Home » » Uamuzi kesi ya AG, Pinda kutolewa Aprili 17

Uamuzi kesi ya AG, Pinda kutolewa Aprili 17

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Aprili 17 mwaka huu, itatoa uamuzi wa kuifuta au kuendelea na kesi ya kikatiba inayomkabili Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Kesi hiyo ilikuja mahakamani hapo jana ambapo juzi, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, aliomba kufutwa kwa kesi hiyo ambayo imefunguliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS).
Katika kesi hiyo namba 24 ya mwaka 2013, LHRC na TLS, wanadai Bw. Pinda alivunja Katiba kutokana na kauli aliyoitoa bungeni Mjini Dodoma, kuhusu Polisi kuwapiga raia ambao watakaidi amri.
Hata hivyo, AG ambaye aliunganishwa katika kesi hiyo, waliweka pingamizi la awali akidai walalamikaji na watu walioorodheshwa katika kesi hiyo hawana mamlaka kisheria ya kumfungulia kesi.
Awali, Masaju alisema, sheria inamlinda Waziri Mkuu kutoshtakiwa wala kuhojiwa na chombo chochote juu ya kauli aliyoitoa bungeni; hivyo kesi hiyo ni batili na iko mahakamani isivyo halali.
Alisema kufunguliwa kwa kesi hiyo ni ukiukwaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, Sheria ya Mamlaka, Kinga na Haki za Wabunge ya mwaka 1988.
Akifafanua hoja hiyo, Masaju alisema Bw. Pinda analindwa na
Katiba Ibara ya 100 (1) na (2) inayosema, "kutakuwa na uhuru wa mawazo na majadiliano bungeni, ambao hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo chochote au katika mahakama yoyote nchini.
Ibara ya pili inasema "mbunge yeyote hatashtakiwa au kufunguliwa shauri la madai mahakamani kwa jambo lolote alilolisema, alilolitenda au alililoliwasilisha bungeni kwa njia ya maombi, muswada, hoja au vinginevyo".
Aliongeza kuwa, msingi wa shauri hili unatokana na jambo lililosemwa bungeni na mmoja wa wabunge wakati wa shughuli za bunge.
Kesi hiyo ipo chini ya jopo la majaji watatu ambao ni Jaji Kiongozi Fakh Jundu, Augustino Mwarija na Dkt. Fauz Twaib.

Chanzo;majira

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa