Home » » Dar kinara ajali za barabarani kwa 54%

Dar kinara ajali za barabarani kwa 54%


Jiji la Dar es Salaam linaongoza kwa ajali za barabarani kwa asilimia 54, likifuatiwa na mikoa wa Kilimanjaro na Pwani.
Kutokana na hali hiyo, Kikosi cha Usalama Barabarani kimetangaza operesheni kabambe ya kukamata madereva wanaokwenda kinyume na sheria za barabarani na kuchukua hatua za kisheria dhidi yao.

Kamanda wa kikosi hicho, Mohamed Mpinga, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari, juu ya tathmini ya matukio ya ajali kwa mwaka 2013 ukilinganisha na mwaka 2012.

Alisema Jiji la Dar es Salaam pekee liliongoza kwa kuwa na ajali 12,983 kwa mikoa ya kipolisi ya Kinondoni na asilimia zake kwenye mabanio ni ajali 6,589 (28), Ilala 3,464 (14) na Temeke 2,930 (12).

Alisema mkoa wa Kilimanjaro kulikuwa na ajali 1,599 sawa na asilimia saba na mkoa wa Pwani ajali 1,460 sawa na asilimia sita na kuitaja mikoa iliyopunguza ajali na aasilimia zake kwenye mabano kuwa ni Arusha (53), Mwanza (37.7), Mbeya (20.6) na Morogoro (12).

“Mikoa hii ilifanikiwa kupunguza ajali kutokana na kukamata madereva wazembe na wanaovunja sheria za barabarani…visababishi vikubwa vya ajali ni ulevi, mwendo kasi na kutofuta sheria za barabarani,” alisema.

Kadhalika, Mpinga alisema wamewasiliana na wamiliki wa magari ili kuanzisha mfumo wa tiketi za kielektroniki ili kuondoa usumbufu wa abiria kusafiri kipindi cha mwisho wa mwaka.

Alisema mwaka 2012 kulikuwa na ajali 23,578 mwaka 2013 23,842 kukiwa na ongezeko la ajali 264 sawa na asilimia 1.1.

Mpinga aliongeza kuwa ajali zilizosababisha vifo mwaka 2012 ni 3,328 na mwaka 2013 3,427 ikiwa ni ongezeko la ajali 99 sawa na asilimia 3.0, vifo vilivyotokana na ajali hizo mwaka 2012 ni 3,969 na mwaka 2013 ni 4,002 ikiwa ni ongezeko la vifo 33 sawa na asilimia 0.8.

Alisema majeruhi mwaka 2012 walikuwa 20,111, mwaka 2013 ni 20,689 kukiwa na ongezeko la 578 sawa na asilimia 2.9.

Alisema makundi yaliyoathirika na ajali hizo kwa mwaka 2013 ni waenda kwa miguu vifo 1,247 na majeruhi 836, abiria 1,105 walifariki na 8,770 walijeruhiwa, waendesha pikipiki walifariki 870 na 5,237 walijeruhiwa, wapanda baiskeli 447 walifariki na 1,162 walijeruhiwa, madereva 297 walifariki na 156 walijeruhiwa na wasukuma mikokoteni 36 walifariki na 156 walijeruhiwa.

Alisema mwaka 2012 kulikuwa na ajali za pikipiki 5,763 na mwaka 2013 ajali 6,831, vifo mwaka 2012 vilikuwa 930 mwaka 2012 1,098 na majeruhi mwaka 2012 walikuwa 5,532 huku mwaka 2013 wakiwa 6,578. 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa