Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WIZARA
ya Maliasili na Utalii, jana imekamilisha mchakato wa kulipa kodi ya
ushuru kwa Mamlaka ya Mapato nchini ili kuruhusu upatikanaji wa silaha
500 aina ya AK 47 ili ziweze kukabidhiwa kwa wapiganaji kwenye Hifadhi
za Taifa, Mamlaka ya Ngorongoro na Mapori ya Akiba kote nchini ili
kupambana na ujangili.
Silaha hizo zilizuiliwa na TRA tangu Novemba
2012 baada ya Wizara hiyo, kushindwa kuzilipia ushuru wa sh. milioni 212
walizokuwa wakidaiwa kama ushuru ili waweze kuzipata.
Waziri wa
Maliasili na Utalii, Bw. Lazaro Nyalandu, aliyasema hayo Dar es Salaam
jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo kufanikiwa kwa
mchakato huo ni utekelezaji wa azimio la Bunge na ahadi ya Serikali kwa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maliasili, Ardhi na Mazingira.
"Silaha
hizi zilinunuliwa kwa gharama ya sh. milioni 427, leo natangaza
kuzipandisha hadhi kanda nane zilizopo katika pori la Akiba la Selous
ili ziweze kujitegemea kiuendeshaji kwa kuwa na viongozi wake kila
kanda.
"Pori la Selous lina ukubwa wa kilometa za mraba 55,000
unaokaribia Hifadhi zote za Taifa nchini zilizopo chini ya TANAPA,
ambazo zina ukubwa wa kilometa za mraba 57,000," alisema Bw. Nyalandu.
Aliongeza
kuwa, Mhifadhi Benson Kibonde ataendelea kuwa Meneja wa pori lote la
Selous kama ilivyo sasa akisaidiwa na wakuu nane wa kanda.
Wakuu hao
ni Msafiri Mashiku (Kanda ya Matambwe), Asterius Ndunguru (Msolwa),
Adili Zella (Liwale), Bigilamungu Kagoma (Kingupira), William Millya
(Kalulu), Munhu Ndunguru (Miguruwe), Ramadhani Mkhofoy (Ilonga) na Msiba
Kombo (Likuyu- Sekamaganga).
Bw. Nyalandu alisema Wizara yake pia
imechukua hatua za kuimarisha kikosi cha kupambana na ujangili nchini
(KDU), katika kanda nane zikiongozwa na wakuu wake.
Aliwataja wakuu
hao kuwa ni Paskal Mrina (Kanda ya Kaskazini- Arusha), Faustine Masalu
(Mashariki-Dar es Salaam), John Mbwiliza (Serengeti-Bunda), Benjamin
Kijija (Kanda ya Ziwa- Mwanza) na Charles Msilanga (Magharibi-Tabora).
Wengine ni Keneth Sanga (Kanda ya Kati-Manyoni), Majid Lalu (Nyanda za Juu Kusini-Iringa) na Ibeid Mmari (Kusini-Songea).
Alisema
katika kuimarisha ulinzi wa tembo na mapambano dhidi ya ujangili katika
Pori la Akiba la Selous, aliishukuru Frankfurt Zoological Society kwa
kuwapa magari matano aina ya Land lover.
Magari hayo yatapelekwa
katika kanda za Matambwe, Msolwa, Kiwale, Kingupira, Kalulu na kuongeza
kuwa, Mfuko wa Wanyamapori umenunua magari 14 aina ya Toyota yenye
thamani ya sh. bilioni 1.63.
Katika hatua nyingine, Bw. Nyalandu
amemteua Bw. Nurdin Chamuya kuwa msemaji wa Wizara hiyo akichukua nafasi
ya Bw. Chikambi Rumisha ambaye anarudi katika idara yake ya Sera na
Mipango.
"Wizara yangu inachukua hatua mahususi kuwajengea uwezo
watumishi wake na askari wanyamapori ili kushinda vita kubwa ya ujangili
nchini," alisema Bw. Nyalandu.
Chanzo;majira
0 comments:
Post a Comment