Home » » Mzazi aeleza ukatili aliofanyiwa mwanaye

Mzazi aeleza ukatili aliofanyiwa mwanaye

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Jamal Salum (12), mtoto ambaye aliuawa na Mohamed Said (36) ambaye ni Mwalimu wa Shule ya Awali na Madrasa ya Al Nur Al eneo la Mbagala Charambe Foma, inadaiwa alitobolewa macho kabla ya kuchinjwa na mtuhumiwa huyo.
Akizungumza nyumbani kwake eneo hilo, Dar es Salaam jana, baba wa mtoto huyo, Salum Ally alikanusha mtoto huyo kuwa mwanafunzi katika madrasa ya mtuhumiwa.
Ally alisema siku ya tukio akiwa anarudi kazini saa 11 jioni, alipopita eneo hilo la madrasa aliona umati wa watu umezunguka eneo hilo na alishangaa kabla ya kuendelea na safari yake.
Alisema baada ya kufika jirani na nyumbani kwake, alipishana na mkewe akilia huku akikimbilia eneo la tukio, akipiga kelele kuwa mtoto wao Jamal kachinjwa.
Mama wa marehemu, Halima Selemani alisema siku ya tukio, marehemu baada ya kujaladia madaftari yake na mwenzake aitwaye Ramadhani waliondoka akimtaka amsindikize kwa mjomba wake eneo la jirani na hapo akachukue kalamu.
Alisema rafiki yake alimhimiza mwenzake waondoke, huku yeye akiwa ametangulia ndipo mwalimu huyo alipomshika mkono marehemu na kuingia nae ndani na mwenzake alirudi na kukuta ameshikwa mkono na ndipo alipoanza kumsihi amwachie.
“Alimsihi sana amwachie kwani hajui kosa lake, lakini mwalimu huyo hakumsikiliza badala yake akaanza kumchoma kwa kisu machoni na usoni,” alisema.
Mtoto huyo alizidi kumwombea mwenzake, lakini akiwa hajui lolote alimshuhudia mwalimu huyo akimchinja mwenzake.
Mwili wa mtoto huyo ulizikwa juzi makaburi ya kwa Mbiku, wakati mwalimu huyo akizikwa kwao Kisiju Pwani. Baadhi ya majirani walidai ndugu za marehemu waliwasilisha cheti polisi mwaka 2007 kuwa aliugua ugonjwa wa akili.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema alifika nyumbani kwa marehemu Jamal na kuwataka ndugu kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na kuiasa jamii kutowaficha watu ambao wana matatizo hususan yale ya akili.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa