SHIRIKA
la Umeme Tanzania (TANESCO) limeendelea na operesheni yake ya kuwakatia
umeme watu wanaodaiwa kuhujumu shirika hilo, ambapo safari hii limekata
na kuondoa nyaya zote za umeme zinazopeleka nishati hiyo katika eneo
lote la Msimbazi bondeni.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es
Salaam jana Kaimu Meneja wa Tanesco Mkoa wa Ilala, Ahmed Mningwa,
alisema operesheni hiyo niendelevu na haitamuacha mtu yeyote ambaye
anatumia umeme isivyo halali.
Alisema kwa wananchi wote wa Jangwani
na sehemu zingine katika eneo hilo wafike katika ofisi za shirika hilo
wakiwa na nyaraka zao halali tangu walivyoanza taratibu zote za kupata
umeme na hadi kufikia hatua ya kupata umeme huo.
"Hii ni operesheni
endelevu na haitamwacha mtu yeyote, hakuna mita inayotumia umeme tofauti
na ilivyotengenezwa na zaidi ya hapo itakuwa imechezewa na wale wote
walioomba umeme kihalali basi wategemee kupata umeme muda mfupi ujao,
kwani kila kitu kimekamilika," alisema Mningwa.
Kwa upande wake
Mkaguzi Kiongozi wa Shirika hilo Mkoa wa Ilala, Christian Simon, alisema
utafiti uliofanywa na shirika hilo katika nyumba 30, nyumba 25
zinatumia umeme bila kulipia na nyumba tano hazina mita kabisa, lakini
zinatumia umeme.
Alisema operesheni ipo katika maeneo yote ambapo
katika baadhi ya maeneo wananchi wameshindwa kutoa ushirikiano na wakati
mwingine kukimbia na kuacha nyumba zao na kwamba kwa muda huu shirika
hilo linasaka kila uniti moja inayopotea.
Kwa upande wao baadhi ya
wakazi katika eneo hilo walisema kumekuwa na tabia ya watu
kujiunganishia umeme kiholela na ni vyema shirika hilo likawakamata watu
hao na kuwachukulia hatua za kisheria
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment