Home » » Bunge lafyeka 26% ya muda wake

Bunge lafyeka 26% ya muda wake

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi (kushoto), akizungumza na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni ambaye pia ni Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Freeman Mbowe, wakati wa kikao cha Bunge hilo mjini Dodoma jana. Picha/Selemani Mpochi
Bunge Maalum la Katiba, jana liliingia siku ya 21, huku likiwa limekaa vikao viwili tu vya Bunge na siku 16 zikitumia kujadili Rasimu ya Kanuni za kuongoza Bunge hilo na siku tatu ni za Jumapili zilizokuwa na mapumziko.
Muda huo wa siku 18 ambao limekaa vikao ni takribani asilimia 26 ya muda wa siku 70 ambazo Bunge hilo limepangiwa kukutana kama hazitaongezwa nyingine 20 endapo halitamaiza shughuli zake kwa muda huo.

Hata hivyo, muda huo wote umetumika katika kujadili Rasimu ya Kanuni za kuendesha bunge hilo, wananchi wengi wakiamini ni kupoteza muda na fedha ilhali wabunge wakisisitiza kuwa kanuni ndiyo msingi wa bunge hilo hivyo muda huo halali kutumika.

Kutokukamilika kwa kanuni hizo kumekwamisha uchaguzi wa Mwenyekiti wa kudumu na makamu wake, viapo vya wajumbe pia uteuzi wa kamati 12 za Bunge Maalumu, ufunguzi wa Bunge, uwasilishaji wa Rasimu ya Katiba na mjadala wa Rasimu ya Katiba kuanza.

Kwa mujibu wa Kanuni, siku za vikao ni kuanzia Jumatatu hadi Jumamosi isipokuwa Jumapili na siku za mapumziko.

Kwa mujibu wa kalenda ya mwaka 2014, kutakuwapo na siku sita za sikukuu ambazo ni Jumatatu ya Pasaka, Mei Mosi, Siku ya Muungano, Kuumbukumbu ya Karume na Ijumaa Kuu huku siku za Jumapili zikiwa 10.

Wajumbe wa bunge hilo waliwasili mkoani Dodoma kuanzia Februari 16, mwaka huu na Februari 18, mwaka huu Bunge hilo lilianza mkutano wa maelekezo ya ukaaji na jiografia ya ukumbi.

Februari 18, mwaka huu saa 8:00 mchana, aliyeteuliwa Olive Luena, kukalia kiti cha Spika na kuongoza mchakato wa kumpata mwenyekiti wa muda.

Walijitokeza wagombea watatu ambao ni Pandu Ameir Kificho aliyepata kura 393, Prof. Costa Mhalu aliyepata kura 84 na Mangdalena Rwebangira aliyepata kura 84.

Mwenyekiti wa muda Kificho alisoma tangazo la kuitisha Bunge Maalum na hotuba yake ya ufunguzi.
Februari 19, mwaka huu, Mwanasheria Mkuu wa serikali, Jaji Fredrick Werema, aliwapa elimu ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Rasimu ya Kanuni za Bunge hilo na baadaye liligeuka kama semina, kisha mwenyekiti akaunda Kamati ya Kanuni na Kumshauri Mwenyekiti wa muda.

Februari 20, mwaka huu, wajumbe waliendelea na semina na waliomba muda wa siku tatu kusoma kanuni hizo na siku tatu za majadiliano, lakini hadi jana Machi 10, mwaka huu mjadala wa kanuni ulikuwa haujafikia mwisho ingawa vifungu 85 kati 87 vimepitishwa huku vifungu vya 37 na 38 vinavyohusu upigaji kura vikiendelea kuwa tete.

Hata hivyo, kwa siku nne wajumbe hao walishindwa kuendelea na semina kutokana na mvutano mkali baina yao katika kupitisha kanuni hizo na mara zote semina hiyo ilihairishwa.
Machi 07, mwaka huu, wajumbe walikutana saa nne asubuhi na baada ya nusu saa lilihairishwa kwa kuwa kamati ya maridhiano iliyoundwa kutafuta namna bora ya kushughulikia vifungu vya 37 na 38 vya kanuni mwafaka ulishindikina.

Jana kikao kilianza saa sita badala ya saa 5 asubihi kama mwenyekiti alivyokuwa ametangaza, na aliwaeleza wajumbe kuwa kanuni hizo zitapitisha zikiwa na vifungu hivyo ambavyo vitashughulikiwa baadaye.

Hali hiyo ilizua mjadala mkali na mwenyekiti alihairisha kikao hadi saa 10 jioni ambapo walikutana wakiwa katika muundo wa Bunge Maalum la Katiba na muda mfupi kuahirishwa kwa ajili ya kuwapatia fursa wajumbe kusoma kanuni zilizofanyiwa masahihisho hadi leo saa 3:00 asubuhi kwa ajili ya kupitisha azimio la kupitisha Rasimu ya Kanuni.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa