Dar es Salaam. Jitihada za mwanamuziki maarufu
wa muziki wa dansi nchini, Nguza Viking ‘Babu Seya’ na mwanaye, Johnson
Nguza ‘Papii Kocha’ kujinasua katika kifungo cha maisha jela zimekwama
baada ya Mahakama ya Rufani Tanzania kutupilia mbali maombi yao ya
marejeo ya hukumu ya rufaa yao.
Hii ni mara ya tatu kwa wasanii hao kugonga
mwamba, baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na Mahakama ya
Rufani kutupilia mbali rufaa zao za kupinga hukumu ya Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu iliyowatia hatiani na kuwahukumu kifungo hicho.
Wafungwa hao, kupitia kwa Wakili Mabere Marando
walikuwa wakiiomba Mahakama ya Rufani ifanye marejeo ya hukumu yake ya
Februari 11, 2010 iliyothibitisha adhabu hiyo waliyohukumiwa na mahakama
ya chini na badala yake iwaachie huru.
Lakini jana, Mahakama ya Rufani katika uamuzi wake
uliotolewa na jopo la Majaji, Nathalie Kimaro, Salum Massati na Mbarouk
Salim Mbarouk, lilitupilia mbali maombi hayo na kusisitiza kuwa
waendelee kutumikia adhabu hiyo.
Uamuzi huo uliibua machungu si tu kwa wafungwa hao
ambao walitoa kauli za kukata tamaa, bali pia kwa wakili wao mwingine,
Gabriel Mnyele ambaye alisema kuwa sasa hakuna namna nyingine ya
kuwachomoa katika adhabu hiyo isipokuwa kwa miujiza tu.
Wakati wafungwa hao na wakili wao wakitoa kauli
hizo za kukata tamaa, ndugu, jamaa na marafiki zao walibaki
wakibubujikwa na machozi tu baada ya uamuzi huo kusomwa, hali
iliyoendelea hata wakati wafungwa hao walipokuwa wakipandishwa katika
gari la Magereza kurudishwa gerezani.
Katika uamuzi wake uliosomwa na Kaimu Msajili wa
wake, Zahra Maruma, Mahakama ya Rufani ilitupilia mbali maombi hayo
ikisema kuwa waomba marejeo hao hawakuwa na hoja za msingi.
Ilisema hoja zilizotolewa katika maombi hayo ya
marejeo si tu kwamba hazikidhi kuifanya irejee hukumu hiyo, bali pia
hoja hizo zilishatolewa wakati wa usikilizwaji wa rufaa na kutolewa
uamuzi.
Pia Mahakama hiyo ilieleza kuwa waomba marejeo hao
hawakuweza kubainisha makosa waliyodai kuwa yalijitokeza katika hukumu
iliyowatia hatiani na kwamba hata kama yangekuwapo, hawakuweza kueleza
ni jinsi gani yalisababisha haki kutokutendeka.
“Kuhusu upande wa mashtaka kushindwa kuwaita
mahakamani mashahidi wanaoonekana kuwa muhimu kuunga mkono ushahidi wa
watoto, tunasema kuwa hoja hiyo haina msingi,” ilisema Mahakama katika
uamuzi wake na kuongeza:
“Suala la shahidi gani aitwe mahakamani
kuthibitisha kesi ya upande wa mashtaka liko mikononi mwa upande wa
mashtaka. Zaidi ya yote, idadi ya mashahidi si hoja ya msingi bali
kuaminika kwao.”
Akizungumza baada ya uamuzi huo, Wakili Mnyele
alisema: “Huu ndiyo mwisho wa mchakato. Kulingana na hukumu
ilivyotolewa, kunahitajika mahakama ya juu zaidi ya hii. Kungekuwapo na
‘Supreme Court’ (Mahakama ya Juu) ambayo ingeweza kusikiliza na kufikia
uamuzi wa haki.”
CHANZO:MWANANCHI
CHANZO:MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment