Home » » Kova aja na mtaa kwa mtaa

Kova aja na mtaa kwa mtaa

Kamishna wa Polisi, Suleiman KovaJESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limeanzisha programu huru ya mtaa kwa mtaa dhidi ya uhalifu ambao unajitokeza mara kwa mara.

Programu hiyo itawahusisha wenyeviti wote wa serikali za mitaa pamoja na askari, yenye lengo la kuboresha masuala ya usalama katika Jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana wakati wa ufunguzi wa programu hiyo ambayo imeanza katika Mkoa wa Ilala, Kamishna wa Polisi, Suleiman Kova, alisema wameamua kufanya hivyo wakiamini kwamba katika kila mtaa watu wanaofanya uhalifu wanajuana.
Alisema serikali za mtaa watashirikiana na polisi kushughulikia vitendo vya uhalifu kwani wapo karibu na wananchi.
“Tunaamini kwamba bila ushirikiano kati ya viongozi mbalimbali na polisi ulinzi hauwezi kuimarika, hivyo kwa kufanya hivi imani yangu uhalifu utaisha kabisa kwani kila mtaa utajitegemea katika ulinzi wake chini ya mwenyekiti wa serikali ya mtaa,” alisema.
Hata hivyo, Kova alisema wataandaa tuzo na kushindanisha mtaa kwa mtaa ambapo ule utakaokuwa umefanikiwa kudhibiti uhalifu kwa kiasi kikubwa utapata zawadi.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Gerezani, Ramadhani Matibwa, alisema wakiwa kama viongozi wanawajua wahalifu hivyo kwa mpango huo utasaidia kupunguza wahalifu na kuwarahisishia kazi Polisi.
“Tumefurahi sana kwani uhalifu ulikuwa umekithiri sana, kwa kuwa kila mtaa utajitegemea katika ulinzi wake utarahisisha upatikanaji wa taarifa kuliko zamani ilikuwa mpaka upige simu polisi,” alisema.
chanzo;Tanzania Daima
Like page yetu bofya hapa: www.facebook.com/blogszamikoa

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa