Home » » Bandari ya Dar kupanuliwa

Bandari ya Dar kupanuliwa

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia maendeleo ya kimataifa, Justine Greening (kulia) akiongozana na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Charles Tizeba (kulia kwake), wakati alipotembelea Bandari ya Dar es Salaam jana. Tanzania na Uingereza zimezindua ushirikiano wa kibiashara baina yao jijini Dar es Salaam juzi.(PICHA:OMAR FUNGO)
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), inatarajia kutekeleza mradi wa uendelezaji na upanuzi wa gati namba moja hadi saba, utakaosaidia bandari hiyo kupokea meli kubwa huku gharama za mradi huo zikikadiriwa kuwa Dola za Marekani bilioni 1 (Sh. Trilioni 1.6).
Kaimu Mkurugenzi wa TPA, Madeni Kipande , aliyasema hayo jana wakati wa ziara ya Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza, Justine Greenings, katika TPA kuangalia miradi ya maendeleo na shughuli mbalimbali zinazofanywa katika bandari hiyo.

Alisema baada ya kumalizika kwa mradi huo, Bandari ya Dar es Salaam itakuwa na uwezo wa kupokea meli kubwa kutoka nje, lakini hakuweza kuweka bayana idadi ya meli zitakazoweza kufika bandarini hapo.

Alisema mbali na kuwa na uwezo wa kupokea meli kubwa, pia kutapunguza msongamano wa meli katika bandari hiyo kutokana na kupanuliwa kwa gati hizo.
Kipande pia  hakuweka bayana siku ya kuanza kwa upanuzi wa miradi hiyo wala muda utakaochukua kumalizika.

“Siwezi kujua lini upanuzi utaanza wala lini utamalizika kwa sababu tupo katika hatua za awali za kuandaa mazingira na utafiti,” alisema Kipande.

Aliongeza kuwa uwezo wa kupokea mizigo utaongezeka kutokana na uwezo wa bandari hiyo kupokea meli kubwa za mizigo.
Naye Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba, alisema mbali na upanuzi wa gati hizo, pia TPA inatarajia kuongeza gati zingine namba 13 na 14 ili kuongeza ufanisi zaidi wa kiutendaji katika bandari hiyo.

Aliongeza kuwa  kampuni ya Trademark East Afrika ya Uingereza ndiyo inayofanya kazi ya kuandika andiko la mradi wa upanuzi wa gati.

Akiwa bandarini hapo, Greenings alitembelea sehemu mbalimbali za bandari ya Dar es Salaam na kujionea shughuli zinazofanyika ikiwamo kitengo cha upakuaji mafuta cha Kurasini Oil Jet.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa