MAHAKAMA
ya Hakimu Mkazi Kisutu jana imeendelea kusikiliza kesi tatu
zinazowakabili vigogo kuhusiana na matumizi mabaya ya madaraka, huku
maofisa Suma JKT wakipatikana na kesi ya kujibu.
Kesi hizo
zilisikilizwa na Mahakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar
es Salaam jana, ambapo mashahidi waliendelea kutoa ushahidi wao katika
kesi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS),
Charles Ekelege na aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Ndege Tanzania
(ATCL), David Mattaka.
Akitoa ushahidi huo mbele ya Hakimu Mkazi
Kisutu wa Mahakama ya Kisutu, Augustina Mmbado,shahidi huyo alidai
mshtakiwa huyo ulikiuka kanuni za fedha.
Akiongozwa na Mwendesha
Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Janeth
Machulya, alidai kitendo cha Mkurugenzi huyo wa zamani wa TBS kutoa
msamaha bila ya kupata kibali cha Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo ni
kukiuka kanuni za fedha
Ekelege anakabiliwa na kesi ya matumizi
mabaya ya madaraka, kwa kuyaondolea ada ya asilimia 50 kampuni ya Jaffar
Mohamed Ali na Quality Motors bila ya kupata kibali cha Bodi.
Alidai
kuwa licha ya kukiuka kanuni za fedha,wakati wa kikao cha Bodi ya
Wakurugenzi cha Juni 30, 2011, Ekelege alikiri kosa hilo na kwamba
Mwenyekiti wa Bodi, alimsamehe na kuonya kosa kama hilo lisirudiwe tena.
Aliongeza kuwa mwaka 2007/2009, alikuwa Meneja wa Fedha na Utawala
na kwamba majukumu yake yalikuwa ni kusimamia masuala ya fedha, utawala,
rasilimali watu, manunuzi na matengenezo.
Shahidi huyo alidai kuwa
mfumo wa kiutendaji wa TBS ulikuwa ukiongozwa na Mkurugenzi, mameneja
wawili na wakuu wa Idara wanne ambao kwa pamoja waliunda timu ya
utawala.
Kuhusu taratibu za kifedha,shahidi huyo wa upande wa
mashtaka alidai kuwa zilikuwa zinaongozwa na kanuni za fedha za 2005
ambazo zilitumika hadi mwaka 2010 na kwamba zilikuwa na ukomo katika
fedha, matumizi ya maendeleo, uzalishaji mali ya umma na kusamehe
madeni.
Aliendelea kuwa ili kutoa msamaha ni lazima uangaliwe uwezo
wa mhusika, jitihada alizotumia kuomba msamaha na kwamba ni lazima
maombi hayo yapelekwe kwa Mkurugenzi ambaye atayapeleka kwa Mhasibu Mkuu
naye atapeleke kwa Mkaguzi wa Ndani ambaye atapitia na kutoa
mapendekezo au vigezo kama vinakidhi kusamehe.
Alidai kuwa hakuwahi
kufahamu kama mkurugenzi wake, Ekelege aliziondolea ada ya asilimia 50
kampuni hizo hadi alipoona ripoti ya mkaguzi wa ndani ya mwaka
2008/2009.
Ekelege anadaiwa kuwa Machi 28, 2008 akiwa Mkurugenzi
Mkuu wa TBS kwa nia mbaya alitumia madaraka yake vibaya kwa kuziondolea
kampuni hizo ada yenye thamani ya Dola 42,543 za Marekani
(sh.68,068,800).
Machulya alidai mshtakiwa aliziondolea ada kampuni hizo bila idhini ya Baraza la Utendaji kinyume na utaratibu wa TBS.
Katika
shtaka la pili, anadaiwa kutokana na kitendo hicho mshtakiwa
alisababisha hasara ya Dola 42,543 za Marekani. Mshtakiwa huyo alikana
mashtaka hayo na yupo nje kwa dhamana.
Kesi ya Suma JKT
Kwa
upande wa kesi ya matumizi mabaya ya madaraka inayowakabili vigogo wa
Suma JKT, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaona washtakiwa hao wana
kesi ya kujibu, hivyo wataanza kujitetea Machi 11 na 14, mwaka huu.
Hakimu Mkazi Aloyce Katemana, alisema kuwa washtakiwa hao wameonekana na kesi ya kujibu hivyo wawe tayari kujitetea.
Washtakiwa
katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Uchumi la Jeshi
la Kujenga Taifa (SUMA JKT), Kanali Ayoub Mwakang’ata Luteni Kanali
Mkohi Kichogo, Luteni Kanali Paul Mayavi, Meja Peter Lushika, Sajenti
John Lazier, Meja Yohana Nyichi na Mkurugenzi wa Miradi ya Matrekta wa
shirika hilo, Luteni Kanali Felex Samillan
Kesi ya Mattaka
Kwa
upande mwingine, ushahidi katika kesi ya matumizi mabaya ya madaraka na
kununua magari ya mitumba kinyume na Sheria ya manunuzi ya umma ya mwaka
2004 inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Ndege (ATCL),
David Mattaka na wenzake umeendelea kutolewa mahakamani hapo.
Akitoa
ushahidi wake, mbele ya hakimu Augustina Mmbando, shahidi AD,
Bathorimeo ambaye ni Operation Meneja wa Bondade Ware House of
Customers, alidai kuwa alipelekewa barua ya wito iliyomtaka apeleke
ripoti iliyoonesha muda wa kutoa magari, kuingia na gharama za kufanya
matengenezo.
Alisema kati ya magari yaliyoingizwa 15 yalitolewa na
magari 9 yalibaki, ambapo ATCL ilikuwa tayari imepunguza deni kwa kiasi
cha dola za Marekani 48,250 hadi kufikia Desemba mwaka 2011, ambapo
mpaka sasa magari 9 yamehifadhiwa Mbagala yanasubiri kulipiwa ushuru wa
forodha, ambapo kila gari litatozwa dola 250 kila mwezi hadi kufikia
Novemba mwaka 2013 ATCL ilikuwa inadaiwa dola 129,000.
Alidai magari
yalihifadhiwa katika kampuni yao kutokana na ukosefu wa fedha kwa kuwa
yangeachwa bandarini yangelazimika kulipiwa dola 1,200 kwa mwezi ambapo
kwa siku yangelipiwa dola 25 hadi 45.
Katika kesi hiyo Mattaka anatetewa na wakili Peter Swai na Alex Mgongolwa, ambapo wakili wa Serikali ni Shedrack Kimaro.
Kesi
hiyo imeahirishwa hadi Februari 25, mwaka huu. Novemba 22 mwaka huu,
Mattaka, Kaimu Ofisa Mkuu wa Kitengo cha Fedha Elisaph Mathew Ikomba na
Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Ndani, William Haji walifikishwa mahakamani
hapo kwa mara ya kwanza wakikabiliwa na makosa kushindwa kutunza
kumbukumbu za mawasiliano ya manunuzi waliyokuwa wakifanya na mtoa
huduma kinyume na kifungu cha 55(3),87(1)(f) cha Sheria ya Manunuzi ya
Umma Na. 21 ya mwaka 2004 na Kanuni ya 17(1) ya Sheria ya Manunuzi.
Wakili
wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) alidai shtaka la
pili ambalo linawakabili ni la kushindwa kutimiza matakwa ya vifungu
vya Sheria ya Manunuzi ya Umma na Kanuni zake kinyume na kifungu cha
87(1)(f) cha Sheria ya Manunuzi ya umma ya mwaka 2004.
Shtaka la
tatu linalomkabili Mattaka peke yake ni matumizi mabaya ya madaraka
kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya
mwaka 2007 ambapo Mattaka alitoa idhini ya kununuliwa kwa magari hayo
bila ya kuwepo kwa mkataba wa pande zote mbili na bila idhini ya Bodi ya
ATCL
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment