Home » » MAONI: Vijana wanaofeli wasitelekezwe mitaani

MAONI: Vijana wanaofeli wasitelekezwe mitaani

Idadi kubwa ya vijana wanamaliza shule na kufeli katika ngazi mbalimbali kama vile darasa la saba, kidato cha nne, cha tano na vyuo. Wanapofeli, wengi wao wanaishia mitaani ambako hakuna mfumo unaoeleweka wa kuwasaidia.

Moja ya matukio yaliyochukua nafasi katika vyombo vya habari nchini wiki hii ni kukamatwa kwa kundi la vijana wanaoendesha uhalifu katika maeneo ya Kiwalani na Yombo kwa Limboa, Dar es Salaam linalojulikana kwa jina la Mbwamwitu au watoto wa mbwa.
Taarifa za Polisi Mkoa Maalumu wa Ilala zinasema kuwa vijana 14 wanaotuhumiwa kufanya uhalifu huo wamekamatwa na baadhi yao wamekimbia nje ya Dar es Salaam ambako pia wapo waliokamatwa na wengine wanaendelea kusakwa.
Mbali ya vijana hao wanaojiita Mbwamwitu, kuna taarifa za kuwapo kwa makundi mengine ya kihalifu katika Jiji la Dar es Salaam hususan maeneo ya Tabata Kisiwani, Mabibo, Kigogo na Ilala Boma. Vijana hao wamekuwa wakiwavamia watu njiani au kuvunja nyumba wakitumia silaha za jadi na kujeruhi na kupora mali hivyo kusababisha wakazi wa maeneo hayo kuishi kwa wasiwasi.
Yumkini haya ni maeneo machache tu kati ya mengi ambayo yamekuwa na vijana wenye tabia hizo chafu na zisizostahili katika jamii. Tunalitaka Jeshi la Polisi kukaza uzi katika kupambana na aina hii ya uhalifu kwani ikiachwa iendelee, itakwamisha shughuli nyingi za kijamii na kimaendeleo katika maeneo husika na uhuru wa wananchi kuishi kwa amani katika nchi yao utakuwa umetoweka.
Hata hivyo, uhalifu huu wa vijana ni matokeo ya mambo mengi yakiwamo malezi na makuzi.
Kwa upande wa malezi, tunapenda kuwakumbusha wazazi kote nchini usemi wa wahenga kwamba mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Haya ni matokeo ya malezi ya watoto wetu katika jamii. Watoto hawa waliachwa bila ya uangalizi wa wazazi au walezi na hata jamii inayowazunguka na haya ndiyo matunda yake. Kukana wazazi wao na kujiita watoto wa mbwa ni ushahidi tosha wa malezi mabovu yasiyozingatia maadili.
Kama Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Marieta Minangi alinukuliwa na vyombo vya habari akisema, nasi tunasisitiza, kila familia ijitathmini inavyolea na kudhibiti nidhamu za watoto wake. Hilo ni jambo la msingi kabisa na kama lingekuwa limefanyika inavyostahili, tusingekuwa na aina hii ya uhalifu.
Kwa upande wa makuzi, hapa ndipo tunapoliona lile bomu la ajira likianza kulipuka taratibu. Idadi kubwa ya vijana wanamaliza shule na kufeli katika ngazi mbalimbali kama vile darasa la saba, kidato cha nne, cha tano na vyuo. Wanapofeli, wengi wao wanaishia mitaani ambako hakuna mfumo unaoeleweka wa kuwasaidia.
Kwa mantiki hiyo, tunapenda kutumia fursa ya tukio hili kuikumbusha Serikali kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na tatizo hili.
Lazima kuwe na mikakati inayoeleweka kwa vijana wanaofeli darasa la saba. Watoto hawa wasiachwe tu kama kuku wa kienyeji mitaani, lazima kuwe na mpango mahsusi wa kuwaendeleza ama kielimu, kiufundi au kujitegemea, vivyohivyo, kwa wale wanaohitimu kidato cha nne, sita na hata vyuo.
Kuna msemo kwamba asubuhi yako inaanzia pale unapoamka, hata kama ni saa saba mchana. Hatuna haja ya kuishia kujilaumu kwamba tumechelewa, tuanze sasa kupanga mikakati ya kuwasaidia vijana wetu ili waondokane na aina hii ya maisha.
Tunaamini kwamba kwa kufanya hivyo, siyo tu kwamba kutatusaidia nasi kuishi kwa amani na utulivu, bali hawa ndio wanaotegemewa kuwasaidia wazee wao watakapostaafu au kushindwa kufanya kazi za uzalishaji.
Chanzo;Mwananchia

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa