Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » Chadema: Hatukuzuiwa kumjadili Zitto Kabwe

Chadema: Hatukuzuiwa kumjadili Zitto Kabwe

“Suala la hatima ya uanachama wake ndiyo halitajadiliwa, lakini jambo jingine lolote likijitokeza, Kamati Kuu ya chama ina haki ya kumjadili mtu yeyote yule.” John Mnyika   

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kuwa Mahakama Kuu haikuzuia kikao cha Kamati Kuu yake kujadili mambo mengine yanayomhusu aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wake, Zitto Kabwe bali uanachama wake pekee.
Juzi mahakama hiyo iliweka zuio, ikitaka chama hicho kupitia kikao hicho kutojadili ajenda zozote zinazomhusu Zitto, ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini.
Uamuzi huo ulitolewa na Jaji John Utamwa, baada ya kupokea maombi ya Zitto kupitia wakili wake, Albert Msando kukata rufaa yake iliyowasilishwa Baraza Kuu la Chadema kusikilizwa kwanza, kabla ya kufanyika uamuzi mwingine.
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi kabla ya kuanza kwa kikao hicho cha Kamati Kuu jijini Dar es Salaam jana,  Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, John Mnyika alisema: “Kuna watu walipotosha amri iliyotolewa na mahakama… Ilitoa zuio la kujadili uanachama wa Zitto, lakini haikuzuia mambo mengine kujadiliwa.”
Mnyika alifafanua: “Baada ya wao kufungua kesi ya msingi kusema Kamati Kuu isijadili masuala ya uanachama wake mpaka pale rufaa yake ambayo bado hajaikata itakapojadiliwa, ameeleza tu kusudio la kutaka kuikata itakapojadiliwa na Baraza Kuu.”
Aliongeza kuwa jambo hilo liliwekewa pingamizi la awali na mawakili wa chama hicho juzi na kwamba jana, walikuwa wakiandaa majibu ya maswali yaliyofikishwa mahakamani na mpeleka madai (Zitto).
“Suala la hatima ya uanachama wake ndiyo halitajadiliwa, lakini jambo jingine lolote likijitokeza, Kamati Kuu ya chama ina haki ya kumjadili mtu yeyote yule,” aliongeza Mnyika.
Alisema kuwa mkutano huo utatangaza majina ya watu waliopelekwa kwa Rais Jakaya Kikwete kwa ajili ya kuteuliwa kuwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.
Aliongeza kuwa Bunge la Katiba linapaswa kuchukua maoni ya wananchi, huku akiwalaumu baadhi ya viongozi wa CCM kwa kuanza kupinga pendekezo la Serikali tatu.
“Tayari CCM imekwishatoa msimamo ambao baadhi yao wanauendeleza wa Serikali mbili, wakati wananchi wameshasema Serikali tatu,” alisema.
Mnyika alibainisha kuwa mkutano huo pia utajadili namna ambavyo Tume ya Taifa ya Uchaguzi(Nec), ambayo inalalamikiwa na chama hicho kupewa kazi ya kusimamia uchaguzi na kwamba chama hicho kinawasiwasi kuwa mchakato wa kura ya maoni utakuwa shakani.
“Bungeni tulitaka Daftari la Kudumu la Mpigakura lingeboreshwa, lakini baadaye tulipomaliza Bunge, tume ikasema halitaboreshwa,” alisema Mnyika.
Hali ilivyokuwa eneo la mkutano
Kabla ya kuanza kwa mkutano huo, wajumbe walionekana wakiwa na furaha huku wakizungumza katika makundi makundi nje ya ukumbi.
Wajumbe hao walipoingia ndani waliwataka waandishi wa habari kuingia kupiga picha, kisha kutoka nje kwa kuwa hawakuruhusiwa kusikiliza.
Saa 7:27 mchana, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema, Samson Mwigamba na aliyekuwa Mjumbe wa Halmashauri kuu, Dk Kitila Mkumbo waliwasili katika eneo la mkutano, huku wakipokelewa na Mwenyekiti wa Bazara la Vijana Chadema (Bavicha), John Heche na Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa chama hicho, Willfred Lwakatare na kuwaelekeza sehemu ya kukaa wakati wakisubiri kuitwa ndani kwenda kujitetea.
Zitto, Mwigamba na Dk Kitila walivuliwa nyadhifa zao zote walizokuwa nazo ndani ya chama hicho baada ya kubainika kuwa walikuwa wakiandaa waraka wa siri kwa ajili ya kukihujumu chama hicho, ikiwamo kumng’oa mwenyekiti wake kinyume na kanuni,  sheria na Katiba ya Chadema.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa