Dar es Salaam. Uchaguzi Mkuu wa nane wa Chama
cha NCCR-Mageuzi, umemchagua tena James Mbatia kuwa mwenyekiti wa chama
hicho kwa kipindi kingine cha miaka mitano ijayo huku mizengwe ikitawala
katika uchaguzi huo.
Katika uchaguzi huo ulioanza juzi, idadi kubwa ya
wajumbe walikuwa na mkakati wa kumng’oa Katibu Mkuu, Samwel Ruhuza
aliyekuwa akitetea nafasi yake, Mosena Nyambabe na Rehema Sam waliokuwa
wakiitaka nafasi hiyo.
Wajumbe walikuwa na mpango huo kwa kuwa Nyambabe
yuko vizuri kiutendaji ikilinganisha Ruhuza. Jana kwa nyakati tofauti,
wajumbe walionekana katika makundi kujadili hali hiyo wakiongozwa na
Mwenyekiti wao, Mbatia.
Ukiacha hali hiyo, Mbatia alipata upinzani mkali
akichuana kwa mbali na aliyekuwa Kamishna wa chama hicho Mkoa wa Katavi,
Charles Makofila, ambaye ni mlemavu wa viungo.
Tangu kuanza kwa mkutano huo katika Ukumbi wa
Diomond Jubileee, hapakuwa na dalili za upinzani wa nafasi hiyo ya
uenyekiti na baadhi wa wajumbe wa mkutano walisikika wakisema, “Makofila
bwana sijui amekosa cha kufanya, ila ndo hivyo wacha amsindikize
mwenzake.”
Zoezi la upigaji kura lilianza saa 10 jioni hadi saa moja usiku chini ya Msimamizi wa Uchaguzi huo, Moses Machalli.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wajumbe 228 kati ya 289.
Machalli akitangaza matokeo hayo alisema, Mbatia ameshinda kwa kura 201 na Makofila ameambulia kura 26 na kura moja imeharibika.
“Ndugu Mbatia atakiongoza chama hiki kuanza hii
leo (jana) hadi Januari 2019 hivyo tumuunge mkono na uchaguzi usiwe
chanzo cha migogoro, tumemaliza salama na sasa tunaangalia mbele,”
alisema Machalli.
Mbatia akitoa shukrani zake alisema, “Nawashukuru
sana kwa kutumia demokrasia yenu kunichagua, nawaahidi kuwatumikia kwa
moyo wangu wote, uchaguzi umekwisha sasa tujenge chama chetu.”
Mwenyekiti huyo mpya, aliwataka wabunge wa chama
hicho kuacha kubweteka katika majimbo yao na sasa wazunguke nchi nzima
kukijenga chama.
“Machali, Kafulila kumbukeni kulipa fadhila za
chama, zungukeni nchi nzima acheni kujisahau bila NCCR tusingekuwa
katika Bunge tukufu, sasa kazi kwenu kwani tunaweza kama tutaamua,”
alisema Mbatia.
Akiongea baada ya kutangazwa matokeo, Makofila alisema uchaguzi
ulifanyika kwa uhuru na uwazi ila wajumbe wa mkutano huo waliomnyima
kura wamepoteza kura zao.
“Niliwaahidi ningeongeza posho za mkutano kutoka
elfu 30 hadi elfu 60 sasa kwa kuwa hawakunichagua wamepoteza kura zao,”
alisema Makofila.
Makofila alisema kushindwa kwake hakutamfanya
ajitoe ndani ya NCCR ila atatumia kipindi hiki kuongeza elimu ambayo
hadi kufika uchaguzi mwingine mapema mwaka 2019 atakuwa amejiimarisha
zaidi.
Katika uchaguzi huo ambao haukuwa na ushindani
katika nafasi nyingi kutokana na baadhi ya nafasi kujitokeza wagombea
wanaokidhi nafasi husika hivyo kuwachagua kwa kura za ndiyo au hapana.
Mfano ni nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Tanzania
Bara na Visiwani hapakuwa na washindani hivyo wajumbe walipiga kura za
ndiyo na hapana.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment