, yalisababisha daktari huyo aombe
kuletewa gari la wagonjwa la wagonjwa maarufu (VIP) ambalo lililitwa na
muda mfupi baadaye akapakizwa tayari kwa safari ya kukimbizwa
Muhimbili.
Alisema wakati akikimbizwa Muhimbili anakumbuka namna alivyokuwa
akipatwa na maumivu makali wakati wote gari ile ya wagonjwa ilipokuwa
ikipanda matuta ya barabarani na kuna nyakati alikuwa akihisi kupoteza
pumzi na kuishiwa nguvu.
MTANZANIA MTANDAONI
0 comments:
Post a Comment