Home » » Mwili wa Dk. Mvungi wawasili

Mwili wa Dk. Mvungi wawasili

  Vilio,simanzi vyatawala Uwanja wa Ndege Dar
Waombolezaji wakiwa wamejipanga kandokando ya jeneza lenye mwili wa Dk. Sengondo Mvungi, muda mfupi baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam jana, ukitokea Afrika Kusini.
 
Vilio na simanzi jana vilitawala katika  Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam  baada ya mwili  wa aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, DK. Sengondo Mvungi (61), kuwasili ukitokea nchini Afrika Kusini.
Mamia ya wakazi wakiwamo ndugu, jamaa, viongozi wa serikali na vyama vya siasa, walifika katika uwanja huo kuupokea mwili huo.

Ndege iliyobeba mwili wa Dk. Mvungi iliwasili majira ya saa 1:29 jioni ambapo ulipokelewa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na baadaye kuingizwa kwenye gari la wagonjwa kuelekea katika Hospitali ya kijeshi la Lugalo.

Akizungumza kabla mwili huo kuwasili, Mkuu wa shule ya sheria, Profesa Paramagamba Kabudi, alisema Dk. Mvungi alikuwa kati ya wanafunzi aliosoma naye na kufanya naye kazi ya uandishi wa habari katika gazeti la Uhuru na Mzalendo

Alisema wakati wa uhai wake, Dk. Mvungi alikuwa mtu anayetekeleza jambo analoliamini kwa vitendo. Kabudi alisema Dk. Mvungi ameondoka lakini wanajua kile alichokuwa amekisimamia alikifanya kwa niaba ya Watanzania.

Alisema Dk. Mvungi aliamini tiba mpya ya mageuzi katika kuimarisha demokrasia, haki za binadamu , uongozi bora unaozingatia maadili na kutanguliza maslahi ya Watanzania na hicho ndiyo kielelezo tosha katika chuo chake cha Bagamoyo alichokuwa akifundisha somo la utawala na uongozi bora.

 “Maadam tunayaamini haya tutayasimamia na kuyatekeleza kwa vitendo, Dk alikuwa akifanya yote bila kuangalia kama atalipwaje, bila kujali msharahara alikuwa akitekeleza kwa maslahi ya Watanzania,” alisema.

Dk. Mvungi alitoa mchango mkubwa katika mchakato wa kupata katiba mpya na kuondoka kwake kumeacha pengo kubwa kwa kuwa waliosomea katiba na sheria ni wachache. Mtoto wa marehemu, Dk. Natujwa Mvungi, alisema kuwa wakati wa uhai wake, baba yao alikuwa akiwahamasisha kupenda elimu, na suala la katiba alikuwa akizungumza nao kila alipokuwa nao.

Alisema kuwa mchakato wa katiba ulipoanza baba yake aliwaambia lengo la kuingia katika mchakato huo ni kupata katiba ambayo itawasaidia Watanzania hususani wenye hali ya chini.

Viongozi waliojitokeza kuupokea mwili huo ni pamoja na wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, Jaji Mstaafu Othuman Ramadhani, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angella Kairuki na Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu Hellen -Kijo Bisimba.

Wengine ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Said Meck Sadick, Naibu Katibu Mkuu CCM, Mwigulu Nchemba na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Nchi huru za Afrika (OAU), Dk. Salim Ahmed Salim.

Leo mwili wa marehemu unatarajiwa kuagwa katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam na baadaye kusafirishwa kwenda kijijini kwao Kisangara Juu wilaya ya Mwanga ambako utazikwa Jumatatu.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa