Dar es Salaam: Uamuzi wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuruhusu malori makubwa ya mizigo yaendelee kuzidisha uzito wa mizigo, umetajwa kuwa ni hatari na utaisababishia Serikali hasara ya mamilioni ya fedha.
Hasara hiyo inatokana na uharibifu wa barabara za
lami ambao unachangiwa kwa kiasi kikubwa na malori yanayozidisha uzito
wa mizigo kinyume cha sheria na kanuni namba 7 (3) ya Sheria ya Usalama
Barabarani ya 2001.
Ujenzi wa barabara ni wa gharama kubwa na hata
ukarabati wake umekuwa ukitengewa mabilioni ya fedha za walipakodi
kutokana na uharibifu unaofanywa.
Mathalani katika bajeti yake ya 2013/14, Serikali
kupitia Wizara ya Ujenzi, imetenga kiasi cha Sh314.535 bilioni kwa ajili
ya mpango wa matengenezo ya barabara kuu na barabara za mikoa.
Kiasi hicho cha fedha ambacho ni zaidi ya robo ya
bajeti nzima ya wizara hiyo kwa mwaka, kinatosheleza kujenga barabara
mpya ya lami yenye urefu wa kilometa zipatazo 315, kwa makadirio ya
kilometa moja kugharimu Sh1 bilioni. Katika mwaka huu wa fedha, bajeti
nzima ya Wizara ya Ujenzi ni Sh1.226 trilioni.
Kauli ya Dk Magufuli
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, aliwahi
kunukuliwa akisema ataendelea kusimamia sheria ya barabara namba 30 ya
mwaka 1973, hadi anaingia kaburini kwa kuhakikisha hakuna magari ambayo
yanazidisha uzito na kuharibu barabara.
“Nchini Ujerumani, uzito wa magari yote ni tani
40, Uingereza tani 40, Ufaransa 40, Urusi 38 lakini Tanzania tani 56,
wakati mwingine tunakamata hadi tani 96,” alisema Dk Magufuli.
Hata hivyo, ujasiri wa Dk Magufuli ulizimwa na
amri ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, aliyetengua agizo la waziri huyo na
kuamua kuruhusu magari yenye uzito uliopitiliza kuendelea kutumia
barabara.
Wasemaji wa Serikali
Ofisa Habari wa Wizara ya Ujenzi, Martin Ntemo
alisema suala hilo wameliachia Ofisi ya Waziri Mkuu. “Hilo suala liko
Ofisi ya Waziri Mkuu, siwezi tena kulizungumzia,” alisema Ntemo kwa
kifupi.
Hata hivyo, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk
Florence Turuka alisema siyo sahihi kusema kwamba Waziri Mkuu amevunja
sheria kwani ilikuwa ni lazima serikali ichukue hatua jumuishi kwa
kuwashirikisha wadau husika.
“Siyo sahihi kusema kuwa tunataka kuvunja sheria, sisi tumepokea
mapendekezo na tutayaangalia kabla ya kutoa ripoti. Wewe vuta subira
tu,” alisema Dk Turuka.
Dk Turuka alisema kamati iliyoundwa na Serikali
ikiwajumuisha wadau mbalimbali wa barabara ilikamilisha kazi yake
Desemba mwaka jana na kwamba hivi sasa Serikali inatafakari mapendekezo
yaliyotolewa.
“Kamati ilishamaliza kazi tangu Desemba mwaka
jana… tulipokea mapendekezo kwa sababu ile ilikuwa kamati jumuishi,
kulikuwa na watu wa Tatoa, Taboa na Wizara ya Ujenzi na wataalamu, na
sasa tunayafanyia kazi,” alisema Dk Turuka.
Baadhi ya barabara ambazo zilikuwa katika hali
nzuri hivi sasa zimeharibika vibaya chanzo kikiwa ni uzito wa magari ya
mizigo. Miongoni mwa hizo ni Barabara Kuu ya Morogoro - Dodoma kati ya
Kijiji cha Magubike na Mji wa Gairo pamoja na Barabara ya Dar es Salaam
ya Morogoro eneo la kati ya Mlandizi na Chalinze.
Hali hii ndiyo iliyomsukuma Waziri wa Ujenzi, Dk
John Magufuli kufuta waraka unaoruhusu magari ya mizigo kuzidisha uzito
na badala yake kutaka sheria inayotaka malori yanayozidisha uzito uliopo
ndani ya asilimia tano kupunguza mzigo, kupanga mzigo upya au kulipia
uzito uliozidi mara nne ya tozo ya kawaida, ifuatwe.
Uamuzi wa Dk Magufuli ulipingwa na wamiliki wa
magari makubwa ya mizigo na kuungwa mkono na wamiliki wa mabasi ya
abiria, hivyo Waziri Mkuu Pinda aliingilia kati na kuamuru utaratibu wa
awali uendelee, ilhali suala hilo likiwa linatafutiwa ufumbuzi wa
kudumu.
Hata hivyo, Pinda alitangaza uamuzi wa kusitishwa
kwa utekelezaji wa amri ya Dk Magufuli katika mkutano ambao hata hivyo
waziri huyo wa sekta husika hakuhudhuria. Wakati huo kulikuwa na tishio
la kusitishwa kwa usafirishaji nchi nzima kama amri hiyo
isingetenguliwa.
Chanzo cha habari ndani ya Wakala wa Barabara
Tanzania (Tanroads) kinasema: “Tatizo kuna viongozi wengi wenye malori
na mabasi ndiyo wanaokwaza utekelezaji wa sheria hiyo.”
Kiliongeza: “Utakuta mtu ana magari hadi 300 na
yote yanazidisha uzito kwenye barabara kwa kisingizio cha kusamehewa
asilimia tano, unadhani barabara zetu zitaishia wapi? Ndiyo maana Dk
Magufuli kwa uchungu aliamua kuweka msimamo”.
Takwimu za vipimo
Takwimu za upimaji wa magari ambazo ziko kwenye
tovuti ya wakala huyo wa barabara nchini zinaonyesha kuwa licha ya
kuwepo nafuu katika sheria bado magari mengi yamekuwa yakizidisha uzito.
Mathalan 2011/12 magari 684,600 yalipimwa na kati
ya hayo, 167,310 sawa na asilimia 24.44 yalikutwa yakiwa yamezidisha
mizigo, huku mengine 8,856 sawa na asilimia 1.30 yalipitisha kiwango cha
asilimia tano.
Chanzo;mwananchi
Chanzo;mwananchi
0 comments:
Post a Comment