Upanuzi wa Gati namba 13 na 14 katika
Bandari ya Dar es Salaam, uliosababisha kung’olewa kwa aliyekuwa Waziri
wa Uchukuzi, Omary Nundu, umeendelea kupata vikwazo baada ya kampuni ya
Kichina iliyopewa zabuni ya upanuzi huo kutofika kwa kazi hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari(TPA), Madeni
Kipande aliiambia Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali(PAC),
iliyofanya ziara jana katika bandari hiyo kuwa hatua hiyo licha ya
kuwasikitisha imesababisha kuchelewa kwa upanuzi huo.
“Hiyo kampuni ya kichina ilitakiwa iwe imeanza
kazi tangu Oktoba mwaka jana, lakini ajabu ni kwamba ipo kimya na
hakuna mawasiliano ya aina yoyote. Tumeamua kufuta zabuni hiyo,
tutatangaza nyingine mapema mwezi huu kwa kuwa tunakusudia kwamba, Julai
tuwe tumeshaanza kazi. Hapa hatutaki siasa zimetuchosha,” alisema
Kipande.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Kabwe Zitto
aliisisitiza TPA kuhakikisha kwamba zabuni hiyo inatangazwa na
kukamilika mapema akieleza kuwa kuendelea kuchelewesha kuanza kwa
upanuzi huo ni kuikosesha mapato Serikali.
“ Upanuzi huo ni muhimu sana kufanyika kwa sababu
ukikamilika ndiyo unaoweza kuweka ushindani na Bandari ya Mombasa, pia
itasaidia kuiongezea mapato Serikali,” alisema Zitto.
Kamati hiyo pia ilisisitiza TPA kuhakikisha
inaanza matumizi ya kupakua mafuta kwa njia ya mita kwa sababu utaratibu
wa kupima kwa kijiti(Dip Stick) unaikosesha mapato Serikali.
“ Katika hili tumeamua kuunda kamati maalumu,
itakayofuatilia kwa kina kubaini kwa nini tangu utaratibu huo ulipopaswa
kuanza kutumika mwaka 2008 umekuwa ukipigwa danadana. Tunahisi kuna
jambo, inawezekana hata ni hujuma za wafanyabiashara wa mafuta, tutaujua
ukweli,” alisema Zitto.
Akiwa Waziri wa Uchukuzi, Dk Shukuru Kawambwa kwa
kushirikiana na Mamlaka ya Bandari, walitafuta mkopo kutoka Serikali ya
China kupitia Benki ya Exim ya nchi hiyo iliyoridhia kutoa Dola 524 za
Marekani ili zisaidie upanuzi wa Gati namba 13 na 14 katika Bandari ya
Dar es Salaam.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment