Home » » Nyalandu kuisuka upya Wizara ya Maliasili na Utalii

Nyalandu kuisuka upya Wizara ya Maliasili na Utalii

Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, akipongezwa na wafanyakazi wa wizara yake jana.
 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, ametangaza 'kuisuka' upya wizara yake ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa na kuwafanya watumishi wa chini kuwa na amani kazini.
Kadhalika, amesema tayari rasimu ya kuanzisha Wakala wa Wanyamapori (TWA) imeandaliwa na kwamba inatarajiwa kuwasilishwa kwenye Mkutano ujao wa Bunge.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Nyalandu ambaye aliambatana na Naibu wake, Mahmoud Mgimwa, alisema atafanya mabadiliko kwenye idara mbalimbali wizarani hapo na kwamba kila idara itapimwa kwa namna ya utendaji wake.

“Kila idara itapimwa kulingana na jinsi inavyosaidia watumishi wa chini. Kama unafanyakazi vizuri kazi yako itaonekana...tutafanya mabadiliko makubwa kwenye kila idara ili tumfanye kila mtu awe na amani kazini,” alisema.

Hata hivyo, alisema ana imani kubwa na watumishi wizarani hapo akieleza kuwa kwa kipindi alichokuwa Naibu Waziri, alijifunza mengi kwao na pia alishirikiana vizuri kwenye utekelezaji wa majukumu ya kila siku.

“Tufanye kazi kwa ushirikiano kwa maslahi ya taifa letu,” alisema.
Nyalandu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), alisema sekta ya utalii duniani inaongoza kwa kutoa ajira kwa watu wa ngazi mbalimbali na kwamba ndicho anachotaka kitokee wakati wa uongozi wake wizarani hapo.

Alisema hakuna sababu ya wakuu wa idara kutokuwa karibu na watumishi wa chini au 'kununiana' baina ya watumishi wizarani hapo kwa sababu kufanya hivyo hakutafanikisha malengo yaliyowekwa na wizara.

Aliwataka wakuu wa idara zote kuwa wakarimu kwa watumishi wa chini na kuwasaidia kutimiza majukumu yao. “Kuna watu wapo kwa ajili ya kukwamisha jitihada mbalimbali zinazofanywa, lakini tukishirikiana kwa pamoja, hilo halitapata nafasi na pia malengo yetu haya yote hayatawezekana kama watumishi wa chini hawana amani. Tunataka sekta ya utalii nchini iwe kinara wa kutoa ajira nchini,” alisema.

Alisema hatotumia utaratibu wa zamani wa kuita mtumishi mzembe na kumhoji hadharani badala yake atamwita ofisini kwake na kuzungumza naye kwa kina ili ajue tatizo linalosababisha uzembe ndipo atachukua hatua.

Naye Mgimwa alisema ushirikiano wa watumishi wa kada zote ndiyo utakaomaliza kashfa za kunyooshewa kidole kwa utendaji mbovu wizarani hapo.

UJANGILI
Kuhusu ujangili, Nyalandu alisema serikali inakusudia kuanzisha TWA itakayokuwa huru na yenye vifaa vya kukabiliana na tatizo hilo.

Alisema vita dhidi ya ujangili ni jukumu la kila mmoja, hasa watumishi wa wizara hiyo, hivyo akaeleza kuwa ushirikiano wa wafanyakazi wote unahitajika ili kufanikisha lengo hilo.

Nyalandu alisema ili kufanikisha vita hivyo, watumishi wanapaswa kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake amewataka kubuni mbinu mbalimbali zitakazosaidia kushinda vita dhidi ya ujangili.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa