Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) linakusudia kuteketeza
kinywaji chenye ladha ya matunda (juisi) kijulikanacho kwa jina la
Smile, baada ya kubaini kuwa hakina viwango vinavyohitajika.
Akizungumza jana Dar es Salaam, Kaimu Mkuu wa
Kitengo cha Kudhibiti Ubora wa Bidhaa wa TBS, Ashura Katunzi alisema
maofisa wa shirika hilo walipata taarifa kutoka kwa walaji kuhusu juisi
hiyo inayotengenezwa na Kampuni ya A One Products and Bottlers Ltd,
ambayo ni miongoni mwa kampuni tanzu za Mohamed Enterprises.
“Maofisa wa TBS walikwenda kufanya ukaguzi kwenye
kiwanda eneo la Vingunguti, Dar es Salaam Januari 20 mwaka huu, na
walichukua sampuli ya juisi mbili ya Smile na Pride zenye ladha ya
machungwa kwa ajili ya kuzichunguza, kabla ya kubaini kutokuwa na
viwango vinavyotakiwa,” alisema.
Alisema gharama za kuteketeza juisi hiyo
zitatolewa na kampuni husika, kwa sababu TBS haipo tayari kuona bidhaa
ambazo hazijakidhi kiwango cha ubora zinaendelea kusambazwa sokoni.
Mwenyekiti wa Kampuni ya Mohamed Enterprise, Gulam
Dewji akizungumzia suala hilo, alisema walishakubaliana na TBS
kutopelekwa sokoni juisi hiyo na walitoa cheti cha ubora wa kuendelea
kuzalisha nyingine kwa kiwango kinachotakiwa.
“Nachofahamu ni kwamba kulikuwa na makubaliano na
TBS kuhusu ubora wa juisi hizi, tulikubali kuzalisha nyingine badala ya
hizi,” alisema Dewji.
“Njoo nikuonyeshe vyeti vya TBS, tayari wametupa
maelekezo tuliyaelewa na cheti cha kuthibitisha ubora wa juisi hiyo
tayari wametupatia,” alisema Dewij.
Akifafanua zaidi Ofisa Viwango wa TBS, Zena Issa
alisema kwa kawaida kinywaji cha aina hiyo, kinapaswa kuwa na kiasi cha
sukari 10, lakini yenyewe ilipopimwa ilikutwa na kiwango 2.5.
“Pamoja na kuwa kwenye hali hiyo, bado juisi hii
siyo sumu kwa watumiaji, ila ilipaswa kuwa na kiwango kinachokubalika
cha sukari kama taratibu za ubora zinavyoonyesha,” alisema.
Aliongeza: “Kwa kuwa bidhaa hii inatumika zaidi na
watoto pengine na wagonjwa, ilipaswa kuwa na virutubisho vitarajiwa kwa
mnywaji, siyo hii ambayo ni kama maji yaliyowekwa rangi na ladha tu
basi,” alisema.
Mwanasheria wa shirika hilo, Baptista Bitao
alipohojiwa ni adhabu gani wanazokusudia kuchukua dhidi ya kampuni hiyo,
alijibu kwamba Sheria ya Viwango namba 2 ya mwaka 2009 inaeleza wazi
hatua zinazotakiwa kuchukuliwa.
“Kuna sheria husika kwa makosa kama haya ya kuzalisha bidhaa chini ya kiwango kinachohitajika,” alisema Bitao.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment