Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira
Wassira aliyasema haya baada ya Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, kutembelea Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango kukagua uratibu wa utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Idadi ya Watu.
Alisema ongezeko hilo linachochea mitafaruku mbalimbali kwa kuwa mahitaji ya matumizi ya ardhi yanaongezeka kila uchao.
“Mwaka 1961, kulikuwa na Watanzania milioni tisa tu, sasa tupo takribani milioni 45 na ukubwa wa ardhi ni ule ule,” alisema.
Wassira alisema kuna haja ya kupanga matumizi mazuri ya ardhi ili kukidhi mahitaji ya sasa na kizazi kijacho. Akijibu baadhi ya maswali ya wabunge ambao ni wajumbe wa kamati hiyo waliotaka kujua msimamo wa Tume ya Mipango katika changamoto ya matumizi ya ardhi, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dk. Philip Mpango, alisema kuna umuhimu mkubwa wa kupima ardhi ya nchi na kubainisha matumizi yake.
Mpango alisema kutokana na maendeleo na teknolojia ya upimaji ardhi kwa sasa, inawezekana kupima ardhi kwa muda mfupi na kupanga ipasavyo. “Tuwekeze zaidi katika ardhi maana hakuna maendeleo yanayoweza kufanyika bila ardhi,” alisema.
Kuhusu mkakati wa mradi wa uratibu wa utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Idadi ya Watu ulioanzishwa mwaka 1986, Wassira alisema mradi huo ulianzishwa kwa ajili ya kuratibu maendeleo ya Sera ya Taifa ya Idadi ya Watu. “Mradi huu unafadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) ambalo limekuwapo hapa nchini tangu mwaka 1971 likifadhili miradi mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani,” alisema.
Kwa mujibu wa Msimamizi Mkuu wa mradi huo ambaye ni Naibu Katibu Mtendaji (Idadi ya Watu na Huduma za Jamii), Florence Mwanri, utekelezaji wa mradi huo unakabiliwa na changamoto nyingi.
“Masuala ya idadi ya watu bado hayajulikani vizuri miongoni mwa wananchi/wadau kupanga masuala mbalimbali katika kila ngazi,” alisema.
Akitaja mafanikio ya mradi huo, Mwanri alisema kwa kushirikisha wadau mbalimbali mradi umefanikiwa kupitia Sera ya Taifa ya Idadi ya Watu ya mwaka 1992 na kuandaa sera mpya ya mwaka 2006 na mkakati wake wa mwaka 2007 ambao unatoa mwongozo kwa sekta mbalimbali kuzingatia na kuweka kipaumbele katika masuala ya idadi ya watu katika mipango na bajeti.
Aidha, masuala ya idadi ya watu hususan takwimu zimekuwa zikitumika kwa kiwango kikubwa katika mipango na bajeti kwa mikoa na halmashauri. Mafunzo ya masuala ya idadi ya watu, mazingira na jinsia katika vyuo vikuu vya Dar es Salaam na Mzumbe na Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Dodoma.
Ziara hiyo iliongozwa na Mwenyekiti mpya wa Kamati hiyo, William Ngeleja, ambaye aliwapongeza watendaji wa Tume ya Mipango kwa kazi wanazozifanya za kupanga kwa ajili ya taifa na kuongeza na kwamba wazidishe bidii ili kuiletea Tanzania maendeleo makubwa.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment