UTEUZI
wa wabunge wa Bunge la Katiba uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete, hivi
karibuni umezidi kupata upinzani ambapo Jukwaa la Katiba Tanzania
linahoji uteuzi wa kada wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru, kupitia kundi
la asasi za kiraia, wakati hajawahi kuwa mwanachama wa asasi yoyote.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mjumbe wa Kamati ya Uongozi
ya Jukwaa hilo, Hebroan Mwakagenda, alisema nafasi 20 walizokuwa
wametengewa asasi za kiraia, majina matano ni ya wanasiasa na makada wa
CCM.
Alitolea mfano kwa Kingunge Ngombale Mwiru, akisema ameingizwa
kwenye kundi la asasi wakati hajawahi kuwa na asasi wala hawajawahi
kumshuhudia hata kwenye msiba wa mwanaharakati mwenzao.
"Watuambie
Kingunge wamemtoa wapi na asasi yake ilisajiliwa wapi na inaitwaje...
mimi nimekuwa kwenye asasi kwa miaka 22, lakini sijawahi kumwona hata
kwenye msiba wa mwanaharakati mwenzetu, sasa iweje leo hii aibukie
kwenye kundi la asasi?" alihoji Mwakagenda na kuongeza;
"Huyo ni
kada wa siasa wa muda mrefu sasa ameingizwaje kwenye nafasi zetu?"
Alimtaja mwingine kuwa ni Elizabeth Minde, akisema licha ya kuwa na
asasi, lakini ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimajaro.
Alisema jina
lake lilitakiwa liwe kwenye kundi la wanasiasa na si kwenye asasi, kwani
sheria hairuhusu. Alimtaja mwingine aliyeingizwa kwenye nafasi zao kuwa
ni Sixtus Mapunda, ambaye ni Mwenyekiti wa UVCCM.
"Tumefanya
uchambuzi wa kina katika hayo majina na tumeagiza wenzetu wa Zanzibar
wayachambue ili kujua majina ya wanasiasa ambayo yameingizwa maeneo
ambayo si makundi yao," alisema na kuongeza; "Kwa mwelekeo huu kuna
uwezekano wa kupata katiba yenye mashaka."
Alisema asilimia 90 ya
wabunge wa Bunge la Katiba ni wanasiasa. Alisema tangu awali Jukwaa la
Katiba lilitaka Rais Kikwete, asifanye uteuzi huo kwani walijua atateua
wanasiasa wenzake ambao wataenda kuteka mchakato wa Katiba Mpya. watu
wenye mlengo unaofanana.
Wakati huo huo, jukwaa hilo limeandaa
mafunzo ya siku mbili kwa wabunge 201 ambao wamechaguliwa ili kuwapiga
msasa na kuwaelekeza hoja za kwenda kuingia nazo bungeni.
Alisema
katika mafunzo hayo Profesa Issa Shivji atafundisha namna kujenga hoja
kuhusiana na maudhui ya bunge hilo la Katiba, kwani katika bunge hilo
hakuna upande wa Serikali, vyama wala waziri.
Kwa upande wake
mkurugenzi wa mtadao wa watetezi wa haki za binadamu,Onesmo Olengurumwa,
alisema wamesikitishwa sana na Rais Kikwete, kutochagua kundi lao kwani
hakuna hata mmoja aliyechaguliwa kwa ajili ya kutetea haki za binadamu.
Alitoa mfano kuwa mauaji yaliyotokea wakati wa Operesheni Tokomeza
yalisababisha vifo vya watu wengi na wengine kukosa haki zao za msingi,
lakini kwa jinsi Rais Kikwete, alivyofanya uteuzi wa wabunge hao ni wazi
kuwa hakuna wa kwenda kuwatetea.
Alisema waliochaguliwa ni kundi
kubwa la chama kimoja linaloenda kupitisha katiba hiyo, wakati suala
hilo ni la Watanzania wote na si la vyama wala Serikali.
Chanzo;majira
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment