WIZARA
ya Fedha imesema deni la taifa limepanda hadi kufikia dola za Marekani
bilioni 17.10 sawa na sh. trilioni 27. 04 ilipofika Desemba, mwaka jana.
Hayo yamebainishwa Dar es Salaam jana na Waziri wa Fedha, Saada
Mkuya, wakati akizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni mara ya kwanza
tangu ateuliwe kuwa waziri wa wizara hiyo.
Alisema kati ya deni
hilo, deni la nje ni dola za Marekani bilioni 12.79 sawa na sh.trilioni
20.23. Alitaja sababu za kuongezeka kwa deni hilo ni mikopo
iliyopokelewa na Serikali na ambayo muda wake wakulipa haujafika kutoka
vyanzo vya masharti nafuu na ya kibiashara na malimbikizo ya riba ya
deni la nje.
Alisema Septemba mwaka jana Serikali ilifanya tathmini
ya kupima na kuangalia uhimilivu wa deni la Taifa kwa kutumia vigezo
vilivyowekwa na kutambuliwa na Taasisi za kimataifa na matokeo ya
tathmini hiyo yanaonesha kwamba deni la taifa ni himilivu.
Waziri Mkuya alisema hiyo ni kwa sababu viashiria vyote vilivyowekwa kimataifa, kwani bado viko chini ya ukomo unaotakiwa.
"Hatua
tulizochukua kuhakikisha uhimilivu wa deni la taifa ni kuhakikisha
kwamba mikopo inayopewa kipaumbele ni ile yenye masharti nafuu na mikopo
hiyo inatumika kwenye maeneo ambayo yana vichocheo vya ukuaji wa
miundombinu ikiwemo miundombinu ya barabara, mawasiliano, bomba la gesi
na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Zanzibar," alisema Mkuya.
Aidha
aliongeza kuwa Serikali inatoa kipaumbele kwa miradi ya ubia kati ya
Serikali na sekta binafsi ili kuiwezesha sekta binafsi kuchangia
maendeleo ya uchumi wa nchi na kuipunguzia Serikali mzigo wa deni.
Akiongelea
kuhusiana na matumizi ya mashine za kielektroniki (EFD), alisema kuwa
hilo ni suala muhimu ambalo wanaendelea kulitolea ufafanuzi na
kulisimamia vyema kwa madhumuni ya kukusanya kodi kwa ufanisi zaidi ili
kuongeza pato la taifa na kupunguza ukwepaji kodi.
Alisema kuwa
mamlaka ya mapato (TRA) wataendelea kutoa elimu ya matumizi ya mashine
hizo kwa wafanyabiashara pia makubaliano kati ya serikali na viongozi wa
wafanyabiashara kuwa muda wa kuanza kutumia mashine usogezwe hadi leo
ili kuwapatia wananchi muda wa kutosha kujiandaa na utekelezaji wa
matumizi ya mashine.
Aidha alitoa wito kwa wadau kutoa ushirikiano
wa dhati katika utekelezaji wa azma hii ya kuboresha mapato ya Serikali
na kutekeleza malengo mbalimbali ya kimaendeleo
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment